Hakuna anayeweza kukataa kwamba dunia inabadilika, na sio tu kwamba inabadilika, bali inabadilika kwa kasi kubwa sana. Mtandao wa intaneti umegusa kila eneo la maisha, na kwenye biashara ndio umegusa kila eneo la biashara.
Wakati mtandao wa intaneti unaanza kukua na kusambaa kwa kasi, watu wengi walifikiri ni kitu ambacho hakitahitajika na kila mtu. Na hivyo mwanzoni ni ofisi muhimu tu zilizoweza kutumia mtandao wa intaneti. Baada ya mtandao wa intaneti kukua sana, mitandao ya kijamii nayo ilizaliwa kwa kasi kubwa. Wakati mitandao hii ya kijamii inachipukia kwa kasi, wengi walifikiri ni kitu cha kupita tu, lakini uwepo wa mitandao ya kijamii kwa zaidi ya miaka kumi sasa na huku ikiendelea kukua, ni ushahidi tosha kwamba hiki siyo kitu cha kupita.
Pia kutumiwa sana kwa mitandao hii na vijana na lengo la kuwasiliana tu, kulifanya wengi waone sio kitu muhimu kila mtu kukitumia. Na hivyo biashara nyingi hazikuchukua fursa ya kutumia mitandao hii ya kijamii katika kukua na kuwafikia wateja wengi zaidi.
Kwa hali tuliyofikia sasa, hasa kwenye maendeleo ya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii kwa ujumla, kama biashara yako bado haijaanza kutumia mitandao ya kijamii jua ya kwamba unapoteza wateja wengi. Watu wengi kwa sasa wapo kwenye mitandao hii ya kijamii na hivyo wateja wako pia wapo kwenye mitandao hii.
Leo katika makala ya KONA YA MJASIRIAMALI, tutaangalia jinsi unavyoweza kutumia mitandao ya kijamii kukuza biashara yako zaidi.
Tengeneza mahusiano bora na wateja wako kupitia mitandao.
Wengi wanaposikia matumizi ya mitandao ya kijamii, hufikiria kitu kimoja pekee, kutangaza biashara. Sawa hili ni lengo moja la biashara ila usiishie kutumia mitandao kutangaza pekee, kwa kufanya hivi utapoteza hata wateja ulionao. Tumia mitandao ya kijamii kujenga mahusiano mazuri na wateja wako. Tumia mitandao hii kuwapa taarifa muhimu wateja wako kuhusiana na mambo yanayohusu biashara zako. Tumia fursa hiyo kujibu maswali na changamoto ambazo wateja wa biashara yako wanakutana nayo kwenye maisha yao. Na pia tumia mitandao hii ya kijamii kupata na kujibu malalamiko ya wateja wako. Tumia mitandao ya kijamii kuwa karibu na wateja wako ili nao wawe karibu na biashara yako.
Tumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara yako.
Mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu sana kwa kutangaza biashara. Lakini watu wengi hawajui mbinu bora za kutangaza biashara kupitia mitandao hii. Matangazo ya kupitia mitanda ya kijamii hayatakiwi kufanana kabisa na matangazo ya njia za kawaida. Usiende tu kwenye mitandao na kusema mimi nauza hiki, au natoa huduma hii. Unahitaji kwanza kujenga mahusiano kama tulivyoona hapo juu, na kupitia mahusiano haya ndiyo unaweza kuwaambia watu kuhusu huduma au bidhaa unazotoa. Imani baina ya watu wanaokutana kwenye mitandao ni ndogo sana hasa kama hawajajuana kwa muda mrefu, ndiyo maana unahitaji kujenga mahusiano kwanza. Kama nakujua kupitia mitandao hii kwa mambo unayoelimisha kuhusu biashara yako, nitakuamini na kuweza kununua kwako. Kama ninachoona ni matangazo ya biashara yako pekee, ni vigumu kuwa na imani kwako.
Tumia mitandao ya kijamii kuajiri wafanyakazi bora kwa biashara yako.
Kuajiri ni moja ya maeneo muhimu sana ya ukuaji wa biashara yako. tofauti na zamani ambapo ulikuwa ukiangalia wasifu wa mwombaji kupitia maombi ya kazi aliyotuma. Hivyo ilikuwa vigumu kujua tabia halisi za mtu unayetaka kumwajiri kwa sababu kwa kuandika pekee kila mtu anaweza kujipendelea. Ila kwa uwepo wa mitandao ya kijamii umefanya kuwa rahisi kumjua vizuri mtu kabla hujamwajiri. Na utamjua vizuri kwa kuangalia mambo anayoweka kwenye mitandao yake ya kijamii. Na ni rahisi sana, ingia kwenye mitandao mikubwa ya kijamii na tafuta jina la mtu huyo, utapata taarifa zote anazoweka kwenye mitandao hii.
Kama mpaka sasa biashara yako haijaingia kwenye mitandao ya kijamii unakosa fursa kubwa sana ya kuikuza biashara yako. Hakikisha unatengeneza uwepo wako kwenye mitandao hii. Na mitandao mikubwa unayohitaji kuanza nayo ni facebook, linked in, twitter, instagram na whatsapp.