Kuna mtu amekuwa anakuibia muda wako kwa muda mrefu sana. Na amekuwa akifanya hivi kila wakati. Kwa kukuibia muda wako amekuwa anakunyima fursa ya kufurahia chochote unachokifanya. Je ungependa kumfahamu mtu huyu na njia za kumkomesha? Basi nafasi ndiyo hii hapa.

Mwizi wa muda wako ni wewe mwenyewe, ndiyo, wewe hapo ulipo umekuwa unajiibia muda wako. Na muda ambao umekuwa unajiibia ni muda ulionao kwa wakati husika. Kwa mfano muda huu unaotumia kusoma hapa sasa hivi, ndio muda ambao unaweza kujiibia.

Njia ambazo umekuwa unatumia kujiibia muda ni kuwa unafanya kitu kimoja huku unafikiria kitu kingine.

Unafanya kazi yako huku ukifikiria ulichokosa jana, au kutokuwa na uhakika na kesho.

Unapata chakula huku ukifikiria kazi uliyoshindwa kukamilisha.

Unakwenda kukamilisha kazi yako huku ukifikiria chakula ambacho hukula vizuri.

Tumekuwa tunapoteza muda wetu wote, kwa kutoruhusu akili yetu kuwa kwenye kile ambacho tunakifanya kwa wakati husika.

Hali hii inakujaza hofu na kutuondolea furaha inayotokana na kile ambacho tunakifanya.

Ufanye nini ili kuondokana na changamoto hii ya kujiibia muda?

Na njia pekee ni kuhakikisha unayatawala mawazo yako, hakikisha mawazo yako yapo kwenye kile unachofanya kwa wakati husika.

Unawezaje kuhakikisha hili?

1. Gawa jukumu lako kwenye mafungu madogo madogo na chagua kuweka dakika chache kwenye kila fungu ulilogawa. Kila baada ya fungu pumzika kidogo. Unaweza kufanya kitu kwa nusu saa mfululizo na kupumzika dakika tano.

2. Kila baada ya muda unapokuwa unafanya kitu, jisimamishe na kujihoji ni nini unafanya na mawazo yako yapo wapi.

3. Mara kwa mara jipe mazoezi ya kudhibiti akili yako. Kaa mwenyewe bila ya kufanya chochote na hesabu pumzi zako, ukivuta pumzi hesabu moja, ukitoa pumzi hesabu mbili. Nenda hivi mpaka ufike kumi, halafu anza tena moja. Fanya hivi kwa dakika 10, kuna wakati akili yako itataka kutoroka, irudishe hapo kwa kuendelea kuhesabu pumzi zako.

4. Vaa mpira (rubber band) kwenye mkono wako, na kila wakati mawazo yako yanapohama kutoka kwenye kile unachofanya vuta mpira ule ukunase, hii itakujengea kuepuka kuhamisha mawazo ili kuepuka maumivu.

5. Kaa na orodha muda wote, unapokuwa unafanya kitu na wazo jipya likaja kichwani mwako, andika wazo hilo kwenye orodha yako, na endelea kufanya ulichokuwa unafanya. Kwa kuliandika wazo hilo unakuwa umelitoa akilini mwako kwa muda.

Kwa kuanza na hayo, na kuwa na nia ya dhati utaweza kuyadhibiti mawazo yako ili kuweza kutulia sehemu moja na kufanya mambo yako kwa ubora.

Kuanzia sasa hebu kuwa mlinzi wa muda wako na kile unachofanya. Kila wakati jisimamishe na jiulize je mawazo yako yapo kwenye kile unachofanya? Kama jibu siyo yarudishe haraka. Siyo zoezi rahisi lakini ukishaweza kudhibiti akili yako, hakuna kitakachokushinda kudhibiti.

SOMA; Vitu Viwili Ambavyo Vimekuwa Adimu Sana Kwenye Dunia Ya Sasa, Na Ukiwa Navyo Ni Mtaji Mkubwa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba mimi ndiye mwizi mkubwa wa muda wangu mwenyewe. Nimekuwa najiibia muda wangu kwa kushindwa kuweka mawazo yangu kwenye kile ninachofanya kwa wakati husika. Kuanzia sasa nitahakikisha mawazo yangu yote yako kwenye kile kitu ninachofanya kwa wakati husika, kwa kujikumbusha mara kwa mara kurudisha mawazo yangu kwenye kitu hiko.

NENO LA LEO.

“If you want to conquer the anxiety of life, live in the moment, live in the breath.” ― Amit Ray

Kama unataka kushinda wasiwasi wa maisha, ishi kwa wakati ulipo sasa, ishi kwa pumzi unayopumua sasa.

Weka mawazo yako yote kwenye kile kitu unachofanya sasa, na utakuwa na wakati bora sana. Usisumbuke na yaliyopita au yajayo, kitu muhimu kwako ni kile unachofanya sasa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.