Katika kila unachofanya kwenye maisha yako, utakutana na watu ambao ni wasumbufu, watu ambao wanaudhi sana. Mnakubaliana mfanye kitu fulani lakini wao hawatimizi wajibu wao. Au wanafanya mambo ambayo yanapelekea wewe kukasirika na kuudhika sana. Au mtu anaamua kukukosoa na kukutukana kwa jambo ambalo hana hata uhakika nalo.
Hizi ni hali ambazo zinawapelekea wengi kupata hasira na hata kukosa furaha. Na wengine hufikia hatua ya kufanya mambo ambayo yanawaingiza kwenye matatizo zaidi baadaye.
Leo nataka tushirikishane mbinu bora ya kukabiliana na watu hawa, ili uhakikishe hakuna anayekuharibia utulivu wako na furaha yako. Na mbinu hii ni kukataa kuwa kama watu hao.
Kama mtu anafanya kitu cha kukuudhi, na wewe ukakasirika unafikiri ni nini kimetokea? Kilichotokea ni kwamba mtu huyu amefanikiwa kukufanya uwe kama yeye.
Kama mtu amekutukana na wewe ukamtukana, unafikiri ni nini kimetokea? Kilichotokea ni kwamba mtu huyo ameweza kukuvuta na ukafika upande wake.
Lengo lako ni kuepuka kuwa kama watu hawa, ambao ni wasumbufu na wanaudhi. Na njia bora ya kufanya hivi ni kuhakikisha unakuwa imara na hutetereshwi na maneno au matendo ya wengine.
Unakuwa imara kwa kutegemea wengine kutokuwa kama unavyotaka wawe, jua kila mtu ana nafasi yake ya kufanya makosa, kuna wengine ni wasumbufu na wanaoudhi. Na pia katika mambo mengine ambayo mtu anafanya, usiyape uzito sana. Kama mtu amekutukana, kinachokuumiza wewe siyo tusi alilokupa, bali tafsiri yako kwenye tusi hilo ndiyo inakuumiza.
Kwa mfano mtu akikutukana halafu hukusikia amesema tusi gani, itakuumiza? Jibu ni hapana, hivyo kinachokuumiza siyo neno linalotolewa, bali tafsiri yake. Badala ya kuumizwa na tafsiri, usilipe uzito kabisa. Na kama tukio lililotokea linapaswa kuadhibiwa, basi fuata utaratibu mzuri wa kumwadhibu aliyefanya. Na hufanyi hivi kwa sababu wewe umeumia, bali unafanya hivyo kuhakikisha kitu kama hiko hakitokei tena wakati mwingine.
Wewe ndiye mwamuzi wa mwisho kwenye maisha yako, usikubali maneno au matendo ya wengine yavuruge utulivu wako na furaha yako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba njia rahisi ya kuepuka watu wasumbufu na wenye maudhi ni kukataa kuwa kama wao. Sitakubali kuvurugwa au kukasirishwa na kitu chochote mtu atasema au kufanya, badala yake nitachukulia kama sehemu ya matatizo yao ambayo sikubali kuyanunua. Nitachukua hatua ya kutoa adhabu pale inapohitajika kufanya hivyo, lakini sitaruhusu kuvurugwa kwa utulivu na furaha yangu kwa mambo yanayofanywa na wengine.
NENO LA LEO.
Kwenye maisha kuna watu ambao ni wasumbufu na wenye maudhi. Njia bora ya kukabiliana na watu hawa ni kuepuka kuwa kama wao. Usikubali maneno au matendo ya mtu mwingine yavuruge utulivu wako na furaha yako. Badala yake wachukulie kama watu wenye matatizo yao na usitake kuyanunua.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.