Maisha bora yanaanza na amani ya moyo ambayo unayo. Kama moyoni mwako huna amani, haijalishi unamiliki vitu gani, bado maisha yataonekana kuwa magumu na huwezi kuyafurahia.
Na amani hii ya moyo inatokana na mambo mengi. Kwanza inaanza na kufanya kile ambacho unapenda, kuchagua kuishi maisha ambayo yana maana kwako na kuwa na mchango mkubwa kwa wengine.
Tumekuwa tukipata amani, lakini pia imekuwa siyo ya kudumu. Mara kwa mara amani hiyo imekuwa inatikiswa na hivyo furaha yetu kuingia mashakani kila mara. Leo tutaangalia njia moja ya uhakika ya kuwa na amani isiyotishika na hivyo kuyafurahia maisha mara zote, bila ya kujali unapitia nini.
Njia hii ni kutokuweka thamani kubwa kwenye vitu ambavyo vinaweza kuondolewa kwako kwa muda wowote ule. Hii ni njia rahisi sana lakini ngumu kuifuata. Kwa sababu tumezoea na tunapenda kuweka thamani kubwa sana kwenye vitu ambavyo hatuna udhibiti navyo. Na inapotokea pale wenye udhibiti wanachukua hatua ambayo ni tofauti na matarajio yetu, basi tunajikuta tunakosa amani.
Usiweke thamani kubwa kwa kitu ambacho mtu mwingine anaweza kukiondoa kwako mara moja. Usiweke matarajio makubwa kwenye kitu ambacho huwezi kukidhibiti. Hapo utakuwa unajiandaa kukosa amani muda wowote.
Lakini pia hii haimaanishi usitumie kitu ambacho huwezi kukidhibiti, bali kitumie na kifurahie kwa wakati wowote unapokuwa nacho, lakini pia jua wakati wowote hutakuwa nacho. Hii itakusaidia kuwa na maandalizi na pia kuwa na amani ya kudumu.
SOMA; UKURASA WA 416; Sio Vyote Vitaenda Kama Utakavyo.
TAMKO LANGU;
Nimejifunza ya kwamba ili niwe na amani ya moyo ya kudumu, basi nisiweke thamani kubwa na mategemeo yangu yote kwenye kitu ambacho mtu mwingine anaweza kukichukua kwangu mara moja. Kitu ambacho siwezi kukidhibiti. Badala yake nitumie vitu vya aina hiyo nikijua vinapita, nivifurahie kwa wakati huo wakati najiandaa kwa njia nyingine mbadala.
NENO LA LEO.
Don’t depend on other people to be responsible for you. Don’t make yourself stressed out over nonsensical things like material things. – Eartha Kitt
Usitegemee watu wengine wabebe majukumu yako. usikubali kuvurugwa na vitu visivyo muhimu kama mali za kupita.
Usiweke mategemeo yako makubwa kwenye vitu ambavyo huwezi kuvidhibiti, utakuwa unajiandaa kuangushwa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.