Kila kitu unachochagua kufanya kwenye maisha yako kina gharama. Kila hali unayochagua kwenye maisha yako ina gharama. Hii ni sheria ya asili, hivyo ni wewe kuchagua ni gharama gani uliyo tayari kuilipa.
Katika maisha tunaweza kuwagawa watu kwenye makundi mawili, na makundi haya yanaendana kisifa na aina mbili za wanyama.
Kundi la kwanza ni kondoo, kama wote tunavyojua kondoo huwa wanafanya kile ambacho kondoo wengine wanafanya, hawahoji wala kutaka kuboresha. Na kila watakachoambiwa kufanya, basi wao wanafanya. Kwenye sifa za watu hawa ni wale ambao wapo tu kufuata mkumbo, hakuna chochote kikubwa wanafanya, wanasubiri waone wengine wanafanya nini na wao wafanye. Na mara nyingi ni waajiriwa, tena wa kawaida sana.
Kundi la pili ni mbwa mwitu, hawa huwa wapo kivyao, wanafanya kile ambacho ni muhimu kwao na wanakomaa mpaka wapate kile ambacho wanakitaka. Kwa tabia za binadamu hawa ni wale wapambanaji, wale ambao wanajitoa zaidi kupata kile wanachotaka. Ni wabunifu na wanajitoa kweli, ni wajasiriamali na kama wameajiriwa basi kazi zao ni tofauti kabisa na wafanyakazi wengine.
Sasa kuna gharama, kwenye kila upande.
Gharama ya kuwa kondoo ni kuchoka, kwa sababu unafanya yale yale ambayo kila siku unafanya. Unachoshwa na kundi zima unaloongozana nalo na hakuna kikubwa unachoweza kufikia.
Gharama ya kuwa mbwa mwitu ni upweke, kwa sababu utakapochagua kufanya kile ambacho ni muhimu kwako, itakubidi uliache kundi na kwa kuwa unafanya tofauti wengi hawatakuelewa, utakuwa mpweke, hasa pale unapoanza.
Chagua kama unataka kuwa kondoo na uishi maisha ya uchovu ambayo hayana jipya, au unataka kuwa mbwa mwitu na uishi maisha ya upweke lakini yenye mafanikio makubwa baadaye.
SOMA; Njia 30 Za Kufikia Mafanikio Makubwa Sana(World Class)
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kila kitu ninachochagua kufanya kwenye maisha kina gharama. Na kwenye maisha kuna makundi ya aina mbili, kondoo na mbwa mwitu. Kondoo wanachoshwa na kufanya mambo yale yale, wakati mbwa mwitu wanakuwa na upweke kwa kufanya mambo mapya. Mimi nachagua kuwa mbwa mwitu na hivyo nitafanya mambo mapya na makubwa, ili niweze kufikia mafanikio makubwa.
NENO LA LEO.
“either you get eaten by a wolf today or else the shepherd saves you from the wolf so he can sell you to the butcher tomorrow”
― Ogden Nash
Gharama ya kuwa kondoo ni kubwa, ni labda uliwe na mbwa mwitu leo, au mchungaji akuokoe usiliwe na mbwa mwitu ili kesho akuuze kwa mchinjaji.
Usikubali kuwa kondoo, kuwa mbwa mwitu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.