Kama kitu ni muhimu sana kwako, basi lazima utapata njia ya kukifanya, hutakuwa na sababu yoyote kwa nini huwezi kufanya.
Kama kitu ndiyo pekee unategemea, yaani huna namna nyingine, utatafuta kila njia uweze kukifanya, sababu yoyote itakayojitokeza mbele yako hutaipokea, badala yake utatafuta njia ya kuweza kufanya.
Hivyo kama kuna kitu ambacho umekuwa unataka kufanya lakini umejikuta unaahirisha, jua jambo hili moja, hujakifanya kuwa muhimu sana kwako. Hujakifanya kitu hiko kuwa ndiyo pekee unachohitaji na huna namna nyingine.
Chochote unachokitaka kwenye maisha yako, kipe umuhimu mkubwa, na utaona fursa ya kuweza kukifikia au kukifanya. Akili zetu zina uwezo mkubwa wa kutupatia kile ambacho tunakitaka kweli. Kama kitu ni muhimu sana kwako hakitaondoka kwenye mawazo yako na hivyo kuwa rahisi kuziona fursa zinazoendana na kile unachotaka.
Weka umuhimu mkubwa kwenye kile unachotaka, ona hiko ndiyo kitu pekee unachotaka na huna namna nyingine zaidi ya kukipata, na akili yako itakuonesha kila fursa iliyopo kwa wewe kufikia kile unachotaka. Unachohitaji hapo ni wewe kuchukua hatua, ili uweze kupata unachotaka.
SOMA; KIPAUMBELE; Uhusiano Kati Ya Mafanikio Makubwa na Kuweka Kipaumbele.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kitu chochote ambacho ni muhimu kwangu ni lazima nitapata muda wa kukifanya, hata kama kuwe na sababu gani. Na kitu chochote ambacho nimekuwa naahirisha kufanya mpaka sasa, sababu kubwa ni kwa kuwa sijakiwekea umuhimu mkubwa. Kuanzia sasa chochote ninachotaka kufanya nitakiwekea umuhimu mkubwa sana na najua nitaweza kukifikia.
NENO LA LEO.
Kitu chochote ambacho ni muhimu sana kwako ni lazima utapata muda wa kukifanya, hata kama kuna sababu za kukuzuia.
Kama kuna kitu umekuwa unaahirisha, sababu kuu ni wewe kutokukiwekea umuhimu mkubwa na hivyo kutokipa kipaumbele.
Chochote unachotaka kufanya, kiwekee umuhimu mkubwa sana, na akili yako itakuonesha kila fursa ya kuweza kukifikia.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.