Fedha ni hitaji muhimu sana kwenye maisha yetu, ukiondoa hewa ya oksijeni ambayo ni muhimu ili maisha yetu yaweze kwenda, fedha inafuatia kwa umuhimu. Lakini pamoja na umuhimu huu mkubwa wa fedha, bado jamii zetu zimekuwa zinabeza sana fedha. Mazungumzo ya fedha yamekuwa yakionekana kama ni mwiko. Ukionekana unazungumzia sana fedha watu wanakuona una tamaa au huna wema. Lakini watu hawa hawa ndiyo wanaozifikiria fedha kabla ya kulala na wanapoamka mawazo yapo kwenye fedha.
Hivyo pamoja na malengo na mipango yako mikubwa kwenye maisha, kufikia uhuru wa kifedha au utajiri ni hitaji muhimu sana kwa kila mmoja wetu. Na hapa ndipo mwandishi David Taylor anapotushirikisha mwongozo wa uhakika wa kufikia utajiri na uhuru kwenye maisha yetu kupitia kitabu chake cha NAKED MILLIONARE. Kwa lugha rahisi kitabu hiki kinaweka wazi kabisa mbinu zote muhimu za kukuwezesha wewe kufikia umilionea na hata ubilionea kwenye maisha yako.
Karibu hapa nimekuandalia mambo 20 muhimu sana niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki. Karibu tujifunze kwa pamoja.
1. Kwanza kabisa kuwa wewe, hili ndilo hitaji muhimu sana kwako kuw ana maisha ya furaha na mafanikio. Sehemu pekee unayoweza kuanza nayo ni kuanza kuwa wewe. Mamilionea wengi wanasema walifikia umilionea baada ya kuanzia kwenye eneo sahihi na kwa wakati sahihi. Eneo sahihi kwako ni hapo ulipo sasa na wakati sahihi ni huu ulionao sasa. Usitake kuiga maisha mengine, usitake kufanana na wengine na usisubiri tena. Kuwa wewe, anzia hapo ulipo na anza sasa. Hakuna njia nyingine rahisi zaidi ya hiyo.
2. Kuwa wazi ni kitu gani hasa unachotaka kwenye maisha yako, shika hatamu ya maisha yako kwa chochote unachofanya au unachosema. Pia shika hatamu ya vipaji ambavyo tayari unavyo, hasa vile ulivyozaliwa navyo. Hizo ni mali zako na zimiliki ili uweze kuzitumia. Fanya maamuzi ya kweli ya kile unachotaka kukifanya na kifanye. Na katika kufanya, hakikisha unawasaidia wengine, kufanya maisha yao kuwa bora zaidi. Na hapa ndipo utafikia mafanikio makubwa huku ukiwa na furaha.
3. Kile unachofanya ndicho kinacholeta majibu. Haijalishi unajua kiasi gani, haijalishi unasema nini, majibu yako yatatokana na kile unachofanya. Ni kile unachofanya kila siku ndiyo kitakachokupeleka kwenye mafanikio au kukuzuia kufikia mafanikio. Vingine vyote ni kelele tu, kinachoonekana ni majibu yanayotokana na vitendo. Kuwa mtu wa vitendo.
4. Kwa chochote kile unachofanya, simama kwa muda na jiulize swali hili muhimu sana. Je hiki ninachofanya kinanisogeza karibu na malengo na mipango yangu kwenye maisha? Kama jibu ni ndiyo endelea kufanya zaidi na weka juhudi kubwa sana. Kama jibu ni hapana acha mara moja na fanya kitu kingine ambacho kitakupeleka kwenye malengo yako.
5. Ishi maisha yako kwa ukamilifu, kwa kila siku na kila dakika. Fanya kile ambacho ni muhimu. Na fanya mpaka utakapopata unachotaka, au unapoamua kukata tamaa. Kuna wakati utakuwa na hofu kama kweli unaweza au kama kweli utapata unachotaka. Lakini kabla hujakubali hofu hii ikutawale, kumbuka kwamba siku moja utafunga macho yako na hutayafungua tena, na hofu yoyote uliyonayo sasa wakati huo haitakuwa na maana tena.
6. Safari yako ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa na utajiri siyo safari nyepesi, na wala njia haijanyooka. Utakutana na changamoto nyingi, utakatishwa tamaa na pia utashindwa. Unachohitaji kwenye safari hii ni kuwa wewe, kuwa mkweli kwako mwenyewe na furahia safari hii. Jifunze kwenye kila jambo unalopitia. Fanya kile unachohitaji kufanya kwa wakati unaohitaji kukifanya, na hii inahitaji kuweka juhudi kubwa, kuwa na umakini na kuwa na nidhamu kubwa.
7. Ni lazima ushike hatamu ya maisha yako kama kweli unataka kufikia mafanikio. Hakikisha unaweza kudhibiti mawazo yako, maneno yako na hata matendo yako. usikubali kuwa mwathirika wa mambo yanayotokea au wanayofanya wengine. Usiwe mtu wa kulalamika au kulaumu wengine. Usikubali kutafuta sababu ya kukufanya ujisikie vizuri. Unapokosea chukua hatua, kama umechelewa kwenye kikao na mtu jua kabisa umekosea, usitake kusingizia foleni au kitu kingine chochote, omba radhi na wakati mwingine usirudie tena. Timiza kile unachoahidi na kama huwezi kutimiza sema mapema na ahidi vyema. Hivi ni vitu vidogo vidogo sana, lakini vinawashinda wengi kufanya na ndiyo maana wanakuwa na maisha magumu.
8. Kujiamini ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio yako. kuweza kuendesha biashara yenye mafanikio, kuweza kutengeneza mahusiano bora na wengine na kuweza kuwa tajiri ni lazima ujiamini. Kujiamini ni kujua kwamba una uwezo mkubwa na kuweza kutumia uwezo huo kuwa bora zaidi. Kujiamini hakuhitaji kujigamba kwa wengine bali kufanyia kazi kile unachoweza. Watu wanaojiamini wana utu na wapo tayari kuwasaidia wengine ili nao wawe bora. Pia watu wanaojiamini hawahitaji kuwatambia wengine kuhusu mafanikio yao.
9. Njia rahisi ya kuweza kujijengea kujiamini ni kuanza kuigiza kama vile tayari unajiamini. Akili yako haiwezi kutofautisha uhalisia na maigizo. Unapofanya mambo yako kama mtu anayejiamini, taratibu unaanza kujijengea kujiamini. Kadiri unavyofanya kama mtu mwenye kujiamini ndivyo utakavyoanza kupoteza ile hali ya kutokujiamini.
10. Tengeneza mahusiano ya uaminifu na watu wengine. Kuwa mwema kwa watu ambao huhitaji kuwa wema kwao. Inapotokea umekosana na mwenzako kwenye kazi au biashara fanya jambo kuondoa tofauti zenu. Chochote unachotaka kinatoka kwa wengine, utajiri wako unatoka kwa wengine na mafanikio yako yanatoka kwa wengine. Kadiri watu wengi wanavyokuamini kutokana na mahusiano bora uliyotengeneza, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kufanikiwa.
11. Tengeneza mahusiano yako na fedha vizuri. Hili ni jambo ambalo hujawahi kufundishwa popote, lakini ni muhimu sana. Mahusiano yako na fedha ni muhimu mno. Kinachowafanya wengine wafuatwe na fedha, huku wengine wakizitafuta kwa shida ni mahusiano ambayo mtu amejijenga na fedha. Fedha inaenda kule inakopendwa na inakimbia kule isikopendwa. Ipende fedha, ithamini na ione kama alama ya mafanikio. Unaweza kuwa tajiri, kuwa na furaha na kuleta tofauti kwenye maisha ya wengine.
12. Kabla hujajenga mahusiano mazuri na wengine, kuna mtu mmoja muhimu sana ambaye unahitaji kujenga naye mahusiano mazuri na ya kuaminiana. Mtu huyu ni wewe mwenyewe. Kamwe huwezi kuwa na mahusiano bora na watu wengine kama wewe mwenyewe huna mahusiano bora na nafsi yako. hii ni kwa sababu kama hujiamini wewe mwenyewe, utakuwa unatafuta dhamana ya wengine kwa kila unalofanya na kwa hali hii huwezi kujenga mahusiano bora. Anza kujiamini mwenyewe na utajenga mahusiano bora na wengine.
13. Utakapoanza kufanya yale ambayo ni muhimu kwako, utakapoanza kufanikiwa sana na utakapoanza kujenga utajiri mkubwa, wataibuka watu wengi sana kukupinga. Wengine watakusema vibaya, wengine watasema unadhulumu, wengine watasema njia unazotumia siyo za kawaida na mengine mengi. Hili lisikutishe, ni hali ya kawaida kwa watu ambao hawawezi kuvumilia kuona wengine wakifanya makubwa kwenye maisha yao. Jua ya kwamba huwezi kufanikiwa bila ya kuacha kelele kwa wengine, kelele hizi zisikurudishe nyuma, endelea kusonga mbele.
14. Huwezi kuwa tajiri kwa kujitegemea wewe mwenyewe. Unahitaji msaada, ushirikiano, mawazo, fedha na vingine vingi kutoka kwa watu wengine. Hata kama biashara yako umeianzia chini kabisa na kwa kuteseka, basi siyo wewe mwenyewe umeikuza, kuna wateja ambao walikuamini na wakashawishi wengine nao wawe wateja wako. Usijitambe kwamba unaweza kufanya kila kitu mwenyewe, tunategemeana sana hivyo tengeneza mahusiano yako vizuri.
15. Tafuta wazo lako kubwa na lifanyie kazi usiku na mchana. Kila mmoja wetu kuna kitu fulani ambacho anapenda kukifuatilia sana, au kukiongelea sana. Haijalishi kitu hiko ni nini, kama utafikiria vizuri unaweza kukigeuza kuwa chanzo chako cha kipato. Kikubwa unachohitaji ni wazo ambalo lina maana kwako, linalowasaidia wengine kuondokana na maumivu au kupata wanachokosa na wakati huo likikuingizia wewe kipato.
16. Mafanikio hayaendi kwa wale wenye akili sana, bali yanaenda kwa wale wanaojua ni nini wanataka, na wamejitoa kupata kile wanachotaka. Huhitaji akili nyingi kuwa na maisha bora, kuwa tajiri na kuwa na furaha, unahitaji kujua unataka nini ambacho unakipenda kweli na kujitoa kukipata kitu hiko. Mapenzi na juhudi zitakufikisha popote unapotaka kwenda.
17. Ni kitu gani kinachokusukuma wewe kufanya kazi unayofanya, au biashara unayofanya? Hili ni swali muhimu sana kujiuliza na kujijibu kwa sababu jibu utakalopata litakuwezesha kwenda mbali zaidi. Na katika kujua kinachokusukuma, jiulize maswali haya matatu muhimu;
Swali la kwanza; Jiulize ni nini hasa unachotaka.
Swali la pili; Jiulize hiko unachokitaka kitakufanyia nini baada ya kukipata?
Swali la tatu; Jiulize kwa nini hiko unachotaka kukifanya ni muhimu sana kwako?
Kwa maswali haya utapata hamasa kubwa ambayo itakusukuma hata kama utapitia mambo magumu kiasi gani.
18. Ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako, ili uwe na maisha ya furaha, ili uone maana kubwa kwenye kile unachofanya na ili uwe tajiri basi unahitaji kujua vipaji vyako na kuvigeuza vipaji hivyo kuwa sehemu ya kujipatia kipato. Na ili kujua kipaji chako jiulize maswali haya matatu;
Swali la kwanza; ni kitu gani ambacho kinanipa hamasa na kunisisimua?
Swali la pili; ni kitu gani ambacho napenda kukizungumzia mara kwa mara?
Swali la tatu; kama ningejua hakuna kushindwa, au kama fedha isingekuwa tatizo kwangu ni kitu gani ningefanya kwenye maisha yangu?
Maswali haya matatu yatakuwezesha kujua kipaji chako.
19. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa, unahitaji kuona vitu jinsi vilivyo. Ukweli ni kwamba hatuoni vitu kama vilivyo, badala yake tunaona vitu kama tunavyotaka viwe. Hii inatunyima fursa nzuri ya kuona na kuchukua hatua. Usifanye mambo kwa sababu umezoea kufanya, fanya kwa kujifunza na fungua macho yako na masikio yako ili uone vitu kwa uhalisia wake.
20. Jambo muhimu sana unalotakiwa kulijua na kukumbuka kila siku kwenye maisha yako ni hili; UFUNGUO WA UHAKIKA WA MAFANIKIO NI KUONGEZA THAMANI. Iwe kwenye kazi au biashara, mafanikio yako hayatatokana na kile unachofanya tu au masaa unayoweka kwenye kazi, au mwonekano wako kwa kazi unayofanya, bali kwa thamani unayoongeza kwa wengine. Tunaishi kwenye dunia ambayo ushindani ni mkali sana, ila wale wanaotoa thamani kubwa hawakosi kupata faida kubwa. Na kikubwa cha kukumbuka ni kwamba ili utoe thamani kubwa, unahitaji kuweka juhudi kubwa pia.
Hakuna chochote kinachoweza kukuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. unachohitaji ni kujua ni nini hasa unachotaka, kujua kwa sasa upo wapi, kujua ni nini unatakiwa kufanya ili kufika unakotaka na kuchukua hatua mara moja. Maana haijalishi unajua kiasi gani, kama huchukui hatua ni kazi bure.
Kila la kheri.
Asante sana kocha, Dr. Makirita Aman kwa uchambuzi huu bora kabisa; nimejifunza mengi hapa.
LikeLike
Vizuri sana, fanyia kazi yale uliyojifunza.
LikeLike