Moja ya mabadiliko makubwa sana yanayoendelea kwenye ulimwengu wa biashara kwa zama hizi ni urahisi wa kuingia kwenye biashara. Zamani ili uingie kwenye biashara ilihitaji uwe na mtaji mkubwa sana. Ila kwa sasa unaweza kuanza biashara kwa mtaji mdogo au wakati mwingine bila ya kuwa na mtaji kabisa. Kwa urahisi huu wa kuingia kwenye biashara kwa upande wa mtaji, unafanya vikwazo vya kuingia kwenye biashara mtaji usiwepo.

Pamoja na kuwa rahisi kuingia kwenye biashara, hasa kwa upande wa mtaji, bado kuna mambo muhimu sana ambayo mfanyabiashara anahitaji kuzingatia ili kuweza kukuza biashara yake hasa pale anapoanza biashara hiyo kwa mtaji kidogo.

Kabla ya kuanza kuangalia mambo hayo matatu kwanza tukumbushane kitu muhimu sana. Kitu hiki ni kwamba unapoanza biashara kwa mtaji kidogo, njia yako inakuwa tofauti na yule anayeanza biashara kwa mtaji mkubwa. Na hivyo uendeshaji wako wa biashara unapaswa kuwa tofauti pia. Kwa kuendesha biashara yako kama wengine ambao huenda wameanza au wana mtaji mkubwa kuliko wewe, ni kujiandaa kushindwa kwenye biashara.

Karibu sasa tujifunze mambo matatu muhimu ya kuzingatia na uanze kuyafanyia kazi.

Jambo la kwanza ni UBUNIFU.

Unapoanza biashara kwa mtaji kidogo, au bila ya kuwa na mtaji kabisa, unahitaji kuwa na ubunifu wa hali ya juu sana. Hii ni kwa sababu huna nguvu kubwa ya kushindana kwa upande wa rasilimali. Badala yake unahitaji kuja na vitu vya tofauti ambavyo vitawafanya wateja wako waje na pia wawaambie watu wengine ili pia nao waje.

Mtu anayeanza au kufanya biashara kwa mtaji mkubwa anaweza kuwa na bajeti ya kuitangaza biashara yake. Ila wewe unayeanza kwa mtaji kidogo, au bila ya mtaji unaweza kukosa bajeti hii. Hivyo njia pekee ya kutangaza biashara yako inabaki kuwa wateja ambao wameridhishwa na bidhaa au huduma unazotoa. Ili uweze kuwaridhisha wateja, unahitaji kuwa na ubunifu, ili kuwapatia kitu cha tofauti na kile walichozoea kupata kupitia wafanyabiashara wengine.

Na katika ubunifu wako kwenye biashara, zingatia yale maeneo ambayo yanafanya maisha ya mteja wako kuwa bora zaidi. Angalia ni jinsi gani biashara yako inawasaidia watu kupata kile wanachotaka au kuondokana na kile wasichopenda. Kisha kila siku jiulize ni kwa jinsi gani unaweza kuboresha zaidi. Kamwe usiendeshe biashara yako kwa mazoea au kwa kuangalia wengine wanafanya nini. Endesha biashara yako kwa ubunifu wa hali ya juu sana na utawafanya wateja wako kuwa watangazaji wakubwa wa biashara yako.

Jambo la pili ni KUJITOA.

Ni rahisi kuingia kwenye biashara kwa mtaji kidogo, ila ni vigumu sana mpaka uweze kusimamisha biashara yako. unahitaji kujitoa hasa, yaani siyo kidogo. Unahitaji kujitoa kwa kuweka juhudi kubwa sana kwenye biashara yako. kwa sababu unapoanza biashara kwa mtaji kidogo au bila ya mtaji, utahitaji kuvaa kofia nyingi kwa wakati mmoja. Wewe ndiye mmiliki wa biashara, wewe ndiye mtoa huduma kwa wateja, wewe ndiye mhasibu, wewe ndiye afisa mauzo nakadhalika. Huwezi kusema kwamba eneo fulani la biashara yako haliendi vizuri kwa sababu huna wa kukusaidia, unahitaji kuwa vizuri kwenye maeneo yote, na hapo ndipo unapohitaji kujitoa sana.

Wale wanaoingia kwenye biashara kwa mtaji mkubwa, wana uwezo wa kuajiri wa saidizi wengi na hivyo kufanyia kazi yale maeneo machache ambayo ni muhimu sana. Lakini wewe utahitaji kufanyia kazi maeneo yote, muhimu na ambayo siyo muhimu. Wakati mwingine utajikuta unahitajika kufanya kazi zaidi ya muda wa kawaida wa watu kufanya kazi. Kuna baadhi ya vitu ambavyo unatakiwa uwe tayari kuviacha japo ulikuwa umezoea kufanya. Kujitoa sio kazi rahisi, inahitaji uwe umeamua hasa kufanikiwa kupitia biashara yako.

Jambo la tatu ni UVUMILIVU.

Kuna kitu kimoja naweza kukuhakikishia unapoingia kwenye biashara kwa mtaji mdogo, njia yako itakuwa ngumu sana. Kwa biashara zote njia ni ngumu, ila kwa biashara zinazoanza kwa mtaji kidogo njia ni ngumu zaidi. Hii ni kwa sababu kwanza unaanzia ngazi za chini sana, ngazi ambazo huenda wengi hawataweza kukuelewa. Na sababu nyingine kubwa ni wengi wa watu wanaofanya biashara kama unayofanya wewe, kwa kuwa ni rahisi kuingia, wengi wanaingia. Hivyo utajikuta mnagombea wateja wachache sana, na hili linafanya safari hii kuwa ngumu. Unahitaji kuwa na uvumilivu sana ili kuweza kuvuka changamoto mbalimbali utakazokutana nazo. Kuna wakati mambo yatakuwa magumu na utakaribia kukata tamaa, ni wakati huu ambapo unahitaji kuwa mvumilivu zaidi kwani kukosa uvumilivu kutakuondoa kwenye biashara mapema sana.

Watu wengi wamekuwa wakiingia kwenye biashara kwa mitaji kidogo, na kujikuta wakishindwa kwenye biashara hizo haraka sana. Na wale wanaofanikiwa kuendelea, wengi huishia kuwa na biashara ndogo ambazo hazikui. Wewe umeshapata maarifa haya kwa mambo matatu ya kuzingatia, yafanyie kazi na utaweza kuikuza biashara yako. Kila la kheri.