Je wewe ni mjasiriamali? Au unataka kuingia kwenye ujasiriamali? Kuna mambo muhimu sana unayotakiwa kujua katika safari yako ya ujasiriamali. Bila ya kujua mambo haya utajikuta kwenye wakati mgumu na hata kukata tamaa, kwa sababu ujasiriamali sio safari rahisi kama wengi ambao bado hawajaingia wanafikiri.
Karibu tujifunze mambo 100 ambayo kila mjasiriamali au anayetaka kuwa mjasiriamali anatakiwa kuyazingatia ili aweze kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.
Mambo haya 100 yametokana na kitabu ALL TIME ESSENTIALS FOR ENTREPRENEURS ambacho kimeandikwa na mwandishi JONATHAN YATES. Mambo haya 100 yamegawanyika kwenye makundi kumi yenye mambo kumi kila moja. Karibu tujifunze kwa pamoja.
KUNDI LA KWANZA; KUANZA.
1. Anza sasa. Chukua wazo lako, lile wazo ambalo limekuwa kwenye mawazo yako kwa muda mrefu, ambalo umekuwa ukiwaambia sana marafiki zako na anza kulifanyia kitu. Fanya chochote cha kulifanya wazo hilo kuwa uhalisia, liandike, fanya utafiti na anza kutekeleza.
2. Tafuta wakati wako wa uvumbuzi. Uvumbuzi hautokei mara moja tu, bali unatokana na kukifanyia kazi kitu muda mrefu. Unapokutana na changamoto kama hutakata tamaa ni lazima utapata wazo zuri sana.
3. Jua dhumuni lako kwenye maisha. Jua ni lipi dhumuni lako kwenye maisha, ukishalijua hili na kufanya biashara yako iendane na dhumuni hili utafanikiwa sana.
4. Jifunze kuuza wazo. Uwezo wa kuuza wazo ni msingi muhimu sana kwa mjasiriamali. Mara nyingi utakuwa na mawazo mazuri sana, lakini kama huwezi kumwelezea mtu akakuelewa, utakosa fursa nyingi.
5. Tumia muda wako vizuri. Matumizi mazuri ya muda ni ujuzi muhimu sana kwa kila mjasiriamali. Muda una thamani kubwa sana ukishapotea haurudi tena. Weka vipaumbele vyako na vifanyie kazi.
6. Washirikishe familia na marafiki kwa umakini. Wakati wa kuanza, familia na marafiki watakuwa watu wa karibu kukuunga mkono. Lakini familia na marafiki mara nyingi sio washauri wazuri kwenye biashara, kwa kukupenda sana wanaweza kukuzuia kuchukua fursa.
7. Kuwa tayari kubadilika. Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi sana, na wewe pia unahitaji kubadilika kwa kasi, la sivyo utaachwa nyuma.
8. Ondoka kwenye ajira. Je unafurahia kuajiriwa? Unafurahia kuwatengenezea wengine fedha nyingi na wewe kupata kidogo? Je unaweza kupata mteja mmoja wa kuanza naye kwenye biashara yako? jiulize maswali haya na chukua hatua bora kwako. Sio lazima uache kazi yako mara moja, unaweza kuanza bishara ukiwa bado umeajiriwa na mambo yakiwa mazuri unaacha kabisa kazi.
9. Tafuta mtaji wa kuanzia. Kujiwekea akiba na kisha kuanza nayo biashara ni moja ya njia bora za kuanzia biashara. Lakini pia kuna njia za nje kama mikopo, michango kutoka kwa watu wa karibu, na kupata wawekezaji. Jua ni njia ipi utaanza nayo na ipi utatumia baadaye.
10. Anza leo. Ni kitu gani kinaweza kukuridhisha kama kuwa msimamizi wa biashara yako mwenyewe? Kwa wazo ulilonalo, anza nalo leo, ukisubiri unaweza kukuta wengine wameshalifanyia kazi.
KUNDI LA PILI; MAWAZO.
11. Wewe ni wa pekee. Mkusanyiko wa matukio uliyopitia kwenye maisha yako mpaka sasa ni kitu cha kipekee sana kwako. Tumia uzoefu wako, na mtandao ulionao kuziona fursa zaidi za kibiashara. Hutakuja kukutana na mtu anayefanana na wewe kwa kila kitu, wewe ni wa pekee.
