Chukua miti miwili, mti mmoja umeota sehemu ambayo kuna upepo mkali sana na hakuna maji ya uhakika. Na mti mwingine umeota sehemu ambayo ni tulivu, hakuna upepo na maji yapo ya kutosha. Unafikiri kati ya miti hii miwili ni upi utakuwa na mizizi imara?

Mti ulio ota sehemu yenye upepo mkali, ni lazima uwe na mizizi imara kwa sababu bila ya mizizi hiyo usingeweza kudumu, ungeng’olewa na upepo. Na pia kwa sababu maji siyo ya uhakika, mizizi ya mti huo lazima iende mbali zaidi na hivyo kuzidi kuongeza uimara wake.

Mti ulio ota sehemu tulivu kabisa na yenye maji mengi hauna haja ya kuwa na mizizi imara. Kwa sababu hakuna usumbufu wowote na maji yapo karibu.

Hii ni sheria ya asili, kwamba mambo yanapokuwa rahisi na viumbe navyo vinakuwa rahisi na mambo yanapokuwa magumu na viumbe pia wanakuwa wagumu.

Hii pia ipo kwetu binadamu. Kadiri unavyopitia hali ngumu ndivyo unavyojijengea misingi imara ya maisha yako. tofauti na yule ambaye hapitii magumu, anakosa uimara na inapotokea mambo yanabadilika anapata taabu sana.

Unapopitia changamoto au magumu kwenye maisha yako, kumbuka ya kwamba hiyo ni njia ya wewe kuwa mgumu na imara zaidi. Kwa mtazamo huu utachukulia changamoto kuwa sehemu muhimu kwa ukuaji wako.

SOMA; Jenga biashara yako kwenye misingi hii mitatu na itakuwa imara.

TAMKO LANGU;

Nimejikumbusha ya kwamba ugumu wa mazingira unazalisha viumbe imara sana. Hivyo sitalalamika tena nitakapokuwa napitia changamoto na hali ngumu, badala yake nitachukulia kama sehemu ya mimi kukua na kuwa imara zaidi.

NENO LA LEO.

“A tree stands strong not by its fruits or branches, but by the depth of its roots.” ― Anthony Liccione

Mti unasimama imara siyo kwa sababu ya matunda au matawi yake, bali kwa urefu wa mizizi yake.

Jenga misingi yako, hii ndiyo itakayokuwezesha kusimama imara hata mambo yanapokuwa magumu kiasi gani.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.