Linapokuja swala la malezi bora ya watoto, kila mzazi anakuwa njia panda kwa sababu hakuna mtaala maalumu unaotolewa wa kuwaandaa watu kutoa malezi bora. Kama hiyo haitoshi, watoto pia hawaji na kitabu cha maelekezo kama ambavyo ukinunua kitu kipya unapewa. Na kufanya mambo kuwa magumu zaidi, watoto wanatofautiana na hivyo hata kama una watoto wengi, bado malezi ya kila mmoja ni tofauti.
Mwandishi na mshauri wa malezi Kim John Payne anatupatia mwongozo bora wa kuwapa watoto malezi bora kupitia kitabu chake Simply Parenting. Hapa nimekushirikisha mambo 20 muhimu sana niliyojifunza kwenye kitabu hiki. Karibu tujifunze na kuchukua hatua ili kuwaandaa watoto wetu vizuri.
1. Dhumuni la kila mzazi ni kuona familia yake inakwenda vizuri. Kila mzazi anapenda watoto wake wapate malezi bora na kuweza kufanikiwa kwenye maisha. Lakini sio wazazi wote wanaweza kufikia dhumuni hilo, na hii inatokana na changamoto za kila siku za maisha ambazo zinaingilia mipango mizuri ya maisha.
2. Wazazi ndio mwongozo wa familia. Yale maisha ambayo wazazi wanaishi yana athari kubwa kwa watoto wao. Na kwa sababu mara nyingi wazazi wanaishi maisha yao bila ya kujua wanayofanya yana athari kiasi gani kwa watoto, athari hizi hupelekea maendeleo ya watoto kutokuwa mazuri.
3. Watoto wanakuwa na furaha sana pale wanapopewa nafasi ya kujifunza na kuivumbua dunia wao wenyewe. Pale ambapo wanapata nafasi ya kujifunza kupitia mazingira yanayowazunguka na kwa njia hiyo wanakua kifikra.
4. Dunia ya sasa inakwenda kasi sana, kila mtu anakazana kupata zaidi, kuwahi zaidi na kuwa na vitu vingi zaidi. Kwa dunia hii ya wingi, watoto nao wanasukumwa kuwa na vingi, kitu ambacho kinawachosha kabla ya muda wao. Watoto wanalazimika kuingia kwenye dunia hii ya wingi kutokana na jinsi wazazi wao wanavyoishi.
5. Watoto wamekuwa wakikumbwa na msongo wa mawazo unaotokana na kupata taarifa ambazo sio za ngazi yao. Dunia ya sasa habari zipo nyingi sana, na habari nyingi ni hasi. Mtoto mdogo anapopokea habari hizi zinamchanganya kabisa na kuathiri ukuaji wake. Badala ya kukua akiwa chanya na mwenye mategemeo makubwa, anakua akiwa hasi na mwenye kukata tamaa.
6. Kuwalinda sana watoto na kutaka kuwaepusha na kila changamoto pia sio malezi mazuri. Mtoto anatakiwa kukutana na changamoto, hasa zile zinazoendana na uwezo wake wa kuelewa. Kupitia changamoto ndiyo anajifunza na kukua zaidi. Kumwepusha mtoto na changamoto zote ni kumwandaa kuja kushindwa baadae.
7. Maisha ya sasa yamewafanya wazazi wengi kuwa bize sana, na hii imepelekea kukosa muda wa kukaa na watoto wao ili kujua maisha yao yanakwendaje na kujua wakati ambapo wanapitia mambo magumu kwenye maisha yao.
8. Malezi bora ya mtoto yanaanzia kwenye kuyarahisisha maisha ya mtoto. Na sio kuyarahisisha kwa kumwondolea changamoto zote, bali kumwondoa kwenye hali hii ya sasa ya ulimwengu unaokwenda kasi. Kuyafanya mazingira ya mtoto, hasa ya nyumbani kuwa rafiki kwake na kumpa yeye nafasi ya kukua kadiri ya uwezo wake.
9. Magonjwa ya kisaikolojia ambayo yanawapata watoto, huwa yanaanzia kwenye msongo wa mawazo ambao unakuwa umejijenga ndani yao kadiri wanavyokua. Na msongo huu wa mawazo unatokana na kasi ya dunia, na watoto kukutana na mambo ambayo yako nje ya uwezo wao kuelewa.
10. Watoto wengi wanaogunduliwa kuwa na magonjwa ya akili, wanaweza kutibiwa magonjwa hayo kwa kubadili mazingira yao na kurahisisha maisha yao. Tafiti zilizofanywa zinaonesha watoto waliotibiwa kwa kubadili mazingira yao, walikuwa na matokeo mazuri kuliko waliotibiwa kwa madawa.
11. Utoto sio safari ya kufikia ukubwa, utoto ni kipindi cha maisha kinachojitegemea na hivyo mtoto anahitaji kupitia hatua zote za ukuaji. Kwa maisha ya sasa watoto wanalazimisha kukua kabla hata ya muda wao. Hii inatokana na habari wanazokutana nazo na pia ukuaji wa teknolojia. Hii imeongeza changamoto kwa wazazi.
12. Utoto ni wakati ambao mtu anataka kujifunza kwa kila kitu. Mtoto anapoona kitu anataka kukishika, anataka kukionja na hata kukijaribu kwa njia mbalimbali, hii ndio njia ya asili. Inapotokea mtoto amezungukwa na vitu vingi kwenye mazingira yake, atataka kujaribu kila kimoja na hivyo kujikuta anahangaika na kila kitu. Hali hii inaweza kumpelekea kuwa na msongo wa mawazo, hasa pale anapoona hawezi kujaribu kila kitu.