12. Tafuta matatizo ya kutatua. Angalia ni kitu gani kinawaumiza watu, au ni mahitaji gani wanayakosa, na hapo ndipo penye fursa kubwa ya kibiashara. Biashara zote zenye mafanikio zinatatua matatizo ya watu.
13. Wasikilize wateja wako. Wakati unauza bidhaa au huduma zako, wasikilize wateja wako na elewa mahitaji yao. Wateja tayari wanajua wanachokitaka, kwa kuwasikiliza utajua zaidi na kuwahudumia vizuri zaidi.
14. Fanya kitu unachofurahia kufanya. Fikiria ni vitu gani unavyopenda sana kufanya, kisha angalia ni jinsi gani unaweza kupata watu watakaokulipa kwa kufanya vitu hivyo. Utakapofanya biashara inayotokana na vipaji vyako, mafanikio ni uhakika.
15. Jifunze ujuzi mpya. Kama hutajaribu vitu vipya, huwezi kujua mizizi ya mafanikio yako iko wapi. Unahitaji kujifunza vitu vipya ambavyo vitakufanya ufikiri tofauti na ulivyozoea kufikiri.
16. Chukua wazo zuri na lifanyie kazi kwa ubora. Unaweza kupata fursa nzuri kwa mawazo ambayo tayari watu wanayafanyia kazi. Angalia ni maeneo gani ambayo unaweza kuyaboresha, na weka ubora zaidi.
17. Tumia nguvu ya ubunifu. Kila mmoja wetu ana ubunifu mkubwa, lakini tumeamua kutokuutumia. Watoto wadogo ni wabunifu sana kwa sababu wako huru kujaribu vitu mbalimbali. Anza na wewe kujaribu vitu mbalimbali na kujifunza vitu mbalimbali.
18. Thamini wanachopendelea wengine. Fanya utafiti kwenye kitu ambacho hupendelei wewe lakini wengine wanakipendelea, na jiulize kwa nini wanapendelea kitu hiko, unaweza kupata mawazo mazuri sana.
19. Linda mawazo yako. kama una wazo bora sana linaloweza kuleta mabadiliko makubwa, hakikisha unalilinda. Unaweza kulinda wazo lako kwa kuandikisha hatimiliki.
20. Tengeneza ushawishi mfupi wa wazo la biashara yako. je unaweza kumweleza mtu kuhusu biashara yako na akakuelewa na kuhamasika ndani ya sekunde 10? Huu ni muda wa watu walioko bize, unahitaji kuweza kufanya hivyo.
KUNDI LA TATU; HAMASA.
21. Wajibika kwa mabadiliko. Wajasiriamali wanayapokea mabadiliko, wanatengeneza mabadiliko na kuyafurahia mabadiliko. Acha kulalamika kwamba hupendi mambo yalivyo na fanya kitu kuleta mabadiliko. Mabadiliko ni magumu lakini hayakwepeki.
22. Usiishie kuota tu, fanyia kazi. Kukaa na kuongelea mawazo yako mazuri ni kitu kizuri, lakini unahitaji kufanyia kazi ndio mambo unayotaka yatokee. Kuna waongeaji na watendaji, wajasiriamali wenye mafanikio ni watendaji.
23. Pata mapumziko. Kuendesha biashara kuna gharimu sana muda wako na nguvu zako. Kila baada ya muda pata muda wa kuwa mbali na ofisi yako au biashara yako na tumia muda huu kufanya kitu cha tofauti kabisa ambacho hakihusiki na biashara yako. ni nyakati kama hizi unaweza kupata mawazo mazuri sana ya kuikuza biashara yako.
24. Weka malengo ili uweze kuyafikia. Kuwa na picha na vielelezo vinavyoonesha ndoto zako ofisini kwako au chumbani kwako. Kadiri unavyoona vitu hivi ndivyo inavyokuhamasisha kuweka juhudi zaidi ili kuyafikia. Kama unaweza kuona unakotaka kwenda, ni lazima utapata njia ya kukufikisha hapo.
