Hizi ni hisia mbili hasi ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa sana kwenye maisha yako, kama utashindwa kujua jinsi ya kwenda nazo vyema.

Hasira na huzuni.

Tunaishi kwenye dunia yenye utata wa hali ya juu, tungependa mambo yawe rahisi na mazuri kama tunavyotegemea lakini hayaendi hivyo.

Tunapenda watu wawe kama vile tunavyopenda wawe, wafanye yale ambayo tunawategemea wafanye, lakini siyo kinachotokea.

Watu wanafanya tofauti na mategemeo yetu, au wanafanya kile ambacho hatukutegemea kabisa. Mambo yanatokea tofauti na tulivyotegemea na hivyo tunapata hasira.

Kuna vitu ambavyo tunavithamini sana kwenye maisha yetu, tungependa kuwa na vitu hivi kwa muda mrefu, tuendelee kuwa navyo kila siku za maisha yetu, labda ni ndugu, watoto, wapenzi, kazi, biashara na kadhalika. Lakini dunia ni tata, wewe unapanga na dunia inafanya yake. Inatokea kile ulichokithamini sana, na ulichotegemea kuwa nacho kwa muda mrefu, unakipoteza, na hapa unapata huzuni.

Hisia hizi mbili, hasira na huzuni ni sehemu ya maisha yetu. Lakini pia zinatuumiza sana, na tusipokuwa makini zinaweza kuyaharibu sana maisha yetu.

Pale unapokuwa na hasira na kufanya kitu ambacho kinaharibu sana maisha yako. Au unakuwa na huzuni iliyopitiliza na hatimaye kujikuta kwenye msongo wa mawazo au sonona.

Watu wengi wamekuwa wakijaribu kupambana na hisia hizi, kwa kuzikataa, au kufunika kwamba hazipo. Lakini hii pia ni hatari sana. Ni sawa na moto unawaka na wewe kufunika moshi usionekane, moto utaendelea kuwaka na utaleta uharibifu mkubwa.

Njia bora ya kufanya ili kuondokana na hisia hizi hasi ni kuzikubali, kuzipokea, kuzielewa kwamba kuna kitu umekosa au umepoteza. Kisha kuchagua maisha yaendelee. Hujaribu kupambana kwa namna yoyote ile, bali unaelewa kwamba dunia ni tata na pamoja na wewe kuwa na mipango mizuri, bado hakuna aliyekuhakikishia kwamba utaifikia kwa asilimia 100.

Zikubali hisia hasi, jua zinatokana na nini, kubali ile hali iliyokutokea na chagua kuendelea na maisha, ukiendelea kuwa na matumaini kwamba mambo mazuri bado yapo na juhudi zako zitakuletea mambo hayo.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Njia Bora Ya Kujenga Upendo Wako Kwa Wengine.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba hasira na huzuni ni hisia mbili hasi ambazo zinatokea kwenye maisha ya kila mmoja wetu. Na hisia hizi siwezi kuziondoa kwa kuzikataa, bali kwa kuzikubali na kukubali kile kilichotokea na kukubali maisha yaendelee. Najua dunia ni tata, pamoja na malengo na mipango yangu mizuri, lolote linaweza kutokea na nipo tayari kwa lolote.

NENO LA LEO.

“Letting go gives us freedom, and freedom is the only condition for happiness. If, in our heart, we still cling to anything – anger, anxiety, or possessions – we cannot be free.” ― Hanh Nhat Thich

Kuachilia kunatupa uhuru na uhuru ndio hali pekee inayotuletea furaha. Kama kwenye mioyo yetu bado tumejishikiza na kitu, hasira, wasiwasi au umiliki hatuwezi kuwa huru.

Achilia mambo yaende na utaondokana na hasira na huzuni pia na utabaki kuwa huru.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.