Chuma ulete wa biashara yako ni huyu hapa na jinsi unavyoweza kumwepuka.

Moja ya changamoto ambazo zinasumbua biashara ndogo ni imani ambazo wafanyabiashara wanazo. Kuna dhana moja ipo kwenye mitaa yetu kwamba kuna watu ambao ni chuma ulete. Watu hawa wanapokuja kwenye biashara yako na kununua kitu, ukiwarudishia chenchi basi baadaye wanahamisha fedha zote kwenye biashara yako kwa nguvu za kishirikina. Watu wamekuwa wakihofia sana hili na hivyo kukataa kabisa kuwauzia baadhi ya watu ambao wanajulikana kama chuma ulete au wakiwauzia basi fedha zao wanaziweka pembeni, wanazitenga kabisa na fedha nyingine.

Mwanzoni nilipokuwa nasikia haya kutoka kwa wafanyabiashara nilikuwa nafikiri ni kitu cha utani tu, kwamba wanatania, lakini kila siku ninapokutana na wafanyabiashara wadogo kwa ajili ya ushauri au mafunzo, hili la chuma ulete huwa halikosekani. Kuna wakati mpaka nimesikia likijadiliwa kwenye vipindi vya redio na televisheni, watu wakilalamika kwamba mitaa fulani huwezi kufanya biashara kwa sababu wapo watu hao wanaofahamika kama chuma ulete.

KUPATA KITABU HIKI BIASHARA NDANI YA AJIRA, BONYEZA MAANDISHI AU PICHA HII.

Leo kupitia makala hii ya KONA YA MJASIRIAMALI tunakwenda kumwangalia chuma ulete huyu ambaye anatesa biashara yako ndogo na jinsi ya kupambana naye ili asiendelee kuharibu biashara yako.

Je chuma ulete wapo?

Swali muhimu la kuanza nalo kwenye makala hii ya leo ni je chuma ulete yupo? Je kuna kitu kama hicho kinachoitwa chuma ulete?

Mwanzoni nilipokuwa naulizwa swali hili kuhusu chuma ulete nilikuwa nawakatalia watu kabisa ya kwamba hakuna kitu kama hicho kinachoitwa chuma ulete. Nilikuwa nawaambia watu kwamba ni imani zao tu ndiyo zinawasumbua, hakuna chuma ulete yeyote ambaye anawachukulia fedha zao kwenye biashara. Lakini baadaye nikaanza kujiuliza kama chuma ulete hakuna, iweje watu wanapata hasara kwenye biashara zao? Iweje mtu mwisho wa siku yake wakati anapiga mahesabu anakuta amepata hasara kubwa? Hapa ndipo niliposhawishika kwamba lazima kutakuwa na chuma ulete.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuishinda Hofu Ya Kupata Hasara Kwenye Biashara.

Je chuma ulete wa biashara yako ni nani?

Baada ya kushawishika kwamba chuma ulete yupo, hatua iliyofuata ilikuwa kumjua chuma ulete kwenye biashara ndogo ni nani. Na hapa nilikuja na jibu ambalo lilinishangaza, kwa sababu lilikuwa na jibu la kweli ambalo likifanyiwa kazi chuma ulete huyo anakimbia kabisa. Jibu nililopata ni kwamba chuma ulete wa biashara zote ndogo ni mfanyabiashara mwenyewe. Ndiyo, yaani kama wewe ulishapatwa na chuma ulete kwenye biashara yako, basi chuma ulete huyo ni wewe mwenyewe. Hakuna mtu mwingine anayeweza kutoka nje ya biashara yako na kuweza kuchukua fedha kwenye biashara yako kwa njia za kishirikina. Fedha kwenye biashara yako zinaweza kutoka kwa njia mbili pekee, njia ya kwanza ni wewe uzitoe mwenyewe, na njia ya pili ni uzipoteze kizembe. Chuma ulete ni pale ambapo unapoteza fedha kizembe kwenye biashara yako.