25. Furahia kutokuwa na uhakika. Binadamu tunapenda kuwa na uhakika kwa kufanya kile ambacho tumezoea kufanya, lakini kufanya vitu vipya ambavyo hatuna uhakika navyo hatupendi. Ili ufanikiwe kama mjasiriamali unahitaji kuwa tayari kufanya vitu ambavyo huna uhakika navyo.
26. Pata taswira ya mafanikio yako. jitengenezee taswira ya mafanikio yako ya kibiashara. Jione ukiwa kwenye biashara yenye mafanikio, ukiingia mikataba mikubwa mikubwa. Kwa kujikumbusha taswira hii mara kwa mara itakupa hamasa ya kuweka juhudi zaidi.
27. Mezwa na kile unachofanya. Kwa jukumu lolote unalofanya, weka akili na mawazo yako yote kwenye kitu hiko. Kwa kufanya hivi utaona muda kama unapaa na hata majukumu magumu utayaona marahisi.
28. Usikate tamaa, endelea na mapambano. Kuna wakati utakutana na changamoto na mambo kuwa magumu. Huu ndio wakati ambao unahitaji kuweka juhudi zaidi maana utajifunza mengi na unakaribia makubwa.
29. Kama ingekuwa rahisi, kila mtu angekuwa anafanya. Kuanzisha na kuendesha biashara yenye mafanikio sio kitu rahisi, na ndiyo maana wachache sana wanaweza kuwa na biashara kubwa na zenye mafanikio. Jua hili mapema na jiandae kwa furaha na maumivu pia, siyo rahisi lakini ina thamani kubwa.
30. Tafuta kinachokuhamasisha. Kwa kuwa safari hii siyo rahisi, na kwa kuwa utakutana na vikwazo vingi, ni vyema kujua kipi kinakuhamasisha wewe kufanya biashara unayofanya. Katika nyakati hizo ngumu utajikumbusha kwa nini unafanya.
KUNDI LA NNE; FURSA.
31. Jua wewe upo kwenye kundi lipi kati ya makundi haya matatu ya wajasiriamali.
Kundi la kwanza ni wajasiriamali ambao wanasukumwa na kuleta mabadiliko kwenye mambo yaliyopo sasa, na siyo fedha pekee.
Kundi la pili ni wajasiriamali ambao wanasukumwa na kutengeneza fedha na utajiri na wanafanya kazi wao wenyewe.
Kundi la tatu ni wajasiriamali ambao wanaanzisha biashara na kuzikuza zaidi na pia kuwekeza kwenye biashara nyingine zaidi na zaidi.
32. Fanya utafiti. Kwa wazo lolote la biashara ulilonalo, lifanyie utafiti wa soko. Na kwa sasa mtandao wa intaneti umerahisisha mambo, unaweza kufanya utafiti kupitia mtandao wa intaneti.
33. Kuza mtandao wako binafsi. unajua nini ni muhimu, ila nani anakujua ni muhimu zaidi. Hudhuria matukio mbalimbali yatakayokukutanisha na wajasiriamali wenzako na hata wawekezaji. Kadiri unavyojulikana na wengi ndivyo unavyoongeza fursa zako.
34. Chukua kila fursa inayojitokeza mbele yako. kwa hitaji lolote ambalo mteja analo, lipokee na fanyia kazi. Kama huwezi basi tafuta mtu ambae yupo kwenye mtandao wako anayeweza kufanyia kazi.
35. Soma majarida mbalimbali. Kuna majarida ya kibiashara na ambayo yamelenga aina fulani za biashara. Tafuta majarida ambayo utakuwa unayasoma, ambayo yatakupa taarifa muhimu kuhusu biashara.
36. Tengeneza biashara ambayo unaweza kuikuza. Usiishie kufikiria kuanzisha biashara ambayo utaiendesha wewe mwenyewe tu. Anza biashara ukiwa na wazo na mpango wa kuikuza ili iwe kubwa sana na iendeshwe na watu wengine na wewe ubaki kuwa msimamizi tu.
37. Kuwa mstahimilivu. Jua ni kipi unataka na kipi unafanya au kutoa na ng’ang’ana nacho. Hata kama kila mtu anakupiga au kukukatisha tamaa, kama ni kitu unachoamini usikubali kurudi nyuma, mwisho wa siku utapata unachotaka.
