Kuna mazungumzo ambayo ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu, ila mazungumzo haya yanakuwa magumu kufanya kutokana na unyeti wake na umuhimu wake pia. Katika hali kama hii watu wengi hushindwa kutoa kile walichonacho mioyoni mwao na hivyo kubaki wanaumia au kuzikosa fursa muhimu kwao. Mazungumzo kati yako na mwenza wako, kati yako na watoto wako au wazazi wako na mazungumzo kati yako na mwajiri wako yanaweza kuwa magumu sana, hasa pale ambapo kunakuwa na tatizo baina yenu. Haya ni mazungumzo ambayo wengi wapo tayari kuyaepuka.
Lakini kuepuka mazungumzo haya magumu hakukusaidii wewe wala yule ambaye ulitaka kufanya naye mazungumzo hayo. Badala yake unaleta hali ngumu zaidi kwa wewe ambaye ulitaka kufanya mazungumzo hayo.
Ni changamoto hii ya kufanya mazungumzo magumu iliyowafanya waandishi Douglas Stone, Bruce Patton na Sheila Heen kuandika kitabu DIFFICULT CONVERSATIONS, How To Discuss What Matters Most. Kitabu hiki kimeeleza kwa kina mbinu za kufanya mazungumzo haya magumu na hapa nimekuandalia mambo 20 muhimu niliyojifunza kwenye kitabu hiki.
Karibu tujifunze kwa pamoja;
1. Inapofikia kwenye mazungumzo magumu watu wengi hujikuta njia panda. Hujikuta na mawazo ya mambo mawili, moja ni kuepuka mazungumzo hayo au tatizo lililopelekea mazungumzo yahitajike, na mbili ni kufanya mazungumzo hayo. Kuepuka hali hiyo kunatufanya tujisikie vibaya na kuona kama hatujitendei haki. Na wakati huo pia kufanya mazungumzo hayo tunaona kama tutafanya mambo yawe mabaya zaidi.
2. Kuna mazungumzo ya aina tatu, katika matatizo au changamoto zote tunazokutana nazo kwenye maisha, tunaweza kukusanya mazungumzo hayo katika makundi matatu.
Kundi la kwanza ni NINI KIMETOKEA, hapa kinachotakiwa kuzungumzwa ni kitu gani kimetokea au hakikutokea, nani kasema nini, na nani kafanya nini. Pia kwenye mazungumzo haya kunakuwepo na hali ya nani yupo sahihi na nani amekosea, na pia nani wa kulaumiwa.
3. Aina ya pili ya mazungumzo magumu ni yale yanayohusisha hisia zetu. Je kile ambacho tunahisi kipo sawa, je ni sahihi. Je vipi kuhusu hisia za wengine, je wamekasirishwa au kuumizwa. Haya ni mazungumzo ambayo yanahusisha hisia za kila mtu anayehusika kwenye tatizo au changamoto inayohitaji kufanyiwa mazungumzo.
4. Aina ya nne ya mazungumzo ni yale yanayohusu utambulisho. Haya ni yale mazungumzo ambayo tunakuwa nayo sisi wenyewe kuhusu kilichotokea kina maana gani kwetu. Hapa tunakuwa na mjadala ndani yetu kama kilichotokea kinatufanya tuonekane tunajua au hatujui, tunaweza au hatuwezi, ni watu wabaya au watu wazuri, tunafaa kupendwa au hatufai. Majibu ya maswali hayo yanachangia sana katika kufanikisha mazungumzo yetu.
5. Mazungumzo ya NINI KIMETOKEA ndiyo yanatawala sehemu kubwa sana ya mazungumzo yetu ya kila siku. Na mazungumzo haya yamegawanyika katika sehemu tatu kuu muhimu sana.
Sehemu ya kwanza ni ukweli. Hapa tunakazana kujua ukweli hasa uko wapi, ni nani yupo sahihi na nani amekosea, ni nani alifanya au kutokufanya kitu fulani na mengine kama hayo.
6. Sehemu ya pili ya mazungumzo ya NINI KIMETOKEA ni kusudi. Je kitu hiki kimefanyika kwa kusudi gani, aliyefanya alikuwa na nia gani, alidhamiria nini. Kama kusudi lake halikuwa baya basi inapunguza ukali, kama kusudi lilikuwa baya basi mambo yanakuwa magumu zaidi.
