Kwenye maeneo mengi ya maisha yetu tunahitaji usawa, kwa sababu binadamu wote ni sawa, hivyo kila mtu anastahili kupata huduma sawa, hii ni kweli kabisa.
Lakini kuna maeneo kwenye maisha yako ambayo huhitaji kabisa usawa na mtu mwingine yeyote. Yaani kwenye maeneo hayo ukikubali usawa tu umejipoteza mwenyewe.
Kwa mfano ukienda kwenye msitu na miti yote ikawa inalingana kwa kimo, utakachoona ni msitu pekee. Lakini kama utafika kwenye msitu wenye miti mingi inayolingana, lakini kukawa na mti mmoja mrefu kuliko wenzake, utaanza kuona mti ule kabla ya miti mingine.
Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwenye kazi yako au biashara yako. usikubali kabisa kuwa na usawa na wengine kwa kazi unayofanya au biashara unayofanya.
Tafuta kuwa tofauti, tafuta kuwa bora zaidi na tafuta kufanya kwa kipekee.
Kwa kuwa kila unachofanya kila mtu anaweza kufanya, njia pekee ya kusimama ni kuwa tofauti na wengine wote.
Na uzuri ni kwamba unaweza kuwa tofauti, uamuzi ni wako wewe mwenyewe, kuamua kuweka ubunifu na kuongeza ubora ili kuboresha kile unachofanya zaidi. Na kipimo chako kikiwa kutoa huduma bora kabisa kwa wengine.
TAMKO LANGU;
Nimejikumbusha ya kwamba kitu pekee kinachoonekana ni kile ambacho kipo tofauti na wengine. Kwenye dunia ya sasa ambayo watu wengi wanafanya ninachofanya, njia pekee ya kusimama na kuonekana ni kuwa tofauti na wengine. Kila siku nitaongeza ubora na kuwa tofauti na wengine huku nikiweka mkazo katika kutoa huduma bora zaidi.
NENO LA LEO.
In order to be irreplaceable one must always be different. – Coco Chanel
Ili uwe wa kipekee na akosekane wa kuziba pengo lako, kuwa wa tofauti.
Usikubali kuwa sawa na wengine kwenye kazi yako au biashara yako. Hii ni njia ya uhakika ya kushindwa, iepuke kwa kuamua kuwa tofauti, kuwa mbunifu na kuweka ubora.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.