Wanasema vitendo vinaonekana zaidi kuliko maneno yanavyosikika. Kwamba unaweza kusema sana, lakini watu wataona zaidi vitendo vyako.
Dunia inakusoma kwa kila unachofanya. Unaiambia dunia unachoamini na unachosimamia kupitia matendo yako ya kila siku.
Kuwa mtu wa kulalamika na kulaumu na unaidhihirishia dunia kwamba huna mamlaka juu ya kitu chochote kile, hata wewe mwenyewe.
Fanya kazi yenye makosa mengi na unaitangazia dunia kwamba hujali kuhusu kazi yako na uko tayari kuwa wa kawaida.
Wachukulie wateja wa biashara yako kwa ukawaida, na unaiambia dunia kwamba hujajitoa kujenga biashara kubwa na yenye mafanikio.
Wanyime haki yao wale ambao hawawezi kukufanya lolote na unaitangazia dunia kwamba hujali wengine na unajiangalia wewe mwenyewe tu.
Haijalishi unasema nini, haijalishi unataka kuonekanaje kwa wengine, lakini kile unachofanya kinaonekana zaidi. Na kupitia kile unachofanya, dunia inajua ni nini unachoamini na umejipangaje kuwa na maisha bora.
Dunia haina siri, hata kama kwa sasa hakuna anayekuona, haitachukua muda mambo yote yatakuwa hadharani.
Dunia inakusoma, je inakusoma kwa lipi? Hiki ni kitu unachotakiwa kukizingatia kila mara.
SOMA; NENO LA LEO; Mawazo, Maneno, Matendo, Haiba Na Hatima Yako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kwa jambo lolote ninalofanya, dunia inanisoma. Na hainisomi tu kwa kile nilichofanya bali kwa imani niliyonayo ambayo imenipelekea kufanya nilichofanya. Nitaendelea kuboresha kile ninachoamini na kuhakikisha natenda kulingana na imani niliyonayo.
NENO LA LEO.
“I never listen to what a person says. I look at what a person does because what they do tells me who they really are.”
― Patty Houser
Sisikilizi kile ambacho mtu anasema. Ninaangalia kile ambacho mtu anafanya kwa sababu kile anachofanya kinaeleza kwa ukweli mtu huyo ni wa aina gani.
Dunia inakusoma kupitia kile unachofanya, na siyo kile unachosema. Hakikisha unachofanya kinaendana na kile unachopenda kuwa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.