Kuna vitu vingi sana ambavyo huwa tunakuwa tunataka kufanya. Ila kwa sababu nguvu zetu na muda havitoshi, basi tumetengeneza njia nzuri sana ya kuweka pembeni vile ambavyo sio muhimu na kufanya vile ambavyo ni muhimu.

Ila njia hii huwa hatuijui kwa sababu huwa inafanyika kwa mazoea. Na kwa njia hii hii tumekuwa tunaitumia kutoroka au kushindwa kufanya yale ambayo ni muhimu kwetu, hasa kwa muda mrefu.

Njia ya uhakika kabisa ya kujua kama kitu ni muhimu kwako au la ni sababu. Kama kuna kitu ambacho unajua unataka kukifanya, lakini inapofikia kuchukua hatua unakuja na sababu, hata kama sababu ni nzuri kiasi gani, hiyo ni njia ya kuonesha kwamba kitu hiko sio muhimu kwako.

Yaani vile vitu ambavyo sio muhimu sana kufanya, ndivyo ambavyo huwa tunakuja na sababu za kutosha kwa nini hatuwezi kufanya kwa sasa. Lakini kitu kinapokuwa muhimu hasa, hakuna sababu yoyote inayokuzuia.

Tuchukulie mfano, labda kuna ripoti ya kazi unatakiwa uikamilishe siku ya ijumaa, na leo labda ni jumatatu. Ungeweza kuifanya leo, lakini unapata sababu kwa nini usifanye, labda umechoka, labda kwa sasa kuna kingine cha kufanya na mengine mengi, ambayo kiuhalisia sio muhimu kama ripoti hiyo. Kadiri siku zinavyokwenda unakuja na sababu. Sasa inafika alhamisi na ripoti inatakiwa ijumaa, hapa hakuna sababu yoyote itakayokuzuia, utakesha kama itabidi ili tu ukamilishe ripoti kwa wakati.

Tuchukulie mfano mwingine, mtu anakuwa anasema nitaanza biashara kila mwaka haanzi, bali anakuja na sababu, ujue mwaka huu watoto wanaenda shule, mwaka mwingine sijui kuna nini. Sasa inapofika wakati kile chanzo chake kikuu cha mapato kinakatika, ndipo sasa kuanza biashara inakuwa sio kujadili tena, bali ni lazima na hapo hakuna sababu yoyote itakayoweza kumzuia.

Unapopanga kufanya kitu halafu ikaja sababu kwa nini usifanye, kabla hujakubaliana na sababu hiyo, kaa kwanza na utafakari. Je hiki unachotaka kufanya ni muhimu sana kwako? Na hata kama sio muhimu sana kwa sasa, je baadae kitakuwa muhimu sana? Kama jibu ni ndiyo basi weka sababu zote pembeni na anza kufanya. Kwa njia hii utafanikisha mengi makubwa.

SOMA; Amka Na Sababu Hii Kila Siku Na Itakusukuma Kufikia Mafanikio Makubwa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba ninapokuja na sababu kwa nini siwezi kufanya kitu fulani, maana halisi ni kwamba kitu hiko sio muhimu kwangu. Kwa sababu kama kingekuwa muhimu na maisha yangu yote yanategemea hapo, ni lazima ningepata njia ya kukifanya, na hakuna sababu ambayo ingenirudisha nyuma.

NENO LA LEO.

“If you really want to do something, you’ll find a way. If you don’t, you’ll find an excuse.”

― Jim Rohn

Kama kweli unataka kufanya kitu na ni muhimu kwako utapata njia ya kufanya. Kama sio muhimu sana kwako utapata sababu za kutokufanya.

Unapoona unapata sababu za kwa nini huwezi kufanya kitu fulani, basi jua hiko sio kitu muhimu kwako kufanya.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.