Rafiki yangu mpendwa,

Changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kwenye maisha yetu, ndiyo zinayafanya maisha yetu yawe na maana ya kuishi. Pasingekuwepo na changamoto kabisa maisha yetu yangekuwa hovyo sana.

Hivyo furahia pale unapokutana na changamoto, kisha kaa chini na jiulize navukaje changamoto hii. Na ukishaivuka changamoto moja, jua umekaribisha changamoto nyingine.

Karibu kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto ambapo tunakwenda kuangalia hatua za kuchukua kwa wale ambao wanaona umri umeshawatupa mkono na hawana tena cha kufanya.

vitabu softcopy

Rafiki yetu Ngosha ametuandikia haya kuomba ushauri kuhusiana na umri kumtupa mkono;

“Mimi ni mwalimu, ila ndoto yangu ni kuwa kazi yangu binafsi, tatizo naona umri 33 umenitupa na majukumu ya familia.” – Ngosha J.M.

Siyo Ngosha peke yake ambaye amekwama kwenye hali hii, wapo watu wengi sana ambao wapo kwenye miaka ya 20, 30, 40 na hata 50 ambao wanaona umri umeshaenda sana na hawana cha kufanya.

Leo nakwenda kutoa ujumbe muhimu sana kwa wale wote wanaojiambia umri umeshawatupa mkono. Ni ujumbe ambao kama utausikiliza na kuufanyia kazi, miaka kumi ijayo utajishukuru sana kwa hatua ulizochukua leo.

Kabla sijakupa ujumbe huo, nikushirikishe kitu kimoja ambacho ni muhimu zaidi kwenye kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

Tafiti nyingi kuhusu mafanikio na ukuu, ambazo zimefanywa kwa wale watu walioweza kufikia ukuu kwenye maisha yao, zinaonesha kwamba mtu anahitaji miaka kumi ya kuweka juhudi kubwa ili kuweza kufikia ukuu kwenye jambo lolote lile.

Hii ni kusema kwamba, kama unayataka mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako, basi unahitaji kutenga miaka kumi ya kuweka juhudi kubwa sana, juhudi ambazo siyo za kawaida kabisa na utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Sasa jiulize je, kutoka sasa mpaka unakotaka kufika, huwezi kupata miaka 10?

Tukirudi kwa wale ambao wanasema umri umewatupa mkono, ukweli ni kwamba, hakuna mtu ambaye hawezi kupata maisha anayoyataka kwa sababu ya umri.

Niseme pia kwamba umri siyo kisingizio kabisa kwamba mtu umeshindwa kufanikiwa kwa kuwa umri umeenda.

Kama ambavyo nimekushirikisha hapo juu, unahitaji miaka kumi ya kujitoa kweli kweli ili kuweza kupata chochote unachota.

Sasa tuanze na makundi ya umri niliyopanga kuzungumza nayo leo.

Kwa kundi la wenye miaka ishirini na, yaani 21 – 30, usije ukajiambia kwamba umri umeenda, kwanza kwa wengi hapa huenda hujajua hata ni kitu gani unataka na maisha yako. Umetumia muda wako mwingi kwenye elimu, umelishwa sumu ya kila aina, hivyo unahitaji kipindi cha kutapika sumu yote uliyolishwa. Ukiwa kwenye kundi hili, unaweza kupoteza hata miaka 10, yaani miaka kumi ya kutokufanya chochote kabisa na bado ukafanikiwa.

Kula la wenye miaka thelathini na, yaani 31 – 40, hili ni kundi ambalo limeshapoteza muda wa kutosha kwa kujaribu vitu mbalimbali na hapo sasa mtu anakuwa ameanza kuchagua nini atafanya na maisha yake. Hapa napo bado mtu una muda mwingi sana, unaweza ukapoteza muda na bado ukafanikiwa sana baadaye.

SOMA; Najiwasha Moto, Njoo Unione Nikiungua (Azimio La Miaka Kumi Ijayo Ya Maisha Yangu).

Kundi la wenye miaka arobaini na, yaani 41 – 50, hili ni kundi la wengi ambao wameshavurugwa na maisha, wengi wanakuwa wameshajaribu vitu vingi na kushindwa, wakachagua kile wanachotaka lakini bado hawayaoni mafanikio. Kwenye kundi hili pia hupaswi kuwa na wasiwasi sana, lakini hapa huna tena muda wa kupoteza, unahitaji kufanya maamuzi na kuchukua hatua, na kutokuruhusu kabisa kuyumbishwa.