Kabla hujakataa kwamba wewe siyo chuma ulete wa biashara yako, na kuendelea kusisitiza kwamba kuna watu wanakuja kwenye biashara yako na kuchukua fedha kwa njia za ajabu, naomba ujiulize swali hili; ulishawahi kusikia benki inalalamika kwamba wameibiwa fedha kwa chuma ulete? Umeshawahi kusikia biashara kubwa, kama makampuni wakilalamika kwamba kuna chuma ulete wanawaibia fedha? Kwa nini unafikiri ni biashara ndogo pekee zinazoandamwa na chuma ulete? Kama chuma ulete wangekuwa na nguvu hiyo ya kuchukua fedha kwa nguvu za ajabu, je unafikiri wangechukua fedha wapi, kwenye biashara yako ndogo au kwenye mabenki ambayo yana fedha nyingi?

Chuma ulete hawapo kwenye mabenki wala biashara kubwa kwa sababu kule kila kitu kinaendeshwa kwa taratibu. Hakuna fedha inayotolewa bila ya maandishi, hivyo mwisho wa siku kila kitu kinaonekana kimekwendaje, na mzunguko wote wa fedha unaonekana. Lakini wewe kwenye biashara yako fedha inazunguka bila ya mahesabu yoyote, ukitaka kununua kitu unatoa kwenye droo na kununua, nyumbani wakitaka fedha ya matumizi unatoa na kuwapa, akija mtu kukopa unachukua na kumpa. Unakuwa unajiambia baadaye utakumbuka, lakini kwa uchovu wa siku nzima, inapofika jioni huwezi tena kukumbuka kila kitu ulichofanya kwenye biashara yako kwa siku nzima. unafanya mahesabu na kugundua kuna hasara imejitokeza, na moja kwa moja unafikiria chuma ulete tayari wamekuibia. Nafikiri unaanza kupata picha ni kwa namna gani wewe mwenyewe ni chuma ulete wa biashara yako.

SOMA; Wakati Sahihi Na Wakati Mbaya Wa Kuchukua Mkopo Wa Biashara Benki.

Je unawezaje kuondokana kabisa na chuma ulete kwenye biashara yako?

Wahenga walisema, mali bila ya daftari, hupotea bila ya habari. Hii ndiyo dawa pekee ya chuma ulete kwenye biashara yako. Usikiamini kichwa chako na kufikiri utakumbuka kila kitu kwenye biashara yako, badala yake kuwa na daftari, na kila kitu kinachofanyika kwenye biashara yako kiandikwe. Andika kila fedha inayoingia na kutoka kwenye biashara yako, andika kila mali inayoingia na kutoka kwenye biashara yako, na mwisho wa siku fanya mahesabu kuona kama mambo yanakwenda sawa, kwamba kilichotoka na kuingia kimekwenda sawa na mahesabu yaliyopo kwenye biashara.
Kitu kidogo kama daftari kinaweza kuikoa sana biashara yako, kama utakitumia vizuri na kuzingatia, utaweza kuwa na udhibiti mkubwa wa mzunguko wa fedha kwenye biashara yako. kumbuka fedha ndiyo damu ya biashara yako, hivyo ilinde kwa uwezo wako wote ili biashara yako iweze kustawi na kukuletea mafanikio.

SOMA; Jinsi Ya Kuondokana Na Hali Ya Kukosa Uthubutu Na Kuingia Kwenye Biashara Itakayokufikisha Kwenye Ubilionea.

Wewe ndiye chuma ulete wa biashara yako kwa kukubali kuendesha biashara yako kizembe bila ya kuwa na kumbukumbu sahihi za kibiashara. Ili kuondoa hali hii ya chuma ulete kwenye biashara, hakikisha unakuwa na kumbukumbu sahihi za biashara yako. usichukulie mambo kirahisi, huko ndiyo kunakuletea hasara kila siku. Kila la kheri.

TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

One thought on “Chuma ulete wa biashara yako ni huyu hapa na jinsi unavyoweza kumwepuka.

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: