Tunaishi kwenye ulimwengu ambao mstari kati ya kazi, maisha ya kawaida na muda wa kupumzika umefutika kabisa. Yaani kwa sasa ni vigumu kutenge upi muda wa kazi, upi muda wa maisha na upi muda wa kupumzika. Na kadiri teknolojia inavyoboreshwa, ndivyo mstari huu unazidi kufutika kabisa.
Kwa mfano muda wa kazi mtu anaweza kupumzika ndani yake, kwa kufanya vitu ambavyo havihusiani na kazi yake, na muda w akupumzika mtu anaweza kujikuta ameingia kwenye kazi. Wengi wa wanaofanya hivi wamekuwa wakifikiri ya kwamba wanaongeza ufanisi lakini ukweli ni kwamba wanapunguza ufanisi na kukosa vyote viwili. Yaani hawafanyi vizuri kwenye kazi na pia hawafurahii muda wao wa kupumzika na hata maisha mengine ya kawaida.
Na kitu kimoja kilicholeta mvurugano mkubwa kati ya mlinganyo huu wa kazi, maisha na kupumzika ni hisi simu janja (smartphone), kitu kimoja ambacho tumekuwa tunakishuhudia ni kwamba simu hizi zina ujanja kuliko hata wale wanaozimiliki. Na hivyo kuchukua sehemu kubwa ya maisha na kazi pia. Ile kwamba upo kati kati ya kazi nzito, halafu unaingia ujumbe ambao unaona huwezi kuacha kuusoma, unausoma na kukuta hata haukuwa muhimu, unakuwa umeacha kufanya unachofanya na kuja kurudi tena inakuchukua muda.
Au upo kwenye mapumziko yako na unapokea barua pepe kupitia simu yako hiyo janja ambayo inahusiana na kazi na hivyo kujikuta unafanya kazi hata kwa ule muda ambao umepumzika. Imekuwa ni kelele kubwa sana kwa nyakati hizi na muda unazidi kuonekana hautoshi. Kadiri tunavyokuwa na vitu vingi vya kufanya, ndivyo ambavyo muda wetu umekuwa hautoshi na hivyo tunalazimika kuiba muda, na sehemu tunazoiba muda huu ni kwenye maisha yetu ya kawaida na kwenye muda wetu wa kupumzika.

 
Na kitu kimoja ambacho tumekuwa tunakiibia muda sana ni kulala. Kiafya mtu anatakiwa kupata angalau masaa 7 mpaka nane ya kulala kwa siku. Halafu hayo mengine yanayobaki ndiyo ayatumie kwa mambo yake mengine. Sasa kinachoshangaza ni jinsi ambavyo mtu anayatumia masaa mengine hovyo, na kuja kuiba haya ya kulala.
Unahitaji kuwa na njia bora ya kutengeneza mlinganyo wa maisha yako ili kazi, maisha na muda wa kupumzika viweze kwenda sawa.
Leo hapa tutashirikishana njia tano za kuweza kufikia mlinganyo huo bora kwako;
1. Kuwa na malengo na pangilia siku yako.
Bila ya malengo maisha yatakuwa kama mbio za panya, unapita njia ile ile, kufanya kile kile na kupata kile ambacho umezoea kupata. Njia ya kwanza kabisa ya kuhakikisha unakuwa na mlinganyo bora kwenye maisha yako ni kuwa na malengo. Na hapa huweki malengo ya fedha au kazi pekee, bali unaweka malengo katika maeneo haya matano muhimu sana kwenye maisha yako; malengo binafsi, fedha, kazi/biashara, mahusiano na afya. Haya ni maeneo matano muhimu yanayojenga maisha yako. Ni muhimu kila eneo uliwekee malengo.
Kila siku ianze siku yako kwenye karatasi, hii ina maana kwamba kabla siku haijaanza, ipange na sio uipange tu kwenye kicha chako, bali uandike kabisa. Ni vitu gani unataka kufanya kwenye siku hiyo husika, orodhesha kabisa na muda wa kuvifanya. Kwenye orodha yako weka muda wa kupumzika na muda wa kukaa na wale ambao ni wa muhimu kwako.
Kujifunza zaidi kuhusu malengo na mipango soa hapa; Hili ni Jambo Moja la Lazima Kufanya Ili Ufikie Malengo Yako.
2. Jijengee nidhamu ya muda.
Kuwa na malengo na mipango pekee haitoshi wewe kuwa na mlinganyo bora kwenye siku yako. Wengi wanaandika lakini hawatekelezi, huenda na wewe umekuwa unapanga hivyo lakini mwisho wa siku unajikuta hujatekeleza. Kuna kitu kingine muhimu unahitaji kuwa nacho baada ya kuwa na malengo na mipango, na kitu hiki ni kujijengea nidhamu ya muda.
Ni lazima uwe na nidhamu ya matumizi mazuri ya muda wako. Na nidhamu ya muda maana yake unafanya kile ambacho umepanga kufanya kwa wakati ule ambao umepanga kufanya, bila ya kujali ni sababu gani zinazokuzuia usifanye. Na ili kujijengea nidhamu ya muda anza kwa kutekeleza yale uliyopanga na usikubali sababu yoyote ikuondoe kwenye lile unalofanya.