7. Sehemu ya tatu ya mazungumzo ya NINI KIMETOKEA ni lawama. Hapa tunaangalia ni nani wa kulaumiwa kwa kilichotokea, nani abebe lawama, ni nani amesababisha yote haya. Hapa ndipo panapokuwa pagumu sana kwenye mazungumzo yoyote.
8. Kutafuta lawama kunatuzuia kuona ukweli wa mambo. Kwa sababu unapolaumu unajiondoa kabisa kwenye tatizo husika, na hivyo unaona upande mmoja pekee. Njia pekee ya kuhakikisha unapata ukweli ni kuepuka lawama na badala yake kuangalia mchango wa kila mtu kwenye kile kilichotokea. Hapa inakuwa rahisi kujua ukweli na kutatua tatizo.
9. Kwenye tatizo lolote ambalo unapitia, kila mtu anayehusika amechangia tatizo hilo. Hata kama unaona wewe ndiye uliyeonewa, hata kama unaona wewe ndiye mnyonge, bado umechangia kwenye tatizo lolote unalopitia. Kwa kuanzia kwa mtazamo huo kutakusaidia usijikute kwenye tatizo kama hilo wakati mwingine.
kwa mfano tuseme ulikuwa unapita barabarani usiku na wezi wakakukaba na kukuibia. Unaweza kupeleka lawama zote kwa wezi wale au kwa hali mbaya ya ulinzi kwenye eneo hilo. Lakini kumbuka ya kwamba na wewe una mchango, kama usingetembea mwenyewe usiku huo usingeibiwa, kama usingetembea na vitu vya thamani usingepata hasara. Kwa kuanza kufikiria hivi wakati mwingine utakuwa makini zaidi.
10. Unapotawaliwa na hisia ni vigumu sana kufanya mazungumzo magumu na kufikia muafaka. Hii ni kwa sababu hisia zinapunguza uwezo wa kufikiri vyema. Hivyo ni bora kuhakikisha wakati unafanya mazungumzo hisia zako umeshazifanyia kazi. Na hapa siyo kwamba uzifiche, bali uziachie na kuhakikisha unapofanya mazungumzo hisia zako hazikutawali.
11. Kubishana ni njia mbovu sana ya kufanya mazungumzo magumu. Mabishano yanazuia kabisa mabadiliko. Kumwambia mtu mwingine anahitaji kubadilika ndiyo unamfanya akatae kabisa kubadilika. Badala ya kubishana tafuta njia ya kuelewana, tafuta njia ambapo wote mnaanzia pamoja na kwa njia hii mtaelewana vizuri na kuweza kuchukua hatua.
12. Ni muhimu uelewe kwenye mazungumzo kwamba kila mmoja anaweza kuwa na mtazamo tofauti. Na mara nyingi mitazamo yenu inakuwa tofauti kwa sababu kuu mbili;
Sababu ya kwanza ni kwamba tumepitia maisha kwa njia tofauti, huenda tumekuwa na makuzi tofauti au tuna uzoefu tofauti. Na sababu ya pili ni kuwa na taarifa tofauti.
13. Kila mmoja wetu ana hadithi yake kuhusu dunia, kuhusu kitu gani ni sahihi kufanya na kipi siyo sahihi kufanya. Tuna hadithi tofauti kuhusu ni tabia ipi ya kawaida na ipi siyo ya kawaida. Na hizi zinatofautiana kulingana na malezi na taratibu tulizokua nazo. Haya ni muhimu sana kuzingatia kwenye mazungumzo yetu ili kuweza kufikia muafaka mzuri. Na ili kujua hadithi ya mwingine, usiwe mtu wa kuhukumu, badala yake penda kujifunza zaidi kwa kuuliza maswali zaidi.
14. Kitu muhimu sana unachotakiwa kukumbuka ni kwamba dunia ni TATA. Mambo siyo rahisi kama yanavyoonekana au kama unavyotarajia. Unaweza kuumia, kukasirika na pia kukosea, na mwenzako pia anaweza kuumia, kukasirika na kukosea. Kila mtu anaweza kuwa na hadithi yake na hadithi zote zikawa sawa kwa chochote kilichotokea.
15. Kusudio la mtu kufanya kitu linaweza kutuumiza zaidi kuliko kitu chenyewe ambacho mtu amefanya. Kama tukijua mtu alifanya kitu kibaya ila hakukusudia haituumi sana kama tutajua mtu alifanya kitu kibaya kwa kukusudia. Hivyo unapojikuta kwenye mazungumzo magumu, hebu acha kuangalia kwamba mwenzako alikusudia ili uweze kuona ukweli uko wapi.
16. Ni tabia ya binadamu kupenda kujipendelea. Pale wewe unapofanya kosa, ni rahisi kujipa sababu nzuri kwa nini umefanya kosa hilo, labda ulikuwa umechoka au ulipitiwa au hukuwa na taarifa za kutosha. Lakini inapotokea mtu mwingine ametufanyia kosa, moja kwa moja tunakwenda kwenye fikra kwamba ni wazembe, hawakuweka juhudi za kutosha, walidhamiria kutuumiza na mengine kama hayo. Kwa fikra hizi ni vigumu kufikia muafaka katika mazungumzo.
17. Kuna njia nne kuu ambazo unaweza kuwa umetumia kuchangia tatizo fulani kutokea, hata kama unaona hujachangia moja kwa moja.
Njia ya kwanza ni kuepuka kuchukua hatua mapema. Tangu mwanzo umeona mambo hayapo vizuri ila unaacha kuchukua hatua na baadaye tatizo linakuwa kubwa.
Njia ya pili ni kuwa mgumu kufikika, hasa pale wewe unapokuwa mtu wa kufanya maamuzi. Kama watu wanaogopa kukupa taarifa kunachangia kuleta matatizo.
Njia ya tatu tofauti mbili kukutana. Hapa ni pale wewe na yule ambaye una matatizo naye tofauti zenu zinakuwa zimekutana na ndiyo zinazua tatizo.
Njia ya nne ni dhana ambayo unakuwa nayo kwenye tatizo husika. Kama dhana yako ni kwamba mwingine ndiye amekosea na wewe umeonewa tu, tatizo linakuwa kubwa zaidi.
18. Kama huoni mchango wako kwenye tatizo lolote ambalo upo kuna njia mbili unaweza kuzitumia na zikakusaidia kujua mchango wako;
Njia ya kwanza ni kubadilisha nafasi yako na mwenzako. Hapa unajaribu kuvaa viatu vya mwenzako, na kuliangalia tatizo kwa upande wa mwenzako, je wewe ungekuwa yeye na yeye angekuwa wewe, ungelionaje tatizo hilo.
Njia ya pili ni kujifanya kama mtu wa pembeni, kama msuluhishi ambaye amekuja kutatua tatizo lenu. Na hapo unajisikiliza wewe mwenyewe na kumsikiliza mwenzako, kisha unafanya maamuzi kama mtu wa pembeni, na hapa unaondoa hisia zako zote.
Kwa njia hizi mbili utaona mchango wako kwenye tatizo lolote ulilopo.
19. Usijaribu kuzifisha hisia zako pale unapojikuta kwenye tatizo. Kama umekasirishwa basi kasirika, kama unataka kulia basi lia, lakini usiruhusu hisia hizo zikupelekee kufanya jambo ambalo litaongeza tatizo zaidi. Jipe muda wa kuruhusu hisia zako zitulie kabla hujafanyia kazi tatizo lililopo. Pia usijione mbaya pale hisia mbaya zinapokujia, hisia ni hisia, zisikilize.
20. Kuna vitu vitatu muhimu sana unavyotakiwa kuvikubali kuhusu wewe kama unataka kuweza kufanikisha mazungumzo magumu na kutatua matatizo yanayokukabili.
Kitu cha kwanza ni kukubali kwamba unaweza kufanya makosa na kuyakubali makosa yako.
Kitu cha pili ni kukubali kwamba unaweza kuwa na makusudi tofauti kwenye mambo unayofanya na hivyo watu kushindwa kuelewa kusudi lako hasa ni nini.
Kitu cha tatu kukubali ni kwamba tatizo lolote unalokuwa nalo kwenye maisha yako, na wewe una mchango wako. Kuna namna ambavyo umechangia kwenye tatizo hili.
Kwa kukubali mambo hayo matatu utaweza kutatua tatizo lolote linalokukabili.
Haya ndiyo mambo 20 muhimu kati ya mengi niliyojifunza kupitia kitabu hiki.
Naamini kuna mazuri uliyojifunza hapa, kikubwa ni wewe kuyafanyia kazi ili uweze kuboresha mahusiano yako na wale wanaokuzunguka. Kwa sababu sisi kama binadamu tunapitia changamoto nyingi, kuweza kuzitatua ndiyo kunayafanya maisha yetu kuwa bora sana.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,