38. Tafuta fursa kubwa. japokuwa utaanza biashara ikiwa ndogo, lakini usiache kutafuta fursa kubwa na kuziendea. Hata kama huna uwezo huo kwa sasa, utakapopata fursa kubwa utajisukuma na kukua zaidi.
39. Sikiliza wakosoaji na tumia ukosoaji wao. Ni lazima utafika wakati ambapo watu watakupinga na kukosoa wazo lako au biashara unayofanya. Sikiliza yale wanayosema na kama kuna unayoweza kutumia kuepuka changamoto yatumie. Lakini mara zote jikumbushe wewe ni wa pekee na endelea kuweka juhudi.
40. Zungukwa na akili kubwa. Unapoanza biashara hutaweza kujua kila kitu kwa undani wake kuhusu maeneo yote ya biashara yako. na hapa ndipo unapohitaji kuzungukwa na watu wenye uelewa mkubwa kwenye maeneo fulani ya biashara yako. tafuta watu wa aina hii na kuwa karibu nao, watakusaidia sana.
KUNDI LA TANO; CHANGAMOTO.
41. Yapokee matatizo yako. ili uweze kutatua matatizo ya biashara yako kwanza lazima uyakubali. Yapokee na tafuta taarifa muhimu kuhusiana na matatizo hayo kisha fanya maamuzi sahihi katika kuyatatua matatizo hayo.
42. Mambo yanapokuwa magumu, endelea kwenda. Wakati ambapo mambo yatakuwa magumu, na lazima yawe magumu, jikumbushe hamasa ya wewe kufanya biashara hiyo na weka mkazo kwenye yale mambo ambayo ni muhimu zaidi kwako.
43. Jifunze kutokana na makosa yako. huwezi kukwepa kufanya makosa kwenye biashara yako, kila mtu anafanya makosa. Jifunze kwenye kila kosa unalofanya na hakikisha hurudii tena kosa ambalo umeshalifanya.
44. Zishinde changamoto kubwa kwa urahisi. Pale unapokutana na changamoto kubwa, ichunguze kwa makini na ona ni njia ipi rahisi kupita ili kuweza kuivuka. Anza kwa kuandika vitu vitatu unavyohitaji kufanya ili kuondokana na tatizo hilo na anza kufanyia kazi.
45. Omba msaada. Unapokutana na changamoto kubwa, omba msaada kwa wale ambao unaona wanaweza kukusaidia kuondokana na tatizo hilo. Hakuna kitu watu wanapenda kama kuwasaidia wengine, usikazane peke yako.
46. Fanya maamuzi. Kufanya maamuzi bora siyo kazi rahisi, na maamuzi bora yanatokana na uzoefu wa kufanya maamuzi mengi. Anza sasa kufanya maamuzi na usihofie hilo.
47. Tafuta fursa kwenye kila changamoto unayopitia. Biashara inakua na kushika kila mara, ni lazima uweze kuziona na kuzitumia fursa kwenye kila wakati wa biashara yako. hata kama mambo ni magumu angalia ni kwa jinsi gani unaweza kunufaika.
48. Tatua changamoto yako kwa kugeuza swali. Kuiangalia changamoto kwa upande mmoja peke yake unaweza kushindwa kuitatua. Angalia upande wa pili kwa kugeuza swali lako. Kwa mfano badala ya kujiuliza kwa nini sipati wateja wengi, jiulize kwa nini wateja wengi hawapendi kuja kwenye biashara yangu. Kwa njia hii utaona njia nyingi za kutatua.
49. Jifunze kufikiri kwa ubunifu. Kama kuna njia umezoea kuitumia kutatua tatizo lakini bado hupati majibu, jaribu kutumia njia nyingine tofauti. Na njia bora ni kujifunza kufikiri kiubunifu kwa kuondokana na fikra zote ulizonazo sasa kuhusu jambo hilo na kuanza kufikiri upya kama ndio unalijua jambo hilo kwa mara ya kwanza.
50. Ukikutana na mambo magumu, hapo ndio pazuri. Jinsi biashara inavyokuwa ngumu ndivyo inavyokuwa na thamani kubwa. Kwa sababu kwa ugumu huo wengi watakimbia na mnabaki wachache ambao mmejitoa kweli kufanya biashara hiyo.
KUNDI LA SITA; FEDHA.
51. Simamia mzunguko wako wa fedha. Kila mtu anaweza kuanzisha biashara, lakini ni wachache sana wanaoweza kuanzisha biashara yenye faida. Mzunguko wa fedha ndiyo damu ya biashara yako, ukishindwa kuusimamia biashara inakufa.
52. Dhibiti matumizi yako. unapoanzisha biashara yako na wakati huo mapato yako chini, unahitaji kudhibiti sana matumizi yako. nunua vile vitu ambavyo ni muhimu tu, na kama kuna uwezekano wa kupata kitu bora kwa gharama ndogo au bure basi fanya hivyo.
53. Fanyia kazi biashara yako. kuendesha biashara na kufanyia kazi biashara yako ni vitu viwili tofauti kabisa. Watu hufikiri kukaa kwenye biashara na kufanya majukumu ya kila siku ndiyo kuifanyia kazi, hapo unaendesha biashara. Unahitaji kuiangalia biashara yote kwa ujumla ili uweze kuikuza zaidi.
54. Kuwa mratibu mzuri. Katika biashara yako, unahitaji kuratibu muda, watu, bidhaa, huduma, uzalishaji, ubunifu na fedha. Kama unaweza kujisimamia wewe mwenyewe, basi utaweza kuratibu na kusimamia vitu vingine vyote kwenye biashara yako.
55. Mara zote hitaji zaidi. Unaponunua kitu chochote kwa ajili ya biashara yako, uliza kupata kilicho bora zaidi. Usinunue tu kile kinachopatikana, taka kupata kilicho bora sana.
56. Tumia biashara yako kama sehemu ya mtaji. Unapopitia nyakati ngumu za kifedha, unaweza kuitumia biashara ambayo umeshaijenga kama chanzo cha mtaji. Hapa unaweza kuwakaribisha watu kuwekeza fedha zao na wewe kuwauzia hisa. Ni bora kumiliki asilimia kumi ya biashara yenye thamani ya mabilioni kuliko kumiliki asilimia 100 ya biashara yenye thamani ya mamilioni.
57. Tumia fedha za watu wengine. Usitumie fedha zako zote kwenye biashara, kama mambo yakienda vibaya utakosa pakuanzia. Kuna maeneo mengi ambayo unaweza kutumia fedha za wengine katika kukuza biashara yako. unaweza kuchukua mkopo, kutafuta wawekezaji na njia nyinginezo.
58. Wavutie wawekezaji kuwekeza kwenye biashara yako. na ili uweze kufanya hivi ni lazima uwe na mchanganuo wa biashara yako. wawekezaji wanataka kuona kama biashara yako ina soko la kutosha na mipango yako mingine ikoje. Ni muhimu kuwa na mchanganuo wa biashara yako ulioandikwa kitaalamu.
59. Punguza hatari ambayo wawekezaji wanahitaji kuingia kwa kuwekeza kwenye biashara yako. kama unataka watu wawekeze kwenye biashara yako, hakikisha wanaona fedha zao wanazoweka ziko salama. Hivyo kuwa na mpango mzuri ambao utaonesha matokeo mazuri, kama kuweka malengo ambayo yanafikika na kufanya vitu ambavyo sio hatari sana.
60. Jenga na tumia sifa nzuri ya biashara yako. katika mambo ya fedha, jijengee sifa nzuri ya biashara yako kwa kuiendesha kwa uwazi na pia kulipa madeni kwa wakati. Kwa njia hii utawavutia wengi kufanya biashara na wewe.
KUNDO LA SABA; MIKAKATI.
61. Kuwa mtaalamu aliyebobea. Kuwa mtaalamu aliyebobea kwenye biashara unayoifanya. Usiishie tu kuuza, bali pia kuwa mshauri kwa mambo yote yanayohusiana na biashara yako. andika makala za kuchambua mambo mbalimbali ya kijamii yanayohusiana na biashara yako na wengi watakuamini.
