Kila mmoja wetu ni mtumwa, yaani mimi, wewe na yule tu watumwa kwenye maeneo fulani ya maisha yetu.
Kuna ambao ni watumwa wa fedha, wengine watumwa wa mapenzi, wengine watumwa wa dini. Pia kuna watumwa wa madaraka, watumwa wa ajira na hata watumwa wa biashara.
Kinachotutofautisha ni aina ya utumwa na ikiwa tumechagua au hatujachagua.
Kuna ambao wanachagua wawe watumwa kwenye nini, na aina hii ya utumwa huwa inakuwa na matokeo mazuri kwa yule anayechagua. Uka ni watu wachache sana wanaoweza kutumia nafasi hii ya kuchagua ni kitu gani wanataka kuwa watumwa.
Kundi kubwa la watu wanajikuta kwenye utumwa ambao hawajachagua wao wenyewe, bali mazingira au hali ya mambo imepelekea wao kujikuta kwenye utumwa. Ubaya wa utumwa huu ni unaumiza na pia ni vigumu sana kuweza kujinasua kutoka kwenye utumwa wa aina hii.
Na utumwa wetu unaongozwa na nguvu kuu mbili, matumaini na hofu. Tunakuwa na matumaini kwamba kitu fulani kitakuwa bora na hivyo kukitegemea sana na kuweka kila ambacho tunacho katika kuhakikisha tunapata kile tunachotaka. Na pia hofu inatufanya tushindwe kuchukua hatua fulani, au tulazimike kuchukua hatua ambayo huenda hatupendi kuchukua. Matumaini na hofu vinatufanya tuendelee kuwa watumwa kwenye utumwa wetu.
Yatafakari maisha yako na ona ni maeneo gani ambayo umekuwa mtumwa, na jiulize je utumwa huo una matokeo bora kwako? Kama siyo anza kuchukua hatua ya kubadili hali uliyopo sasa.
SOMA; Hivi Ndivyo Waajiriwa Wanavyopoteza Uhuru Wao Wenyewe, Na Jinsi Ya Kuudai Tena.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba mimi na wengine wote wanaonizunguka ni watumwa wa mambo fulani. Na utumwa huu unaweza kuwa mzuri au mbaya. Pia utumwa wangu unachochewa na matumaini au hofu. Leo ninayatafakari maisha yangu kujua ni utumwa gani nilionao na jinsi gani ya kuyafanya maisha yangu kuwa bora zaidi.
NENO LA LEO.
When work is a pleasure, life is a joy! When work is a duty, life is slavery. – Maxim Gorky
Pale kazi inapokuwa kitu unachokipenda, maisha ni furaha. Pale kazi inapokuwa ni wajibu, maisha ni utumwa.
Je ni maeneo gani kwenye maisha yako ambayo bado upo kwenye utumwa? Yajue ili uweze kuboresha maisha yako zaidi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.