Lengo la kuweka malengo siyo uyafikie yote kwa asilimia 100.
Lengo la kuweka mipango ya siku siyo kuikamilisha kwa silimia 100.
Japo kuna wakati unaweza kufikia vyote kwa asilimia 100, lakini sio mara zote unaweza kufikia hivyo.
Siyo vitu vyote vitaenda kama unavyotaka wewe. Sio kila kitu kitatokea kama ulivyotegemea. Hili ni jambo muhimu sana unalotakiwa kulijua ili uweze kwenda vizuri na maisha yako.
Kwa sababu tunategemea kupata kitu fulani, basi tunaweka mawazo yetu yote kama tayari tumeshakipata, hivyo inapotokea hatujakipata, na hii hutokea mara nyingi, tunajikuta tunaumia, kuchukia na hata kukata tamaa.
Ni muhimu kujua kwamba sio kila kitu kitakwenda kama unavyotaka, na hivyo unapoweka mipango yako, pia uwe na njia mbadala. Kama hiki kisipotokea basi nitafanya hivi. Usikubali kuwa na chaguo moja pekee, utakwama kwenye mambo mengi.
Na pia sio kila mtu atakuwa kama vile wewe unavyotaka, siyo kila mtu atafanya kama wewe unavyotaka afanye. Jiandae kwa hilo pia, pale unapopanga mambo yako ili usiishie kuangushwa na hatua watakazoamua kuchukua wengine.
Kubali kwamba huwezi kudhibiti kila kitu, kubali kwamba sio kila unachotegemea au ulichopanga kitatokea, na jiandae kuwa na machaguo mengi.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Jinsi Ya Kujenga Na Kuishi Maisha Yenye Maana.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba pamoja na kuweka malengo na mipango, siyo kila kitu kitakwenda kama nilivyopanga na ninavyotarajia. Najua pamoja na watu kukubaliana na mimi, sio wote watafanya kama walivyoahidi. Nimeshakubali hili na mara zote nitakuwa na njia mbadala ili nisikwame kutokana na yanayotokea.
NENO LA LEO.
“You can’t stop the waves, but you can learn to surf.” ~ Jon Kabat-Zinn
Huwezi kuyazuia mawimbi, ila unaweza kujifunza kuyatumia kwa burudani.
Huwezi kuzia vitu kutokea, au kulazimisha vitu kutokea. Ila unaweza kutumia vile vinavyotokea kwa manufaa yako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.