62. Kuwa na udhibiti wa biashara yako. kuwa na udhibiti wa biashara yako kwa kuisimamia vizuri na kuangalia mipango ya muda mfupi na muda mrefu. Usikubali matatizo madogo madogo yakusahaulishe kuangalia mbele kwenye ukuaji wa biashara yako.
63. Tengeneza utamaduni wa kipekee wa biashara yako. tengeneza hisia fulani ambayo mteja anaipata kwa kutumia bidhaa au huduma zako. Tengeneza utamaduni ambao utamfanya mteja ajione ni sehemu muhimu ya biashara yako.
64. Vunja mazoea. Mara nyingi watu huendesha biashara kama walivyozoea kuendesha siku zote. Mazoea haya huwazuia kujaribu vitu vipya. Huwezi kukuza biashara yako kama hupo tayari kujaribu vitu vipya. Vunja mazoea na jaribu vitu vipya.
65. Jaribu kufanya kitu kipya kabisa, ambacho hujawahi kufanya. Fanya kitu ambacho hakiendani kabisa na biashara yako, kitu ambacho hujawahi kufikiria au kuthubutu kufanya. Inaweza kuwa kusoma kitabu ambacho kiko tofauti na unavyoamini, kula chakula ambacho hujawahi kula au kuvaa nguo ambazo hujawahi kuvaa. Kwa kufanya mambo haya utapata mtazamo mpya.
66. Wafuatilie kwa karibu washindani wako. Wajue washindani wako kibiashara na pia kiubinafsi. Washindani wako ni chanzo kizuri cha wateja. Kujua kile wanachofanya na wasichoweza kufanya kutakusaidia kuikuza biashara yako.
67. Toa majukumu kwa wengine. Using’ang’anie kufanya kila kitu mwenyewe kwenye biashara yako. majukumu mengine tafuta watu wanaoweza kufanya vizuri na wape wayafanye. Hili litakupunguzia wewe majukumu ambayo siyo muhimu sana na hivyo kupata muda wa kufanyia kazi yale ambayo ni muhimu.
68. Mpigie mtu simu sasa hivi. Chukua simu yako na mpigie mtu unayemheshimu sana kwenye biashara na ongea naye kuhusu bidhaa au huduma unayotoa. Hakikisha unaongea naye mambo ya msingi yatakayokuwezesha kukuza biashara yako zaidi.
69. Ongeza mipaka yako. usiendeshe biashara yako kwenye maeneo yale uliyozoea peke yake, nenda hatua ya ziada kwa kuvuka mipaka na kufika mbali zaidi.
70. Fanya kwa ubora kuliko washindani wako. Unapoona mtu mwingine anafanya kitu ambacho unaona ni bora, jiulize je naweza kufanya kwa ubora zaidi ya hapo? Mshindani wako anapokuja na kitu kipya, jiulize je unaweza kutoa bora zaidi ya hapo? Na nenda hatua ya ziada.
KUNDI LA NANE; MASOKO.
71. Kuwa mwinjilisti wa huduma zako. Kama biashara yako haikuhamasishi wewe mwenyewe, haiwezi kuwahamasisha wengine. Hamasika na biashara yako na hakikisha kila unapokuwepo unawahamasisha watu kuhusu biashara yako.
72. Tengeneza jina la biashara yako. tengeneza jina la biashara yako, ambalo jina hilo litabeba maana nzima ya biashara yako. sio tu biashara unayofanya, bali kile ambacho mtu anafikiria anaposikia kuhusu biashara yako.
73. Washirikishe wateja wako kwenye biashara yako. kama mteja atajiona kama sehemu ya biashara yako, atakuwa mwaminifu sana kwenye biashara yako. wafanye wateja wawe wanaiongelea biashara yako mara nyingi, hii ni njia bora ya kujitangaza.
74. Toa ahadi kwa wateja wako. Jina la biashara yako linahitaji kuwa ahadi kubwa kwa wateja wako. Mteja anaponunua bidhaa au huduma yako, anakuwa na mategemeo makubwa ya kile atakachopata. Na hakikisha unatimiza ahadi hiyo.
75. Mshangaze mteja. Mfanye mteja wako ashangae kwa huduma bora sana anazozipata ukilinganisha na mategemeo yake au gharama anayotoa. Nenda hatua ya ziada kwenye kila jambo.
76. Tengeneza mvumo. Tengeneza kitu ambacho kitaivumisha biashara yako zaidi, kitu ambacho kitawafanya watu wawe wanaiongelea biashara yako. kadiri inavyoongelewa na wengi, ndivyo wengi watataka kuijua zaidi na hivyo kuongeza wateja wako.
77. Hakikisha unasikika. Usipige kelele ili kusikika, bali kuwa na mawasiliano bora na wateja wako. Jenga mahusiano mazuri ambayo yatawafanya wateja wajue upo na unawezaje kuwatatulia matatizo yao. Usiwe wa kutangaza tu, kuwa wa kutatua matatizo.
78. Tengeneza familia ya bidhaa au huduma. Unapoanza na bidhaa au huduma moja na ikawa na mafanikio makubwa, angalia jinsi gani unaweza kuanzisha bidhaa au huduma nyingine itakayoendana na hiyo. Ongeza wigo wa bidhaa au huduma unazotoa.
79. Tengeneza mahusiano mazuri na uma. Jiweke karibu na umma kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kufanya mawasiliano ambayo yanaitambulisha biashara yako kwa jamii inayokuzunguka.
80. Kuwa msumbufu kwa upande chanya. Kama kuna mambo yaliyozoeleka kwenye biashara unayofanya, ambayo hayana tija, yapinge na onesha ni njia ipi bora ya kuchukua. Kufanya hivi utafanya wengi watake kujua zaidi biashara yako na hivyo kuikuza.
KUNDI LA TISA; MAUZO.
81. Mpe mteja zaidi ya alichotegemea kupata. Mara zote angalia njia za kuongeza thamani zaidi kwa mteja wako. Kwa mfano unaweza kumpa mteja zawadi baada ya kununua kiasi fulani cha bidhaa zako. Vitu kama hivi vinamfanya mteja aje tena kwako wakati mwingine.
82. Uza manufaa na sio sifa za bidhaa. Usimwambie mtu nakuuzia bidhaa hii ambayo ni bora sana kuwahi kutokea duniani. Bali mwambie mtu nakuuzia bidhaa hii ambayo itatatua matatizo yako uliyonayo sasa. Watu hawataki kujua sana kuhusu bidhaa ikoje, wanachotaka kujua ni inawasaidiaje wao.
83. Tengeneza sifa nzuri kwa wateja wako. Mfanye kila mteja anayenunua kwako aondoke akiwa na hamu ya kurudi tena kuja kununua kwako. Wajali sana wateja wako na wafanye waone wananufaika zaidi kwenye biashara yako kuliko sehemu nyingine yoyote.
84. Omba rufaa kwa mteja wako. Mteja anaponunua kwako, mwombe akuambie ni mtu gani wa karibu kwake ambaye anaona anaweza kunufaika na biashara yako ila bado hajaijua. Mwombe mteja akawaambie watu wa aina hiyo ili nao wanufaike na biashara hiyo, ila hakikisha umemridhisha mteja ndiyo umwombe rufaa.
85. Toa ushauri wa bure kwa wateja wako. Usiwe tu muuzaji, pia kuwa mshauri kwa wateja wako, washauri ni kipi bora wao kufanya, hata kama hakikupi faida wewe. Ukiwashauri vizuri na wakapata wanachotaka, hawatakusahau.
86. Kuwa sehemu ya timu ya mteja wako. Mfanye mteja wako akutegemee wewe kwa kupata kile ambacho anakitaka. Kwa wewe kuwa tegemeo lake, ni vigumu sana mshindani wako kumpata mteja wa aina hiyo.
87. Tengeneza huduma bora sana kwa wateja. Kama kuna tatizo lolote ambalo mteja wako analipata kwa kutumia bidhaa au huduma zako, zingatia na tatua tatizo hilo.
88. Usiwe na wateja, kuwa na marafiki. Biashara inafanywa na watu, na watu wanapokuwa marafiki wanaaminiana zaidi. Wafanye wateja wako kuwa marafiki zako na watakuamini zaidi na kuwa sehemu ya biashara yako.
