Umasikini au utajiri siyo vitu ambavyo vinatokea kama ajali, bali ni vitu ambavyo vinaandaliwa mapema na vina chanzo kimoja kikuu. Kutoka kwenye chanzo hiki ndipo watu wanakuwa matajiri na wengine wanakuwa masikini.
Chanzo hiki ni jinsi mtu anavyoyaweka na kuendesha maisha yake. Kuna namna ambayo inaleta utajiri na kuna namna ambayo inaleta umasikini.
Kama ukiyaendesha maisha yako kulingana na mahitaji ya asili, kamwe hutakuwa masikini. Hii ni kwa sababu mahitaji ya asili ni machache na yanajitosheleza. Ukishapata yale mahitaji ya msingi na kujua maisha ni vile unavyochagua kuyaishi, utajikuta ukiwa tajiri mkubwa sana.
Kama ukiyaendesha maisha yako kulingana na maoni ya watu wengine, kamwe hutokuwa tajiri. Hii ni kwa sababu maoni ya watu hayana kikomo. Ukipata kitu kimoja utataka kingine na kingine na kingine. Mwishowe utajikuta una vitu vingi lakini bado hujaridhika.
Badili sasa maisha yako na anza kuishi maisha ya utajiri, kwa kuyaendesha maisha yako kulingana na mahitaji ya asili. Endesha maisha yako kutokana na kile unachotaka kweli na unachopendelea, maoni ya wati yasikuyumbishe kabisa kwa sababu yatakupoteza.
Maisha ni yako uchaguzi ni wako, chagua kuyaishi maisha yako wewe mwenyewe na utakuwa na maisha bora sana, unayoyafurahia na hatimaye kufikia mafanikio makubwa.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba chanzo cha utajiri au umasikini ni mimi mwenyewe. Kama nikiamua kuendesha maisha yako kwa mahitaji ya asili na kuishi maisha yangu kamwe sitakuwa masikini. Lakini kama nitaamua kuendesha maisha yangu kutokana na maoni ya wengine kamwe sitakuwa tajiri. Nimechagua kuendesha maisha yangu kwa mahitaji ya asili, nimechagua maisha yangu, ili niwe bora zaidi kila siku.
NENO LA LEO.
If you shape your life according to nature, you will never be poor; if according to people’s opinions, you will never be rich. ~ Seneca Quote
Kama utayaendesha maisha yako kwa mahitaji ya asili kamwe hutakuwa masikini. Kama utayaendesha kwa mahitaji ya maoni ya wengine kamwe hutakuwa tajiri.
Chagua kuishi maisha ambayo yana maana kwako na yatakuwa bora sana kwako na kufikia mafanikio makubwa. Ila ukichagua maisha ya wengine, kila siku utajiona kuna kitu unakosa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.