Kuna sehemu moja tu ambayo maisha huwa yanatuchanganya sana. Na sehemu hii ni kati ya ukweli wa maisha, na uhalisia unaotengenezwa na wanadamu.
Unapozaliwa, iko wazi kabisa huji na ahadi yoyote, dunia hailazimiki kukupa wewe chochote. Unakuja kwenye dunia hii yenye kila aina ya fursa ukiwa hujaahidiwa chochote kutoka kwenye dunia hii.
Unapoendelea kukua, jamii inakujengea picha tofauti, kwamba chochote unachotaka wewe subiri na utapewa. Na zoezi hili limefanyika kwa kipindi kirefu mpaka sasa limeshakuwa sehemu ya maisha yetu kabisa.
Ndiyo maana mhitimu atakaa nyumbani ukimuuliza atakuambia nasubiri nipewe/nipangiwe kazi.
Ndiyo maana mwajiriwa ataendelea kupata kipato kidogo akiamini mwajiri wake anatakiwa amwongezee mshahara.
Ndiyo maana wengi wanaorithi mali wanaishia kuzipoteza zote kwa kuamini wao walikuwa wa kupewa.
Ndiyo maana wengi wanacheza kamari na bahati nasibu wakiamini wanatakiwa kupewa fedha nyingi kutokana na ubashiri wao.
Ukweli ni kwamba ni vitu vichache sana ambavyo tunapewa kwenye maisha.
Vitu vingi hupewi, unatakiwa kuvitafuta wewe mwenyewe, unatakiwa kuvichukua. Na hapa ndipo wengi wanapopotea.
Kupewa ni rahisi, unachohitaji ni kusubiri upewe, na usipopewa unaweza kulalamika au kulaumu, japo lawama au malalamiko yako yanaweza yasisaidie chochote.
Kutafuta au kuchukua ni bora sana, maana kwa njia hii utapata chochote unachotaka kwenye maisha yako na kwa njia hii unakuwa na maisha bora sana kwako.
Nimalize kwa kukushirikisha orodha ya vitu ambavyo hakuna mtu yeyote anayeweza kukupa, hata awe anakupenda na kukujali vipi.
1. Uhuru wa maisha yako.
2. Mafanikio ya kudumu.
3. Kazi unayoifurahia.
4. Biashara yenye mafanikio.
5. Heshima.
6. Ushawishi.
7. Utu wema.
8. Mahusiano bora.
9. Afya njema.
10. Furaha
11. Maarifa muhimu.
Vitu hivi na vingine vinavyofanana na hivi unavitafuta wewe mwenyewe, na unavichukua au kuvitengeneza.
Na kwa maana hii kulalamikia vitu hivi ni kujipotezea muda wako bure, maana hata ulalamike vipi hakuna kitakachobadilika. Kama unataka kubadili, amka na ukatafute au ukachukue.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kuwa Na Maisha Bora, Nenda Kinyume na Tabia Za Asili Za Binadamu.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba vitu vyote ninavyohitaji ili maisha yangu yawe bora hakuna mtu yeyote atakayenipa. Bali nahitaji kutafuta mwenyewe, kutengeneza au kuchukua. Kuanzia sasa nitaacha kupoteza muda wangu kudai vitu hivi kwa watu ambao hawawezi kunipa, na badala yake nitajidai mimi mwenyewe.
NENO LA LEO.
If you take responsibility for yourself you will develop a hunger to accomplish your dreams. – Les Brown
Kama utakubali maisha yako yawe jukumu lako, utatengeneza njaa ya kukamilisha malengo yako.
Mambo yote mazuri kwenye maisha yako ni jukumu lako, hupewi na mtu mwingine yeyote. Anza sasa kushika hatamu ya maisha yako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.