Kutokuyaelewa vizuri maisha ni moja ya changamoto kubwa za kufikia mafanikio. Ni sawa na kukata tiketi ya ndege halafu unakwenda kusubiri kituo cha mabasi. Ni zoezi ambalo haliwezi kuzaa matunda unayotarajia.
Kuna mambo mengi kwenye maisha ambayo tunayafanya kwa njia hiyo. Kuna kitu tunakitaka lakini hatutumii njia sahihi kukipata.
Kwa mfano kuna vitu ambavyo tunasubiri tupewe kwenye maisha, wakati kwa uhalisia vitu hivyo hakuna anayeweza kutupa, bali tunatakiwa kuvichukua sisi wenyewe.
Moja ya vitu hivyo ni uhuru, nisikie na niseme kwa herufi kubwa, HAKUNA MTU ANAYEWEZA KUKUPA UHURU, unachukua uhuru wako mwenyewe. Kwenye jambo lolote kwenye maisha yako, wewe ndiyo unachukua uhuru wako, wewe ndiye unayedai uhuru wako, na siyo mtu mwingine anakuletea kwenye mikono yako.
Sasa wengi wamekuwa wakisubiri wapewe uhuru ndio waweze kufanya kile ambacho wanajua ni muhimu kwenye maisha yao. Swali ni je nani unafikiri atakupa uhuru? Kama unasubiri jamii ikupe uhuru ni sawa na unapoteza muda wako, jamii itakuhukumu kwa kila unachofanya, iwe ni kizuri au kibaya. Uhuru unaanza na wewe na unaanzia kwenye akili yako, kwenye mawazo yako, unaamua kuwa huru, huruhusu matarajio ya wengine kukufunga wewe kwa vyovyote vile.
Kwa sababu kitu kikubwa kinachotunyima uhuru ni matarajio ya wengine, tunapotaka kwenda kama jamii inavyotaka kwenda, tunakuwa tumeuza uhuru wetu, na hakuna anayeweza kuturudishia kama hatutaamua kuuchukua tena sisi wenyewe.
Kitu kingine ambacho hupewi bali unachukua mwenyewe ni majukumu. Hakuna anayeweza kukupa wewe majukumu, hasa yale ambayo yatakufanya wewe kuwa bora, kufikia yale maisha ya ndoto yako. wengi watakupa majukumu yale yanayowasaidia wao kwenye ndoto zao. Ila kufikia ndoto zako, kufikia mafanikio makubwa, unajipa majukumu mwenyewe, unachukua majukumu, hata kama wengine hawaelewi au hawachukui hatua.
Jua njia sahihi ya kupata kile unachotaka, ili usiendelee kupoteza muda kwenye njia zisizofaa.
SOMA; SIRI YA 12 YA MAFANIKO; Shika Hatamu Ya Maisha Yako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kunipa uhuru ila ninaweza kuuchukua uhuru wangu mimi mwenyewe. Pia hakuna mtu anayeweza kunipa majukumu yatakayonifikisha kwenye mafanikio makubwa kwenye maisha yangu, nahitaji kuchukua majukumu peke yangu. Ninachukua nafasi ya kuchukua uhuru wangu na majukumu yangu mwenyewe, sisubiri wengine wanipe maana nitakuwa napoteza muda wangu.
NENO LA LEO.
Hakuna mtu yeyote anayeweza kukupa wewe uhuru wako, unachukua uhuru wako mwenyewe, unadai uhuru wako wewe mwenyewe.
Hakuna mtu anayeweza kukupa wewe majukumu yatakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa kwenye maisha yako. unajipa majukumu yako mwenyewe. Wengine watakupa majukumu ya kuwanufaisha wao siyo wewe.
Shika hatamu ya maisha yako, hakuna wa kukutoa hapo ulipo, ni lazima uanze mwenyewe.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.