Moja ya sababu kubwa kwa nini biashara nyingi huwa zinadumaa ni kukosekana kwa uwekezaji endelevu.
Mtu anaanza biashara na miaka inapita lakini biashara inabaki pale pale, haikui wala kutanuka.
Hii inasababishwa na mfanyabiashara kutumia faida yote anayoipata kutoka kwenye biashara yake.
Kama na wewe unaendesha biashara yako kwa mtindo huu unaidumaza na miaka mingi ijayo utajikuta uko hapo ulipo sasa.
Ni lazima ujijengee utaratibu wa kurudisha sehemu ya faida kuwekeza kwenye biashara yako. Ni kutokana na faida hiyo ndiyo unaweza kuikuza biashara na kuitanua kwenye maeneo mengine.
Hata kama unaitegemea biashara hiyo kuendesha maisha yako, bado siyo sababu ya kutumia faida yote. Badala yake kazana kukuza faida, ili sehemu ya faida irudi kukuza biashara na sehemu ya faida ndiyo uitumie wewe kuendesha maisha.
Na unapowekeza sehemu ya faida kwenye biashara ni muhimu ufanye kitu cha tofauti, kitu ambacho kitaonesha kwamba biashara imekua.
Na ili uweze kujua ni sehemu ipi ya faida imerudi kwenye biashara yako, ni lazima uwe na usimamizi mzuri wa fedha kwenye biashara yako. Kitu ambacho kitakuwezesha kuidhibiti vizuri biashara unayofanya.
Ni muhimu leo ujiulize swali hili, ni sehemu gani ya faida umekuwa unaiwekeza kwenye biashara? Kama umekuwa hufanyi hivi chukua hatua.