Watu huwa wanakejeli vitu ambavyo wanavihofia au ambavyo wao wenyewe hawawezi kuvifanya.
Na hivyo wanapomwona mtu mwingine anafanya, inawaumiza na ili kujiondolea maumivu hayo wanakejeli.
Wanatengeneza hadithi zao ambazo zitawafanya wao wawe sahihi kuliko yule ambaye amechagua kufanya kitu cha tofauti. Na watakuwa na maneno mengi ya kejeli.
Vitu viwili vya kuondoka navyo hapa leo.
1. Usiumie au kukata tamaa kwa kejeli za watu, chunguza kwa makini na utajionea mwenyewe kama wanachosema ni kweli au ni kuficha udhaifu wao. Angalia wale wanaokukejeli wewe ni kipi kikubwa ambacho wamewahi kufanya kwenye maisha yao. Kama hakuna basi hata wasikusumbue, wafute kwenye mawazo yako haraka sana.
2. Usikejeli wengine. Kiuhalisia ukisikia kuna mtu anafanya kitu kikubwa kuliko wewe, au amechukua hatua ambazo wewe hujawahi kufikia, kuna mawazo hasi yatakujia. Kwamba anachofanya siyo, au kuna mahali anakosea, au kuna upendeleo amepata. Mawazo haya yanapokujia yaondoe haraka sana na weka mawazo chanya, ya kumshukuru kwa kuchukua hatua kwa sababu itafungua milango kwa wengi. Na kumpongeza pia kwa hatua yake. Na kama huwezi kufanya hayo basi kaa kimya.
Usikubali kejeli ikuingie, usishiriki kejeli.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Art Of Living(Mwongozo wa kuishi maisha ya furaha na mafanikio.)
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba wale wanaokejeli yale makubwa yanayofanywa ni watu ambao wanahofia kufanya makubwa, au hawawezi kuyafanya. Sitawasikiliza tena watu hawa na pia sitakuwa mmoja wa watu hawa.
NENO LA LEO.
Ridicule is the tribute paid to the genius by the mediocrities. Oscar Wilde
Kejeli ndiyo zawadi ambayo wajinga huwa wanawapa wenye akili.
Usikubali kejeli za watu zikurudishe wewe nyuma, maana hawajui. Na pia usishiriki katika kuwakejeli wengine.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.