89. Waambie watu wanunue. Unaweza kumweleza mtu vizuri sana kuhusu biashara yako na akakuelewa, ila ukasahau kitu kimoja, kumwambia anunue. Ukishamweleza mtu kuhusu biashara yako msisitize anunue, kwa njia hii utahamasisha wengi kununua.
90. Patana kwa kila fursa. Unapouza au kununua hakikisha unapatana na unayefanya naye biashara na kuhakikisha wote mnanufaika. Usivutie tu upande wako, unaweza kupoteza wateja.
KUNDI LA KUMI; MAFANIKIO.
91. Kuwa na mtizamo sahihi. Kuwa na mtizamo sahihi kuhusu biashara yako, usikubali mafanikio au kushindwa kukuvuruge na ukajisahau. Kumbuka mambo sio mazuri au mabaya kama yanavyoonekana kwa nje.
92. Kufanya kazi kwa juhudi kunalipa. Hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa kwenye biashara, ni lazima uweke kazi sana, ni lazima uweke nguvu na ni lazima uweke muda na gharama pia. Usitafute njia ya mkato, kuwa tayari kuweka juhudi kubwa.
93. Watu wakikuambia HAPANA, uliza tena. Mtu yeyote anayekuambia hapana kwa pendekezo lako, usikubali na kuishia hapo, chunguza kwa nini wanasema hapana na uliza tena kwa njia bora. Ni rahisi sana kwa watu kukuambia hapana kwenye biashara, kuwa mgumu na endelea kuuliza mpaka upate unachotaka.
94. Tengeneza bahati yako mwenyewe. Kuna nyakati chache sana ambapo mtu anaweza kufanikiwa kwenye biashara kwa bahati. Lakini mara zote wanaofanikiwa na wewe ukaona wanabahati jua wametengeneza bahati hizo wao wenyewe. Kwa kuwa na maandalizi ambayo yamekutana na fursa.
95. Furahia mafanikio madogo madogo. Mafanikio madogo madogo unayopata kwenye biashara yako ndiyo yanajenga mafanikio makubwa ya baadaye. Yafurahie mafanikio haya na utavutia mafanikio mengi zaidi. Kila hatua unayopiga inakusogeza karibu na malengo yako.
96. Tengeneza suluhisho la matatizo. Kama utaweza kutatua tatizo ambalo linawasumbua mamilioni ya watu, basi tayari umeshapata bidhaa na soko. Tafuta kile kinachowatesa watu na angalia kama kuna fursa unayoweza kuitumia.
97. Weka malengo mazuri ambayo utaweza kuyafikia. Kushindwa kufikia malengo yako kwa sababu ambazo ziko nje ya uwezo wako kunaweza kukuumiza sana. Weka malengo ambayo hayawezi kuzuiwa na sababu zilizopo nje ya uwezo wako, na weka nguvu zako zote ili kuyafikia.
98. Kua kuzifikia changamoto. Tumia changamoto unazokutana nazo kwenye biashara yako kukukuza na kukukomaza zaidi kwenye biashara yako. hakikisha unapoitatua changamoto unakuwa mtu tofauti na ulivyokuwa kabla ya changamoto hiyo.
99. Fanya kila kilichopo ndani ya uwezo wako kutekeleza wazo lako. Hakikisha hakuna kitu chochote kinachokuzuia wewe kutekeleza biashara yako. weka juhudi zako zote, weka maarifa na ujuzi wako na nenda hatua ya ziada kuhakikisha biashara unayotaka kufanya umeifanya kwa mafanikio makubwa.
100. Kuwa mjasiriamali. Fanya kila unachofanya kama mjasiriamali. Usiseme hujazaliwa kuwa mjasiriamali, wajasiriamali hawazaliwi, bali wanajitengeneza wao wenyewe. Ukifanya kile unachofanya kama mjasiriamali, na ukaweza kutekeleza wazo lako la biashara, tayari wewe ni mjasiriamali. Na watu watakuona kama mjasiriamali.
Yafanyie kazi mambo haya 100 uliyojifunza, na utakuwa mjasiriamali bora na mwenye mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri,
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,