Kufikia ndoto yoyote kubwa kwenye maisha siyo jambo dogo hata kidogo. Njia ni ndefu yenye mabonde na milima mingi.
Kitu pekee kitakachokuwezesha kuifikia ndoto yoyote kubwa ni ndoto hiyo ikuingie na kukumiliki kabisa. Yaani chochote unachofikiria kwenye maisha yako kiwe kinaongozwa na ndoto hiyo. Fursa yoyote unayoipata kwenye maisha uitumie kutekeleza ndoto hiyo.
Uwe tayari kuiendea ndoto hiyo hata kama kila mtu anasema haiwezekani. Uwe tayari kuiendea ndoto hiyo hata kama kila mtu ameshakata tamaa.
Ifike mahali kila mtu aone kama umechanganyikiwa kwa jinsi ulivyong’ang’ania kuifikia ndoto yako. hapo ndiyo ndoto inakuwa imekuingia kweli na kukumiliki hasa.
Na siyo inakumiliki kwamba inakutumikisha, bali inakumiliki kwamba hiko ndiyo kitu ambacho umechagua kufanya, na hakuna namna yoyote utarudi nyuma.
Uzuri wa dunia ni kwamba huwa inabana, kwa wale wanaojaribu tu, ila kwa wale waliojitoa kweli dunia inachoka kubana na hatimaye inaachia. Hivyo unapokuwa umechagua ndoto ambayo hukubali kurudi nyuma hakuna namna utaweza kushindwa.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoua Ndoto Zako Kubwa Za Mafanikio.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba njia ya uhakika ya kufikia ndoto yangu kubwa kwenye maisha ni kuruhusu ndoto hii iniingie na kunimiliki. Maisha yangu yote niyajenge kutokana na ndoto hii na nisisikilize chochote cha kunirudisha nyuma. Nina hakika nitaweza kufikia ndoto yangu kwa njia hii.
NENO LA LEO.
Kufikia ndoto yako kubwa kwenye maisha unahitaji kuruhusu ndoto hiyo ikuingie na kukumiliki. Maisha yako yote uyajenge kwa msingi wa ndoto hiyo. Usikubali kurudi nyuma kwa njia yoyote ile, bali kuendelea kupambana hata kama wengine wataona umechanganyikiwa.
Dunia itabana lakini mwishowe itakuachilia na utafikia ndoto yako. ibebe ndoto yako popote ulipo, ifanye kuwa maisha yako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.