Kujifunza zaidi jinsi ya kujijengea nidhamu ya muda soma hapa; Anayetakiwa Kutafutwa Sana Kila Kona Kwa Dunia Ya Sasa Ni Nidhamu.
3. Sema HAPANA.
Kama kuna neno moja ambalo linaweza kukuletea uhuru mkubwa sana kwenye maisha yako basi ni neno HAPANA. Umekuwa unatingwa na mambo mengi kwa sababu ya kusema ndiyo. Simu inaita unasema ndiyo, hata kama upo kwenye kazi. Watu wanakutumia meseji za vichekesho unasema ndiyo nazisoma hata kama una kazi muhimu zaidi. Watu wanakutaka uwasaidie kufanya vitu ambavyo siyo muhimu kwako wala kwao na wewe unasema ndiyo.
Sasa anza kusema hapana, sema hapana kwa yale yanayokushawishi uache kutekeleza mipango yako ya siku. Sema hapana kwa kitu chochote ambacho hakina msaada mkubwa kwako au kwa wengine. Na kwa njia hii utajikuta una muda mwingi wa kufanya yale ambayo ni muhimu kwako na kuweza kutengeneza mlinganyo bora kwenye maisha yako.
Jifunze jinsi ya kusema hapana hapa; Jifunze Kusema Hapana, Itakusaidia Sana Kwenye Maisha Yako
4. Tenga muda wa kukaa na kishawishi pembeni.
Katika siku yako ni lazima utenge muda ambao utakaa mbali kabisa na kishawishi, na kishawishi ninachozungumzia hapa ni simu janja. Hata kama simu hiyo janja ndiyo sehemu kuu ya kazi yako, kuna muda unahitaji kuwa mbali nayo. Na muda huu unakuwa kwenye makundi matatu;
Kundi la kwanza ni muda wako binafsi. huu ni muda wa wewe kupumzika au kupanga au kuyatafakari maisha. Hapa huhitaji muda wowote, hivyo ni vyema kuwa mbali na simu yako. na muda mzuri wa kujitengea muda wako binafsi ni asubuhi na mapema, wakati wengine bado wamelala.
Kundi la pili ni muda wako wa kazi zile muhimu sana ambazo hazihitaji usumbufu. Haijalishi ni kazi au biashara gani unafanya, kuna sehemu ya kazi zako ambayo inahitaji utulivu wako wa hali ya juu ili uweze kuifanya kwa ufanisi mkubwa. Tenga muda huu na ni vyema pia ukauweka kuwa asubuhi pale unapoianza siku yako ya kazi.
Kundi la tatu ni kuwa na wale ambao ni wa muhimu kwako, kama familia yako. hapa unahitaji kuwa na muda wa kuwa nao, wewe kaa wewe na siyo kuwa nao kimwili huku kimawazo upo kwingine. Hivyo wakati huu unahitaji kukaa mbali na simu yako na mnakuwa pamoja, hata kama ni kwa muda mfupi inakuwa bora kuliko muda mrefu ambao mawazo yako kwenye simu au tv.
Kujua jinsi ya kuidhibiti smartphone yako soma hapa; Ndoa Inayokuzuia Wewe Kufikia Mafanikio Makubwa, Na Jinsi Ya Kuivunja.
5. Rahisisha maisha yako.
Sisi wenyewe tumekuwa tunayafanya maisha kuwa magumu. Maisha yakiwa rahisi tunatafuta njia ya kuyafanya kuwa magumu, na tumekuwa tunafanikiwa sana kwenye hilo. Ili kuweza kuwa na mlinganyo bora wa maisha yako, unahitaji kurahisisha maisha yako. Kwanza kabisa usiendeshwe na tamaa za kitu chochote kile, tamaa za kupata zaidi kitu chochote kile zinafanya maisha kuwa magumu. Kadiri unavyohitaji vitu vingi, ndivyo maisha yako yanavyozidi kuwa magumu kwa sababu kila wakati kuna kitu utaona umekosa. Jua ni vitu gani vya msingi unahitaji kwenye maisha yako na vifanyie kazi hivyo. Maisha ya furaha hayatokani na vile unavyomiliki, bali ule mchango wako unaotoa kwa wengine.
Kujua jinsi ya kurahisisha maisha yako soma hapa; Fanya Hesabu Hii Rahisi Ambayo Italeta Ukombozi Kwenye Maisha Yako.
Kuwa na mlinganyo kwenye maisha ni kitu ambacho kinazidi kuwa muhimu kadiri siku zinavyokwenda. Hii ni kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda ndivyo teknolojia mpya zinakuja na teknolojia hizi zinaingilia mipaka ya maisha yetu. Kuweza kupatikana kwenye simu masaa 24 kwa siku ni kuuza uhuru wako kwa mtu yeyote yule anayeamua kukusumbua kwa muda wowote anaotaka yeye. Ni jukumu letu kulinda muda wetu ili kuweza kufanya yale ambayo ni muhimu sana kwetu.
Nakutakia kila la kheri katika utekelezaji wa haya uliyojifunza.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz