Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye kipengele chetu muhimu cha mafunzo ambapo tunapeana ushauri wa changamoto mbalimbali tunazokutana nazo katika safari yetu ya mafanikio.
Tunachopaswa kujua ni kwamba changamoto siyo kikwazo kwa mafanikio yetu, bali ndiyo njia ya kuelekea kwenye mafanikio. Hivyo unapokutana na changamoto usichukie wala kukata tamaa, badala yake furahia kwa sababu upo kwenye njia sahihi.
Leo tunakwenda kushauriana njia bora ya kuepuka kuwa chuma ulete wa biashara yako. Na nimetumia neno hili la chuma ulete kwa sababu ndiyo fikra za wafanyabiashara wengi wadogo zilivyo inapokuja upande wa fedha. Kitu cha kushangaza kuhusu chuma ulete ni kwamba huwa wanahangaika na biashara ndogo ndogo tu. Badala wangeenda kuchuma mamilioni ya fedha benki, wao wanahangaika na biashara za mia tano na elfu moja.
Kama hujaelewa mpaka sasa ni kwamba kile wengi wanachoita chuma ulete kwenye biashara ni kushindwa kudhibiti mzunguko wa fedha kwenye biashara. Na kwa kuwa biashara nyingi ndogo hazina mfumo wowote wa kumbukumbu, fedha hazionekani ziko wapi. Sasa kwa kuwa wengi hawapendi kujiumiza kutaka kujua fedha zinapotelea wapi, wanakimbilia jibu rahisi, kwamba kuna chuma ulete.
Nimekuwa nawaambia wafanyabiashara wote hili, hakuna chuma ulete yeyote anayeweza kuidhuru biashara yako, bali wewe mwenyewe ndiye chuma ulete mkuu kwenye biashara yako. Unapokosa nidhamu ya fedha kwenye biashara yako, unaishia kuwa mnyonyaji wa biashara yako bila ya wewe kujua.
Leo nakwenda kukushauri namna bora ya kuepuka kuwa chuma ulete wa biashara yako mwenyewe. Lakini kabla ya kupata ushauri huo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye eneo hili;
Changamoto ni kutokujua tofauti ya faida ya biashara na matumizi. Mimi ni mwajiriwa kipato changu ni kidogo ila nina biashara ndogo ninayoifanya, ila inapokuja kwenye mapato na matumizi najishitukia nimekula, nimegusa hadi na mtaji wenyewe. Naomba msaada nifanyeje? – Veronica J. M.
Kama alivyotuandikia hapa msomaji mwenzetu, wengi wanaoendesha biashara ndogo wanakumbana na changamoto hii ya kushindwa kujua mapato na matumizi, hivyo kila wakati mtaji wa biashara unashuka na kujikuta wanarudi nyuma. Kwa njia hii biashara haiwezi kukua kabisa.
Ili kuondokana na hali hii ili biashara iweze kukua ni kuzingatia haya muhimu sana kwenye uendeshaji wa biashara yako.
Moja; zijue namba muhimu za biashara yako.
Watu wengi huingia kwenye biashara kwa mazoea, hawajawahi kujua namba muhimu za biashara. Wao wanachojua biashara ni kununua na kuuza. Lakini biashara ni zaidi ya hapo. Zipo namba nyingi muhimu za biashara, lakini hapa nakupa zile chache muhimu zaidi.
Mtaji ni fedha unayoweka kwenye biashara, hii hupaswi kuigusa, ni mali ya biashara.
Manunuzi ni fedha unayotoa kununua au kuandaa bidhaa au huduma za biashara yako.
Mauzo ni fedha inayoingia kwenye biashara baada ya mteja kuwa amenunua.
Gharama za kuendesha biashara ni fedha unazotoa ili biashara iweze kwenda, kodi ya eneo la biashara, malipo ya umeme, maji, malipo yako binafsi na wale wanaokusaidia na kingine chochote kinachohitaji fedha kwenye biashara yako.
Faida ni ile fedha ya ziada unayoipata baada ya kutoa mauzo na gharama za kuendesha biashara. Faida inapatikana pale mauzo yanapokuwa makubwa kuliko manunuzi na gharama za kuendesha biashara.
Zijue namba hizi muhimu, kwa sababu ndiyo msingi wa kwanza wa kuwa na udhibiti wa fedha kwenye biashara yako.
Mbili; kuwa na mfumo wa kutunza kumbukumbu kwenye biashara yako.
Wahenga walisema mali bika daftari hutumika bila ya habari. Kauli hii ina ukweli mkubwa na ni muhimu sana kwenye biashara. Kama unaendesha biashara na huna daftari, iwe ni la kawaida au la kielektroniki la kutunza kumbukumbu za biashara yako, haupo kwenye biashara, bali unajifurahisha tu.
Lazima uwe na mfumo wa kumbukumbu kwenye biashara, mfumo huo ndiyo utakuwezesha kujua kama unapata faida au hasara. Unaweza kuanza na daftari ya kawaida, kuwa na upande wa mauzo na upande wa matumizi. Kila fedha inayoingia au kutoka kwenye biashara lazima iandikwe kwenye daftari hilo.
Zipo teknolojia za kurahisisha hilo pia, biashara yako inapokuwa unaweza kutumia teknolojia zikakupunguzia zoezi la kuandika. Lakini kama hujaweza kumudu teknolojia, huna namna, lazima uandike kila fedha inayotoka au kuingia kwenye biashara.
SOMA; Chuma ulete wa biashara yako ni huyu hapa na jinsi unavyoweza kumwepuka.
Tatu; wewe siyo biashara yako.
Hakuna kosa kubwa ambalo wafanyabiashara wadogo wanafanya kama kufikiri kwamba wao ni biashara zao. Wanaona kwa kuwa biashara ni zao, basi wanaweza kufanya chochote kwenye biashara hizo.
Sikia rafiki, wewe unaimiliki biashara, lakini biashara ile siyo wewe. Biashara ni kitu kinachojitegemea kabisa. Hivyo tenganisha maisha yako na biashara yako.
Ikiwa na maana kwamba, usichukue hovyo fedha kwenye biashara kwa matumizi yako binafsi, kama vile unatoa kwenye mfuko wako, heshimu biashara.
Ukishaweka mtaji kwenye biashara, basi usiutoe tena kwa matumizi mengine, iache biashara yako iweze kukua. Kuondoa fedha kwenye biashara, iwe ni kwa matumizi binafsi au mambo mengine ni kuizuia kukua.
Nne; jilipe mshahara au kamisheni kutoka kwenye biashara hiyo.
Baada ya kuitenganisha biashara na wewe, jua huwezi kuondoa hata shilingi mia moja kwenye biashara yako na kununua peremende. Au kutoa kitu kwenye biashara kwa matumizi binafsi. Unapaswa kuiacha biashara ijiendeshe yenyewe kwa uhuru bila ya kuiingilia.
Hivyo wewe unapaswa kujilipa mshahara au posho au kamisheni kutoka kwenye biashara yako. Na malipo unayojilipa yatoke kwenye faida, siyo kwenye mauzo. Ukiona umefanya mauzo makubwa usifikiri una fedha nyingi, badala yake kokotoa kwanza faida kisha jilipe kutoka kwenye faida ile.
Na pia usijilipe faida yote, bali sehemu ya faida inapaswa kurudi kwenye biashara ili iweze kukua zaidi.
Usitoe tu fedha kwenye biashara, bali toa kwa mfumo wa kujilipa, na unachojilipa kiwe kinatoka kwenye faida na siyo vinginevyo. Kama biashara haina faida hupaswi kujilipa hata senti moja, utaiua.
Tano; usikopeshe.
Hakuna sumu kubwa kwenye biashara ndogo kama kukopesha wateja wako. Mtaji wako ni mdogo, unapokopesha wateja unaondoa mtaji kwenye biashara yako. Weka msimamo wa kutokukopesha kwenye biashara yako na waeleze wateja wako wazi kwamba kutokana na ufinyu wa mtaji wako, hutaweza kuwakopesha.
Usihofie kuacha kukopesha kwa kuogopa kuwapoteza wateja, ni kweli usipokopesha kuna wateja utawakosa, ila ni wale wateja wasumbufu ambao kuwakosa ni baraka kwako. Toa huduma bora sana kwa wateja unaowapata, ambao wapo tayari kulipa fedha taslimu na achana na wale wakopaji.
Ukizingatia mambo haya matano, na kuyafanyia kazi kila siku kwenye biashara yako, utaacha kuwa chuma ulete wa biashara yako mwenyewe, utaona kila senti ya biashara yako ilipo na utaweza kuikuza zaidi biashara yako hata kama umeanzia chini kabisa.
Jambo la nyongeza ni kujifunza kila siku ili uweze kuwa bora na kufanya maamuzi mazuri kwenye biashara yako. Ukichagua kuingia kwenye biashara, umechagua kuwa mwanafunzi maisha yako yote. Na unapaswa kujifunza kwa kusoma vitabu, siyo kusoma mitandao ya kijamii. Nimekuandalia programu nzuri sana kwako ya kusoma na kujifunza, kama bado hujajiunga nayo soma hapa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kusoma Vitabu Zaidi Ya 50 Kwa Mwaka Hata Kama Huna Muda Au Fedha Za Kununua Vitabu Vingi.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog