Biashara inahitaji akili sana, biashara inahitaji kujua jinsi ya kwenda na akili na hisia za wengine. Na mambo mengi kwenye biashara hutafundishwa darasani wala kwenye mafunzo mengine ya kibiashara, bali utayaona mwenyewe kama utakuwa makini na biashara yako.
Kwa mfano inapotokea wateja wanafanya makosa, na ikawa kweli ni makosa ya wateja, huhitaji kushinda kila mara. Hii inajenga picha fulani kwa wateja kwamba kwenye jambo lolote linalohusu mvutano kati yako na wateja wako wewe utaishia kushinda.
Mfano mwingine kama kuna majadiliano ya kibiashara au kuna deal ambayo mnaigombania baina ya wafanyabiashara, kama kila mara unapata wewe, au wewe ndiyo unapata sehemu bora, wenzako litawaingia kwenye akili. Na watakuwa wanajaribu kuzificha deal nzuri usizijue maana tayari wewe umeshakuwa na sifa ya kushinda kila kitu.
Ni lazima ujue wakati gani wa kushinda na wakati gani wa kuwaacha wengine nao washinde. Na lengo lisiwe wewe kushindwa tu, bali lengo liwe kila mtu anashinda.
Kwa vyovyote vile tengeneza mazingira ambayo kila mtu anajiona ni mshindi, utajitengenezea sifa nzuri na kila mtu atataka kufanya biashara na wewe. Au kama kuna deal nzuri, watu watakutafuta wewe kwa sababu wanajua kila anayehusika anashinda.
Jifunze kwenda vizuri na watu, iwe ni wateja wako au wafanyabiashara wenzako, itakujenga uaminifu mkubwa ambao utanufaisha biashara yako.
ANGALIZO; Ninaposema deal simaanishi yale madili yanayozungumzwa mitaani, namaanisha fursa nzuri ya kibiashara.
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz