Pamoja na kwamba wewe ni mfanyabiashara, bado pia wewe ni mteja kwenye biashara za wengine. Ukianzia na unapopata mahitaji yako muhimu na hata unapopata huduma nyingine muhimu kwako.
Usiishie tu kuwa mteja, bali hakikisha kupitia uteja wako unajifunza mbinu za kuboresha biashara yako.
Kila unapokwenda kununua kwenye biashara nyingine, jiulize ni kipi umefurahia kwenye biashara ile na kipi ambacho kimekukwaza.
Kama kuna biashara fulani ambayo ndiyo unapendelea kununua pale, jiulize kwa nini unapenda kununua pale pekee.
Ukishajua ni kipi kinakufurahisha pale, jiulize ni jinsi gani na wewe unaweza kuwafanya wateja wako wafurahi kama ulivyofurahi wewe.
Na kama kuna kitu kinakukwaza, hakikisha na wewe hufanyi hivyo kwenye biashara yako.
Na pia kama unakwenda kununua kwenye biashara nyingine kwa sababu hakuna kwingine unakopata unachopata pale, jiulize na wewe unaweza kuwaje wa kipekee kiasi kwamba wateja wako inabidi waje kwako tu.
Tumia uteja wako kwenye biashara nyingine kuwa sehemu kubwa ya kujifunza na kuboresha biashara yako. mambo ni mengi sana ya kujifunza, kama utafungua macho yako kuangalia na kufungua masikio yako kusikiliza, utazipata mbinu nyingi za kuboresha biashara yako.
Anza kufanyia kazi hili sasa, na biashara yako haitabaki kama ilivyo sasa.
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,