Karibu tena rafiki yangu kwenye maongezi haya kati yangu mimi na wewe. Haya ni maongezi ambayo tunagusia maeneo mbalimbali ya maisha ambapo tunaweza kujifunza na kuwa bora zaidi.
Asili yetu binadamu ni kuendelea, yaani kutokubaki pale ulipo sasa. Unahitaji kuwa bora zaidi leo kuliko ulivyokuwa jana. Ndiyo maana watu wengi wanaofanya kazi ambazo haziwapi nafasi ya kuendelea au kukua wao binafsi huwa wanakuwa na maisha yasiyo ya furaha. Hivyo ni jukumu letu kila siku kuwa bora zaidi na ubora huu unaanza na kupata maarifa sahihi. Karibuni sana tushirikishane maarifa haya.
Leo katika maongezi yetu nataka tujadili jambo moja muhimu sana ambalo tunahitaji kufanya, kwa ajili yetu wenyewe, japo tutalifanya kwa kuwafikiria wengine, lakini faida kubwa ni kwetu sisi wenyewe. Kabla hatujajadili jambo hili kwa kina nikushirikishe mfano wangu binafsi.
Nilipokuwa mdogo, katika kula, kama nimeweka chakula mwenyewe au nimewekewa chakula na nikashindwa kukimaliza, basi nilikuwa namwaga. Sasa mama yangu alikuwa ananisema sana kwenye hilo, na akawa ananiambia unajua kuna watu wengine wanatafuta chakula hiko unachokimwaga wewe lakini hawakipati? Sasa mimi huwa napenda kuhoji tangu zamani, nikawa namuuliza mama, sasa kwa mfano hata nisipomwaga chakula hiki, bado hao ambao wanakosa chakula kama hiki wanaendelea kukosa.
Hoja yangu ilikuwa ni kwamba hata kama sitamwaga chakula, bado wale ambao wamekikosa siwezi kuwasaidia moja kwa moja. Yaani kama kuna mtu yupo Iringa analala njaa, na mimi nipo Dar nimemwaga chakula, hata nisipokimwaga si bado yule aliyeko Iringa atalala njaa tu?
Na hii ni hoja nzuri unayoweza kuisimamia kwenye maeneo mengi ya maisha yako.
Lakini kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda, ndiyo nilikuja kuelewa maana nzima ya mama kwa nini usimwage chakula huku wengine, hata kama wapo mbali wanakosa chakula hiko.
Huachi kumwaga chakula kwa sababu usipomwaga utawasaidia wale ambao wamekikosa, bali ni kwa sababu zako wewe binafsi. Humwagi chakula kwa sababu unakithamini na unapojua ya kwamba siyo kila mtu amepata nafasi ya kupata chakula, basi hii inakufanya ukithamini zaidi na uwe mtu wa shukrani. Unakuwa na mtazamo tofauti juu ya maisha na juu yako wewe binafsi, ya kwamba japo leo umepata chakula, kuna uwezekano siku nyingine ukakikosa, na hivyo ni vyema ukakifurahia kwa wakati huu ambao unakipata.
Kitu kingine muhimu cha kuchukua hapa ni kwamba binadamu tuna tabia ya kuzoea, hata mtu ambaye alikuwa hapati kitu fulani, na hivyo kukithamini sana, akishakuwa anakipata kila mara anakizoea. Kwa mfano labda mtu ametoka kwenye kijiji ambapo kula mkate siyo jambo la kawaida, na kufika mjini ambapo kila siku anakula mkate, mwanzoni atakuwa anafurahia sana kula mkate, na atakula mkate wowote. Lakini kadiri anavyozoea, anaanza kuona mkate ni kitu cha kawaida, na utaanza kuona anasema siwezi kula mtake wa aina fulani, au siwezi kula mkate ambao hauna siagi. Ni mtu huyu huyu ambaye awali alikuwa akiona mkate kama kitu cha kipekee sana.
Hivyo kutumia dhana hii ya mama kwamba wakati wewe unamwaga kuna mwingine anakikosa, inakufanya uache kutumia mazoea, na unapoweza kuyashinda mazoea ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kufurahia maisha yako.
Unaweza kutumia wapi dhana hii?
Kwenye kazi; tumekuwa tunaona watu wengi wakiomba kazi kwa unyenyekevu, wakisema nipo tayari kufanya chochote nitakachoagizwa kwenye kazi yangu, nitatekeleza majukumu yangu kwa wakati, na kukubali mshahara anaoahidiwa. Lakini miaka michache baadaye mtu anazoea kazi ile, anaanza kuifanya kwa mazoea, kushindwa kutimiza majukumu yake kwa wakati na kuanza kulalamika kwamba mshahara ni kidogo. Kwa kukaa chini na kufikiria kwamba kuna mtu mwingine ambaye anatafuta kazi kama hii na hata haipati, kutakuwezesha kuipa kazi yako uzito na hivyo kuifanya kwa ubora.
Kwenye biashara; tumekuwa tunaona watu wengi wakiingia kwenye biashara kwa hamasa kubwa, na kuwaahidi wateja huduma bora sana. Wateja wanawaamini na kuanza kufanya biashara na wao, wanaanza kupata faida, wateja wanakuwa wengi, na baadaye anaanza kuona biashara yake ni kubwa sasa na kutokujali tena wateja. Yeye anaishia kuangalia ni kipi kitampa faida zaidi bila ya kujali kitapokelewaje na wateja wake. Kwa hali hii utoaji wake wa huduma kwa wateja unakuwa mbovu sana. Kwa kufikiria ya kwamba kuna wafanyabiashara wengine ambao wanatafuta hata wateja wa chache tu wa kuwa nao ila wanakosa, itawawezesha kuithamini biashara yao na kuweka ubora zaidi.
Kwenye ndoa; tumekuwa tunaona watu wawili wakipendana na kuwa wapenzi, wanaingia kwenye uchumba na kukubaliana kufunga ndoa. Na kwa uhakika zaidi wanawachangisha watu mamilioni ya fedha, ili washiriki kwenye kitendo hiko kikubwa kwao, cha kuungana na kuwa kitu kimoja. Ila maisha yanapoanza na muda unavyokwenda wanaanza kuzoeana, na kila mmoja kumwona mwenzake ni wa kawaida. Yale mapenzi moto moto ya kabla ya ndoa yanapungua na kuonekana hayana nafasi tena. Kwa kufikiria ya kwamba kuna watu wengine wanatafuta nafasi ya kuwa kwenye ndoa kama ambayo mtu yupo lakini hawaipati nafasi hiyo, itakupa hamasa ya kuithamini ndoa na kuweka juhudi zako binafsi kwenye kuiboresha.
Kuna maeneo mengi sana ambayo tunaweza kutumia hali hii, iwe kwenye elimu, uongozi na kila eneo la maisha yetu.
Fikiria ya kwamba nafasi uliyoipata wewe, kuna wengine wanaitafuta ila wameikosa, na hufanyi hivi ili kujiona wewe una bahati sana, bali unafanya hivi ili kuthamini zaidi kile ambacho umekipata.
Fanyia kazi hili kila siku rafiki yangu, ni kitu kidogo lakini kitabadilisha kabisa tazamo wako juu ya maisha yako na kile ambacho unakifanya.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz