Moja ya madhara ya wewe kufanya maisha yako kuwa bora zaidi, ni kutengeneza watu wengi wenye chuki dhidi yako.

Binadamu sisi ni viumbe wa kipekee sana, tunaridhika pale tunapoona wanaotuzunguka nao wapo kama sisi. Wana kipato sawa na chetu, wanafanya kile tunachofanya.

Lakini mtu anapoamua kubadilika, na kuamua kufanya kwa ubora, na kipato chake kikaongezeka, tunaanza chuki. Wengi watatafuta kila sababu ya kusema ubaya dhidi ya yule ambaye maisha yake yamekuwa bora zaidi.

Elewa hili ili lisikuumize au kukurudisha nyuma. Maana kama hujalijua hutaweza kupiga hatua, hasa wale wanaojenga chuki wanapokuwa watu wako wa karibu sana, ndugu, jamaa au marafiki.

Waelewe wale wanaokuwa na chuki juu yako, wale ambao wanatafuta kosa kwenye kila jambo unalofanya, elewa kwamba kinachowasumbua ni kitendo cha wao kubaki pale walipo wakati wewe unasonga mbele.

Kwa kuwa umeamua kuboresha maisha yako, na kuamua kuacha kupoteza muda wako, wengi watasema unaringa. Na pale kipato chako kitakapokuwa kikubwa kuliko cha kwao, hata kama hukumwona mtu mahali ataamini ulimwona lakini hukumsalimia kwa sababu una dharau.

Jiandae kwa hili, kama kweli umekuwa unafanyia kazi haya tunayojifunza, jua ya kwamba hali hii inakuja kama bado hujaifikia.

Na hatua bora ya kuchukua kwenye hali hii ni kuendelea na yale maisha uliyochagua, na ipo siku watakuelewa. Muhimu ni kuwa mwema, lakini usikubali kuwa mtumwa kwa sababu tu maisha yako yamekuwa bora kuliko ya wengine.

SOMA; Kama Unayapigania Mafanikio, Watu Watakuchukia, Usiumizwe na Hilo.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kwa mambo haya mazuri ninayojifunza na kufanyia kazi, maisha yangu yatakuwa bora sana. Na maisha yangu yatakapokuwa bora nitatengeneza watu wenye chuki dhidi yangu. Sitakubali watu hawa wanirudishe nyuma kwa namba yoyote ile, badala yake nitaendelea kuweka juhudi na kuwa mwema, ila sitokubali kuwa mtumwa kwa wengine.

NENO LA LEO.

“Haters don’t really hate you, they hate themselves; because you’re a reflection of what they wish to be”

― Yaira N

Wenye chuki kiuhalisia hawakuchukii wewe, bali wanajichukia wao wenyewe; kwa sababu wewe ni taswira ya kile wanachotamani kuwa.

Kama kuna watu wanaonesha chuki kwako, jua wanajichukia wao kwa sababu hawajaweza kufikia ngazi ulizofikia wewe. Usikubali watu hawa wakurudishe nyuma, endelea kuweka juhudi, kuna siku wataelewa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.