Kama umekuwa mfuatiliaji wa makala hizi kwa muda mrefu, lengo kubwa unalotakiwa kuwa nalo ni kuweza kujenga na kukuza biashara yako, iweze kujiendesha kwa faida na ikuwezeshe wewe kufikia mafanikio unayotarajia. Hili ndiyo inabidi liwe lengo lako kuu, na unahitaji kulifanyia kazi kila siku. Lakini pia hiki ni moja ya vitu vigumu sana kufanya hasa kwenye zama hizi ambapo karibu kila mtu anaingia kwenye biashara na ushindani umekuwa mkali.
Pamoja na sababu za nje ambazo zinaleta changamoto kwenye biashara, sababu kubwa zinazopelekea biashara kufa huwa zinaanzia ndani ya biashara yenyewe. Yaani hata kama uchumi ni mgumu kiasi gani, hata kama ushindani ni mkali kiasi gani, kufa kwa biashara kunaanzia ndani ya biashara na siyo nje. Na mtu anayetengeneza mazingira ya biashara kufa ni mfanyabiashara mwenyewe, yaani mmiliki wa biashara.
Kuna hatari nyingi ambazo huwa zinapelekea biashara kufa, lakini kuna moja ambayo ni kubwa sana na huwa inatengenezwa na mmiliki mwenyewe wa biashara. Leo kupitia makala hii tutakwenda kuiangalia hatari hii kwa undani na jinsi unavyoweza kuepuka kuitengeneza kwenye biashara yako.
Hatari kubwa sana ambayo mmiliki wa biashara anaweza kuitengeneza kwenye biashara yake ni kuwa na mtu mmoja au kitu kimoja ambacho biashara nzima inakitegemea. Kama kuna mtu mmoja ambaye akikosekana basi biashara inayumba, basi biashara yako ipo hatarini, hata kama mtu huyo ni wewe mmiliki wa biashara. Na pia kama kuna hali fulani ambapo biashara inategemea sana, kwa mfano biashara ina mteja mmoja mkubwa, ambapo hali hiyo ikibadilika basi biashara inayumba, biashara hiyo ipo hatarini.
Ili biashara iweze kukua na kujiendesha kwa faida, ni lazima iweze kujitegemea yenyewe. Asiwepo mtu mmoja au hali moja ambapo biashara inategemea sana ili iweze kwenda vizuri. Kama biashara inakutegemea wewe mmiliki, yaani wewe ndiyo kila kitu kwenye biashara yako, siku ukipata shida, na siku hiyo haikosekani, biashara yako itaathirika kwa kiasi kikubwa sana. Kama kuna mfanyakazi ambaye ndiyo anaisimamisha biashara na kuweza kwenda, asipokuwepo kunakuwa na pengo kubwa kwenye biashara yako, biashara hiyo ipo kwenye hatari kubwa.
Kitu kimoja ambacho wote tuna uhakika nacho ni kwamba mambo hayataendelea kuwa kama yalivyo sasa. Mabadiliko yanatokea kila siku, na hivyo biashara yako itakutana na mabadiliko mengi. Hivyo lengo lako ni kuiimarisha biashara yako ili katika mabadiliko ambayo lazima ipitie, itaweza kuendelea kuwa imara. Hata kama itayumba, lakini isifikie kufa kabisa.
Je unawezaje kuiokoa biashara yako na hatari hii ya utegemezi?
Kwanza kabisa tengeneza mfumo wa uendeshaji wa biashara yako. Biashara haitakiwi kumtegemea mtu mmoja, bali biashara inahitaji kutegemea mfumo bora. Unapokuwa na mfumo mzuri wa uendeshaji wa biashara yako, biashara hiyo itakwenda vizuri. Katika mfumo wako unajua kabisa ni maeneo yapi muhimu ya biashara yako, na majukumu ya kila mtu atakayefanya kazi kwenye eneo fulani la biashara. Ni lazima kupitia mfumo wako wa biashara majukumu ya kila mtu anayekusaidia kwenye biashara yako yawe wazi, mtu asifanye maamuzi tu kama anavyojisikia yeye, bali afanye maamuzi kulingana na misingi ambayo umeijenga kwenye biashara yako. kwa kuwa na mfumo wa aina hii, ikitokea mhusika wa eneo fulani amepata changamoto, basi ni rahisi kutafuta mtu mwingine wa kutimiza majukumu yale. Na kama ukimpata aliye bora, basi wateja wako wataendelea kupata huduma bora sana.
Kitu kingine muhimu sana kuzingatia ni kuhakikisha unakuwa na wateja wengi kwenye biashara yako. hata kama biashara yako ni kuziuzia biashara nyingine na umepata mteja mmoja ambaye ananunua kwa kiasi kikubwa, usiridhike na kujisahau. Hakikisha unatafuta na kuwa na wateja wengi kiasi kwamba kama mteja mmoja akiamua kuacha kununua kwako basi biashara yako haitaathirika kwa kiasi kikubwa. Hata kama una mkataba na mteja kiasi kwamba una uhakika akiacha kununua utamshitaki, ikitokea ameacha kununua, hata kama utamshitaki kwa kuvunja mkataba, bado biashara yako inakuwa imeathirika. Licha ya kuwa na uaminifu baina yako na wateja wako, ili kuwa upande salama, hakikisha una wateja wengi ambao wataiwezesha biashara kwenda vizuri.
Wewe kama mmiliki wa biashara unaweza kuizuia biashara yako kuingia kwenye hatari ya kufa kutokana na mabadiliko yanayoweza kujitokeza. Na hili ni kwa wote, iwe una biashara ndogo au kubwa. Anza sasa kutengeneza mfumo mzuri kama huna na ongeza wateja kama bado unategemea wateja wachache. Kila la kheri.