Kundi la wenye miaka zaidi ya 50, hapa wengine huanza kujiita wazee na kuona hawana tena cha kufanya. Ninachokuambia ni hiki, kama una miaka zaidi ya 50 na unasoma hapa, una miaka zaidi ya kumi mbele yako na unaweza kufanya makubwa sana kwenye miaka hiyo 10. Na kama utatumia vizuri uzoefu ulioukusanya mpaka hapo ulipofikia sasa, utaweza kufanya makubwa sana.

Sasa ujumbe mwingine muhimu zaidi ni huu, tunaishi kwenye dunia ambayo eneo la afya limekuwa imara sana. Umri wa watu kuishi unazidi kuongezeka, sasa hivi watu wengi wanaishi miaka zaidi ya 80 na wengi wanafika miaka 100.

Kama utaishi maisha ya adabu, yaani ukajali afya yako, na kuwa na malengo ya muda mrefu, utaweza kuishi miaka zaidi ya 80, na kama utaweka juhudi kubwa zaidi kwenye afya yako na kuwa na umakini na maisha yako, basi utaweza kuishi mpaka miaka 100.

Naomba uelewe siyo kwamba najaribu kukupa moyo hapa, bali natumia tafiti za kiafya za dunia nzima, ambazo zinaonesha umri wa kuishi unakua zaidi siku hadi siku. Na kama unaweza kusoma hapa, basi unaweza kuimarisha sana afya yako.

Na hii ni kusema kwamba, kama una miaka 20 na, una zaidi ya miaka 60 ya kuishi, ndiyo maana nakuambia unaweza hata usifanye chochote kwa miaka 10 na bado ukafanikiwa. Kadhalika kama una miaka 30, una zaidi ya miaka 50 mbele yako. Yaani kama maisha ni mchezo wa mpira, hata kipenga cha kuanza bado hakijapulizwa.

Rafiki yangu, usijidanganye na umri, popote ulipo kwenye maisha yako, unaweza kuchukua hatua sahihi kwa mafanikio yako. Muhimu ni kujua wapi hasa unapokwenda, kipi hasa unachotaka, kisha kuweka nguvu zako na muda wako wote hapo na kuachana na vingine vyote, ambavyo kwako ni usumbufu.

Jipe miaka 10 ya kuweka juhudi kubwa na utaweza kupata chochote unachotaka kupata.

Mambo mengine ambayo Ngosha aliomba ushauri, mfano kuwa na kazi yake binafsi, ni kitu cha kufanya maamuzi sasa na kuishi maamuzi hayo. Mfano kwa kazi ya ualimu ambayo Ngosha ametuambia anafanya, ana muda mwingi mno wa kufanya chochote anachotaka na maisha yake.

Nichukulie mfano, mwalimu kama Ngosha, anaweza akawa na siku mbili kwenye siku yake moja na akaweza kufanya makubwa sana. Kwa mfano, kazi ya ualimu itampasa awe kazini kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa kumi jioni, siku tano za wiki. Hii ina maana kuanzia saa 10 jioni mpaka saa 12 asubuhi siku za wiki na masaa yote 24 ya siku za mwisho wa wiki ni yake.

Sasa kama mwalimu atachagua kitu anataka kufanya, na akatenga muda kuanzia saa 10 jioni mpaka saa 4 usiku kila siku, ya kufanya kitu hicho, na kufanya muda wote kwenye siku za mwisho wa wiki, anaweza kupata masaa zaidi ya 50 kwa wiki ya kuweka kwenye kazi anayotaka kujijengea, huku akiendelea na kazi yake ya ualimu itakayomwezesha kuendesha maisha yake.

Akifanya hivyo kwa miaka kumi ijayo, atakuwa amepiga hatua kubwa mno, na kabla hata hiyo miaka 10 haijaisha, atakuwa ameshaweza kuacha ana kazi ya ualimu na kuweka nguvu zake zote kwenye kazi yake mpya aliyojitengenezea.

Maisha ni yako, uamuzi ni wako, chukua hatua sahihi kupata kila unachotaka, na tafadhali sana, usitumie umri kama kigezo kwamba huwezi kufanya chochote, una mengi sana ya kufanya na muda unao wa kutosha, chukua hatua sasa. Jipe miaka kumi ya mateso, ambayo itakuwezesha kutengeneza msingi muhimu wa mafanikio yako.

Na kwa wale ambao wapo kwenye ajira, kama hujasoma kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA, chukua hatua ya kukipata na kukisoma leo. Kitabu ni softcopy, kinatumwa kwa email na gharama yake ni tsh elfu 10. Kukipata kitabu, tuma fedha tsh elfu kumi kwa namba 0755 953 887 au 0717 396 253 kisha tuma ujumbe wenye email yako na jina la kitabu kisha utatumiwa kitabu.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog