Kama sijawahi kukuambia hili basi naomba nianze nalo mapema kabisa, utakataliwa mara nyingi sana kwenye maisha yako. najua umeshapitia hali hii lakini nina wasiwasi huenda hujajua kwamba utaendelea kukataliwa na wengi zaidi kadiri siku zinavyokwenda.
Hapo nilikuwa nakukumbusha tu, kwamba utakataliwa, mara nyingi na kwenye mambo mengi. Leo nataka nikushirikishe hatua za kuchukua pale unapokataliwa. Kwa sababu wengi huishia kuumia wanapokataliwa na hivyo kukata tamaa ya kuendelea.
Moja jua ya kwamba utakataliwa, na tegemea kukataliwa, angalau na watu wengi. Kosa linalofanywa na wengi ni pale wanapokuwa na wazo na kufikiri kila mtu atalipokea kwa shauku kama aliyonayo yeye, hivyo linapokataliwa kuumia.
Mbili ukishakataliwa ni vyema usipoteze muda kufikiria sababu ya kukataliwa. Wengi watakaokukatalia hawatakupa sababu za ukweli, kwa sababu ukweli unauma na hawataki kukuumiza. Hivyo unaweza kumpa mtu wazo la biashara ambalo unataka mshirikiane. Akakujibu yeye hataweza kwa sababu kwa sasa amebanwa, hili alilokupa ni jibu la kukufurahisha, lakini jibu la ukweli ni wazo lako haliwezi kufanya kazi, unaoteza muda. Lakini hatakuambia hivi moja kwa moja.
Tatu endelea kuweka juhudi, usikate tamaa wala kurudi nyuma. Angalia ni fursa zipi ambazo bado zipo mbele yako na fikiria kuzifanyia hizo kazi kuliko kufikiria ni wangapi wamekukatalia kile ulichopendekeza.
Tegemea kukataliwa, usichukue sababu yoyote unayopewa, endelea kusonga mbele. Hakuna njia nyingine rahisi zaidi ya hii. Na kama ukiifuata lazima tutakutana kileleni. Kila la kheri.
SOMA; Usikubali mtu yeyote awe mzigo kwako.
TAMKO LANGU;
Nimejikumbusha ya kwamba nitakataliwa na wengi katika mambo mengi. Na katika kukataliwa huku sitapewa sababu halisi. Ni jukumu langu kuendelea kusonga mbele bila ya kujali ni nani aliyenikatalia. Hakuna wa kunirudisha nyuma ila mimi mwenyewe.
NENO LA LEO.
Life is a succession of lessons, which must be lived to be understood. – Ralph Waldo Emerson
Maisha ni muendelezo wa masomo ambayo ni lazima uyaishi ili kuyaelewa.
Katika kuishi maisha yako, kuna wengi watakukatalia kile unachopendekeza, elewa na songa mbele.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.