Tunapenda kutatua matatizo ya wengine, kila mmoja wetu ana ndoto kubwa ya kutatua matatizo ya dunia, kuibadili dunia, kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi.
Ila haya yote yanawezekana kama hiki kimoja kitafanyika, kuanza kutatua matatizo yako kwanza.
Ni lazima uanze na matatizo yako kwanza, uweze kuyatatua, na baada ya kuyatatua ndiyo unaweza kutatua matatizo ya wengine.
Kutatua matatizo yako kwanza kunakupa haya mawili muhimu;
1. Kunakupa uzoefu wa jinsi unavyoweza kutatua matatizo na hivyo kuweza kuwashirikisha wengine njia ulizotumia wewe.
2. Kunakupa amani ya moyo, unakuwa na utulivu kwamba tayari matatizo yako yameshatatuliwa. Kujaribu kutatua matatizo ya wengine wakati bado ya kwako yanakusumbua, mawazo yako hayatakuwa kwenye kile unachofanya na hivyo huwezi kufanya kwa ubora.
Anza na matatizo yako mwenyewe, kisha yafanyie kazi matatizo ya wengine na matatizo ya dunia.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba ili niweze kutatua matatizo ya wengine vizuri, nahitaji kutatua matatizo yangu kwanza. Kwa kutatua matatizo yangu nitakuwa na uzoefu mzuri na pia nitapata amani ya moyo na hivyo kuweza kusaidia kwa moyo mmoja.
NENO LA LEO.
“Every problem is a gift – without problems we would not grow.” ― Anthony Robbins
Kila tatizo ni zawadi, bila ya matatizo hatuwezi kukua.
Tatua matatizo yako kwanza kabla hujatatua ya dunia, utapata uzoefu wa kutatua na pia utapata amani ya moyo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.