Kama ambavyo nimekuwa nakuambia mara nyingi, kwenye biashara usiingie kwenye mashindano ya moja kwa moja na washindani wako, maana hii itakuumiza zaidi ya kukujenga.
Unapoingia kwenye mashindano ya moja kwa moja, mshindani wako anaweza kufanya jambo lolote ambalo linaweza kuwaathiri wote wawili kwenye biashara zenu.
Lakini pia nimekuwa nakushirikisha mbinu bora sana za kushindana ambapo siyo za moja kwa moja. Na moja ya mbinu hizo ni kuwa bora kila siku katika biashara yako. kila siku kuongeza thamani zaidi na kuhakikisha mteja wako anaridhika.
SOMA; BIASHARA LEO; Mambo Ya Kuzingatia Unapojikuta Kwenye Ushindani Wa Bei.
Leo nakuongezea silaha nyingine ambayo itakuwezesha kumwacha mshindani wako mbali sana. Na uzuri wa silaha hii ni kwamba shindani wako hawezi kuitumia kukuumiza. Kwa mfano ukisema unamkomoa mshindani wako kwa kupunguza bei, anaweza kukuumiza sana hapo kwa yeye kupunguza bei zaidi yako.
Silaha ninayotaka kukushirikisha leo ni kutengeneza jina zuri la biashara yako. na hapa simaanishi lile jina ambalo umeipa biashara yako, bali ni ile sifa ambayo biashara yako inayo kwa watu wengine. Na sifa hii inaanza na wateja wako na wanaisambaza kwa wengine wengi.
Sifa yako nzuri ya biashara mshindani wako hawezi kuitumia vibaya dhidi yako. weka nguvu kwenye kujenga sifa nzuri, kwa kuwa na viwango ambavyo vinahakikisha mteja anapata huduma bora sana na anaridhika.
Nikudokeze hiki muhimu sana, kujenga jina na sifa siyo kitu cha mara moja na wala siyo kitu cha muda mfupi. Unahitaji muda mrefu na unahitaji kufanya hivi kila siku kwa siku zako zote za kibiashara.
Kila la kheri.
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
shukrani sana kwa makala hiyo kuhusu kumshind mshindani wako.
Samahani, Siku zote umekuwa unasisitiza kuwa ni vema unapoingia kwenye biashara usishindane sasa ningependa unisiadie ni viashiria gani mfanyabiashara anaweza kuwa navyo na kudhihirisha kuwa anashindana katika biashara.
Naomba unisaidie baadhi ya viashiria vinavyonyesha mtu anashindana katika biashara.
Shukrani.
LikeLike