Pamoja na hofu zote ulizokuwa nazo siku za nyuma kuhusu siku za sasa, nyingi hazijatokea. Na hata kama zimetokea mambo hayakuwa mabaya kama ulivyokuwa unafikiria. Nina hakika na hili kwa sababu bado upo na bado unaendelea kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Umekuwa ukihofia ya kwamba mambo yatakwenda vibaya, na kuanguka sana kwa kile ambacho unafanya, lakini sehemu kubwa ya hofu zako hazijatokea.

Vitu vingi unavyohofia leo kuhusu kesho yako, havitatokea, japo kwa sasa unaweza kuwa unaogopa sana, lakini nina hakika asilimia 90 ya unavyoogopa sasa wala havitatokea.

Hivyo acha kuitumia hofu kama sababu ya wewe kuacha kuchukua hatua, kwa sababu sehemu kubwa ya hofu zako hazitatokea.

Badala ya kuitumia hofu kama kikwazo, itumie hofu kama taarifa, kama tahadhari kwamba kuna uwezekano wa mambo kwenda tofauti na ninavyotegemea. Na kwa kuwa na taarifa hizi utaweza kujiandaa vyema ili usifikie kwenye hali mbaya.

Usikubali hofu ikuzuie kufanya makubwa, bali itumie kama kichocheo cha wewe kwenda mbali zaidi.

SOMA; Hizi ndio Hofu mbili ulizozaliwa nazo, nyingine ni uongo.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba pamoja na hofu nyingi ambazo nimekuwa nazo, nyingi hazijawahi kutokea na hata zilizotokea mambo hayakuwa mabaya kama nilivyokuwa nategemea. Kuanzia sasa nimeamua kutokurudishwa nyuma na hofu, nitaitumia hofu kama kichocheo kwangu kufanya kwa ubora zaidi.

NENO LA LEO.

“Fear is not real. The only place that fear can exist is in our thoughts of the future. It is a product of our imagination, causing us to fear things that do not at present and may not ever exist. ― Will Smith

Hofu siyo kitu halisi. Sehemu pekee ambapo hofu ipo ni kwenye mawazo yetu ya siku zijazo. Ni zao la taswira tunayojijengea, inayotufanya tuhofie vitu ambavyo havipo sasa na huenda visiwepo kabisa.

Usikubali hofu ikuzuie, bali itumie kama kichocheo.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.