13. Tabia ya mtoto inajengwa na zile hali anazopitia na jinsi anavyoweza kuzivuka. Ukuaji wa mtoto ni kama utengenezaji wa kinga ya mwili, mtu anatengeneza kinga ya mwili pale anapopata ugonjwa. Hivyo pia mtoto anatengeneza tabia yake kutokana na magumu anayopitia. Ndio maana ni muhimu kwa mzazi kuhakikisha mtoto anakuwa kwenye mazingira bora yanayoendana na uwezo wake, na sio kujaribu kumzuia asikutane na changamoto.
14. Mzazi anapolazimisha mtoto akue kama anavyotaka yeye ndipo ambapo kunatokea mgogoro mkali sana kati ya mzazi na mtoto. Jukumu la mzazi sio kumlazimisha mtoto aendeje, bali kumpatia mwongozo mzuri wakule ambapo anataka kwenda. Kumwezesha mtoto kujenga tabia nzuri zitakazomwezesha kufikia mafanikio kwenye jambo lolote.
15. Kila mtoto anazaliwa na hatima ya maisha yake, na haifanani na mtoto mwingine yeyote. Kama ambavyo mbegu ya mbuyu ikioteshwa itatoa mbuyu wa kipekee, basi hata watoto wanakuja na mambo yao ya kipekee. Lakini wanapofika kwenye jamii, jamii inasahau utofauti wa watoto hawa na kukazana kuwafanya wawe sana na kila mtu. Kwa njia hii ndoto nyingi sana zinapotezwa. Ni jukumu la kila mzazi kujua ni kitu gani cha tofauti kilichopo ndani ya watoto wao, na wanaweza kukijua kama watapata muda wa kuwa karibu na watoto hao.
16. Ni muhimu sana kurahisisha mazingira ya mtoto, kwa kufanya hivi mtoto anakuwa amezungukwa na vitu vichache na hivyo kuwa na muda wa kutosha kudadisi na kujifunza kupitia vitu hivyo. Kama mtoto ana midoli mingi basi ni wakati wa kupunguza abaki na michache. Kama mtoto ana vitabu vingi basi punguza abaki na vichache, vile anavyovipenda sana. Kama nyumbani tv inawashwa masaa 24 na ni habari za wakubwa tu, badili mazingira hayo.
17. Kila mzazi, kabla hajaingia kwenye familia kuna ndoto alikuwa nayo uya jinsi gani alitaka familia yake iwe. Jinsi ambavyo alikuwa anaona familia bora kwake ikoje. Habari njema ni kwamba bado ndoto zile zinawezekana hata kama ni tofauti sana na maisha ya familia uliyonayo sasa. Pata muda wa kuzirudia tena ndoto zile na anza kuzifanyia kazi.
18. Utajuaje kama mazingira yamemharibu mtoto wako? Utaona mabadiliko kwenye tabia zake. Anaweza kuwa mtu wa kukasirika sana, au kuwa mtu wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, au anaweza kuwa halali vizuri usiku. Au kuonekana kujawa na hofu inayonyima furaha. Hapa unahitaji kuchukua hatua ili kuhakikisha mtoto wako anakuwa na ukuaji bora.
19. Watoto wanaoonekana ni watundu, hasa ule utundu wa kupitiliza, wengi inatokana na madhara haya ya mazingira. Watoto wengine hufanya makosa ili tu waonekane wapo (attention seeking). Na hii inakuwa imetokana na migogoro mingi ambayo wanakuwa wamepitia na inakuwa haijatatuliwa. Wewe kama mzazi ni vyema kujua ni mambo gani anapitia mtoto na kumsaidia kuyatatua ili awe na ukuaji mzuri.
20. Katika malezi bora, watoto wanahitaji muda wako kuliko wanavyohitaji fedha zako. Tunaishi kwenye dunia ambayo tunakazana kutafuta fedha nyingi na hivyo kukosa muda wa kukaa na watoto wetu. Unachotakiwa kujua ni kwamba fedha unaweza kuzitafuta zaidi, lakini huwezi kupata muda uliokosa kwenye ukuaji wa watoto wako. Ni vyema kutenga muda wa kutosha wa kuwa na watoto, kujua maisha yao, kujua wanapitia nini na kujua ni kipi cha tofauti wamekuja nacho.
21. Tafiti zilizofanywa kwenye nchi za wenzetu, zinaonesha kwamba wazazi wanapofanya kazi zaidi ya masaa 10 kwa siku, inaleta athari kwenye ukuaji wa watoto wao. Na wale wazazi ambao wanafanya kazi zaidi ya masaa 15 kwa siku, yaani wanakuwa mbali na watoto kwa karibu siku nzima, watoto hao wanaishia kwenye tabia hatarishi kama kutumia mihadarati, kuanza mapenzi katika umri mdogo, kufanya vibaya kwenye masomo na hata kujiua.
Kama mzazi, malezi bora ya mtoto wako ni jukumu lako kubwa. Usikubali kasi ya dunia ya sasa ikukoseshe muda wa kutekeleza jukumu hili. Pia usiruhusu kasi ya dunia hii iingie kwenye maisha ya mtoto wako, kwa sababu itamfanya apate msongo wa mawazo unaopelekea yeye kuwa na tabia hatarishi.
Kila la kheri.