Naamini kama ningeuliza maoni ya watu mia ambao ningekumbana nao, na kuwaulizia matamanio yao thabiti katika maisha yao, wengi sana wangejibu, furaha. Sote mara nyingi tupo kwa ajili ya kutafuta furaha, lengo lenye kuleta amani ya moyo na ufahamu ya kwamba kila kitu kipo sawa.
Kila ukichunguza shughuli nyingi anazo fanya binadamu ni kwa ajili ya kupata furaha hasa ya kweli. Kama wote tunahitaji furaha, kitu cha kujiuliza ni kitu gani ambacho wakati mwingine kinaweza kukupotezea furaha? Kwa kawaida huwa yapo mambo mengi ambayo yanaweza kukupotezea furaha.
Ni vyema kuwa makini na mambo haya ili yasiwe sababu ya kukupotezea furaha na kukufanya ukaishi bila amani. Kumbuka siku zote unapojihisi huna furaha ni kwa sababu ya vizuizi fulani fulani ambavyo tunakwenda kuviangalia hapa. Je, unajua ni vizuizi au mambo yepi yanaweza kukunyima furaha? Karibu kujifunza.
1. Kujilinganisha na wengine.
Hii ni moja ya sababu kubwa sana inayokupotezea furaha katika maisha yako. Unapojilinganisha na wengine inakuwa inakupelekea sana wewe kukuzalishia hisia nyingi hasi. Hiyo yote hutokea kwa sababu kwanza utaanza kujikosoa kwa kujiona hufai. Kumbe kitu kikubwa ambacho unakuwa umekisahau ni kwamba ulikuja duniani ukiwa peke yako tu. Hivyo unataka kuwa na furaha acha kujilinganisha na wengine.

FURAHIA MAISHA YAKO KWA KUFANYA UNACHOPENDA.
2. Majuto.
Kuangalia nyuma hasa pale ulipokosea mara nyingi huleta majuto na kusababisha ukakosa furaha moja kwa moja. Kama kuna sehemu ulikosea basi, anza upya hiyo imeshapita. Jenga utamaduni wa kujisamehe wewe na wengine. Kitu kikubwa acha kujuta kwa mambo ambayo yameshapita. Upo katika siku nyingine ya kutengeza mafanikio yako tena ikiwa pamoja na furaha. Ukijifunza hili vizuri la kutokujutia mambo ya nyuma utamudu kujitengenezea furaha ya kudumu.
3.  Kushindwa kukubaliana na ukweli.
Inapotokea wakati mwingine ukashindwa kukubaliana na ukweli wa kile kinachokutokea katika maisha yako huwa ni rahisi sana kwako kuweza kukosa furaha. Kama kuna kitu kimekutokea na ni kibaya kwako, jaribu kukubaliana nacho kwanza wakati unatafuta majibu. Lakini ukiendelea kupingana na ukweli jinsi ulivyo itazidi kukupotezea furaha kwa muda mrefu na utaona maisha yako kama hayana maana.
4. Kutokuwa na uhakika wa mambo.
Kuishi maisha huku ukiwa huna uhakika mkubwa sana wa kesho yako itakuwaje ni kitu ambacho ni rahisi kukupotezea furaha. Tuchukulie kwa mfano ukawa unadaiwa ada ya mtoto kule shule na inatakiwa ndani ya wiki moja. Kama huna uhakika wa kuipata pesa hiyo ni lazima utakosa furaha. Kutokuwa na uhakika wa jambo lolote lile ambalo lina manufaa kwako ni chanzo kikubwa sana cha kukosa furaha.
5. Hukumu.
Unapohukumu wengine, pia ukajihukumu mwenyewe hilo huwa ni jambo ambalo linakupotezea furaha. Hukumu ni kama matokeo ya kitu ulichonacho tangu ulipozaliwa, lakini huleta upotevu wa furaha kuliko utathamani wake. Siku zote jaribu kufanya jitihada ya kutokujihukumu wewe wala kuwahukumu wengine. Kwa kadri utakavyojihukumu wewe au wengine utazidi kujipotezea furaha kwa kadri siku zinavyokwenda.
6. Mashaka binafsi.
Kizuizi kikubwa cha furaha ni kujihisi si wa thamani na kutokujiamini . Unapokuwa unajitengeezea mawazo kama haya ya mashaka yako binafsi hilo liko wazi lazima utakosa furaha. Acha kujitengenezea mashaka binafsi kwa kufikiria sana kile unachokosa. Weka mkazo mkubwa kwa yale mambo unayotaka yakutokee. Hiyo itakusaidia kukujengea furaha ya kweli.
7. Uwoga.
Ninaweza kusema tunaishi katika dunia ambayo imejaa uwoga. Bila shaka tunaona habari nyingi zaidi ambazo msingi wake mkubwa umejikita katika hofu. Kwa jinsi tunavyozidi kuwa na habari au mambo kama haya yanayotujaza woga si rahisi sana kuwa na furaha kwa mazingira kama haya. Haya ni mazingira ambayo yatakupotezea furaha hata ufanyaje.
Nakutakia siku njema na endelea kujifunza kupitia AMKA MTANZANIA kila siku.
Kwa makala nyigine nzuri za maisha na mafanikio tembelea pia DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika.

Shukrani za pekee zimwendee Arthur Chikoka kwa kutushirikisha makala haya.