Tabia zetu zina athari kwenye biashara au kazi tunazofanya. Kuna baadhi ya mambo tunaweza kuwa tunafanya na yakawa yanaharibu sana sifa zetu kwenye biashara na hata kazi. Mwandishi na mshauri Barbara Pachter anatushirikisha tabia za kuzingatia kwenye maeneo yetu ya kazi na hata biashara katika kitabu chake The Essentials Of Buseness Etiquette.

Karibu tujifunze kwa pamoja na tuyatumie kwenye maeneo yetu ya kazi ili kuongeza thamani zetu.

1. Kufanya kazi yako vizuri pekee haitoshi kwenye dunia ya sasa ambayo ina ushindani mkubwa, badala yake unahitaji kuonekana wa tofauti kutokana na tabia zako unazoonesha kwenye eneo lako la kazi na jinsi unavyojichanganya na wengine. Unahitaji kuwa na mwonekano wa kitaalamu na hata mahusiano yako na jinsi unavyofanya mambo yako kuendane na ulimwengu wa biashara.

2. Mara zote unapoongea au kuwasiliana na mtu ambaye hakujui na humjui basi jitambulishe kwa majina yako mawili kwa usahihi. Usitumie jina moja pekee na hata kama unaongea kwenye simu jitambulishe kwa majina yako kamili. Na pia unapoongea na mtu unayejua jina lake au ambaye ameshakuambia jina lake, mwite kwa majina yake kamili. Usifupishe jina la mtu labda kama ndiyo anapendelea kuitwa hivyo. Kama mtu anaitwa Elizabeth mwite hivyo hivyo, usimuite Eliza.

3. Unaposalimiana na watu kwenye mazingira ya kikazi au kibiashara basi kushikana mikono ni muhimu. Na jua namna sahihi ya kushikana mikono (handshake), kidole gumba lazima kiwe juu. Pia mkono wako unahitaji kuwa imara na siyo legelege. Mtu anaposhika mkono wako anaondoka na picha kama uko imara au upo dhaifu.

4. Unapoongea na watu au kutoa hoja yako, hakikisha unasimama. Kuongea ukiwa umekaa ni rahisi watu kupuuza au wasikusikilize kwa makini. Lakini unaposimama unawafanya wawe makini na kukusikiliza vizuri. Pia unaposimama unaonesha nguvu ya kujiamini na hivyo wengine nao wanakuamini.

5. Popote unapokwenda kwa mazungumzo ya kikazi au kibiashara hakikisha umebeba kadi zako za kibiashara (business cards). Kadi hizi zina maelezo muhimu kuhusu wewe na ni njia rahisi ya kujitangaza kw akile unachofanya na hata kutoa mawasiliano yako. pia kwenye kadi yako weka anwani ya mitandao ya kijamii unayotumia.

6. Unapokutana na mtu kwa mara ya kwanza, mara nyingi inakuwa vigumu kuanzisha mazungumzo. Hii inaweza kukunyima fursa nzuri, mara zote kuwa mtu wa kuanzisha mazungumzo na wengine. Na anzisha mada ambazo ni rafiki na salama. Mara kama hali ya hewa, michezo, habari zinazoendelea, safari na hata foleni za barabarani ni sehemu nzuri ya kuanzia. Epuka kuingia kwenye mazungumzo yanayohusu dini, siasa au mapenzi, haya yatakuharibia kibiashara.

7. Sheria ya msingi ya mazungumzo ni kusikiliza, hivyo kuwa msikilizaji mzuri sana. Usiwakatishe wengine kabla hawajamaliza sentensi zao, weka mawazo yako yote kusikiliza kile ambacho mtu anaongea. Usichezee vitu au kushika sehemu za mwili wako kama nywele wakati mwingine anaongea. Sikiliza kwa makini na unapofika wakati wako ongea.

8. Sema asante, hili ni neno ambalo litakupa fursa nyingi sana kwenye kazi na biashara. Kitu chochote ambacho mtu anafanya na kikakusaidia kwa namna moja au nyingine mwambie asante. Mtu anafurahi sana pale unapothamini mchango wake hata kama ni kidogo, na hii itawahamasisha kukusaidia zaidi pale unapohitaji msaada wao.

9. Popote unapokuwa, kuna picha ambayo unaituma kwa wengine. Je watu wengine wanakuonaje unapoingia kwenye chumba? Ni mawazo gani ambayo yanawajia watu wanapokuona unaingia mahali? Kumbuka huwezi kuwazuia watu kukuchukulia vile wanavyotaka wao ila unaweza kujenga mazingira ambayo yatawafanya wakuchukulie vizuri. Mara zote fanya mambo yako na ongea kitaalamu, unachotoa ndicho wengine wanachopokea. Onesha picha kwamba wewe ni mtu makini na wengine watakuchukulia hivyo.

10. Jinsi unavyotembea, unavyosimama na hata unavyokaa kunaeleza vizuri sana kuhusu wewe. Kama unatembea umeinama kidogo, mabega umeshusha chini na mikono ipo lege lege unaonekana kama mtu asiyejiamini na aliyekata tamaa. Lakini kama unatembea ukiwa umesimama wima, mabega yako sawa na mikono ipo pembeni ya mwili unaonesha kujiamini na kuwa kitaalamu. Pia unapokaa kuna mikao ya watu makini na mikao ya watu ambao siyo makini. Moja ya mambo unayotakiwa kuepuka unapokaa ni kuweka mguu mmoja juu ya mwingine.

11. Kuwa makini na kauli unazotumia hasa unapouliza au kujibu kitu. Kauli zako zinaonesha kama wewe ni mtu makini au la. Epuka sana kauli hizi sita;

Moja; Samahani, naweza kukuliza swali? Huna haja ya kuomba samahani, uliza swali.

Mbili; Nisamehe kwa kukusumbua… kwa nini umsumbue mtu, uliza je una muda.

Tatu; Natumaini kama una muda wa…. usiweke matumaini, uliza kama mtu ana muda.

Nne; asante kwa kunisikiliza. Sema tu asante, inatosha.

Tano; kwa kuwa mwaminifu… kusema hivi unaonesha kuna wakati huwa sio mwaminifu.

Sita; nilikuwa najiuliza kama… hii inaonesha kama hujiamini kwa swali unalouliza, usianze na kauli hiyo, uliza swali.

12. Mavazi yako yana mchango mkubwa sana kwa jinsi wengine wanavyokuchukulia. Mara zote vaa kiheshima, kitaalamu na vaa kulingana na tukio. Unapokuwa kazini au kwenye biashara, vaa mavazi ambayo yamezoeleka sehemu za kazi au biashara. Suti nyeusi ni vazi ambalo linaonesha nguvu na kujiamini. Epuka nguo zenye rangi kazi, zinawafanya watu wakuone sio mtu makini.

13. Usivae vitu ambavyo vitawafanya watu wakuhukumu kwa ulichovaa badala ya kukuhukumu kwa uwezo wako. Kwa wanawake vaa nguo ambazo ni za heshima, ambazo haziachi mwili wako wazi. Pia urembo usiwe mwingi kiasi cha watu kukushangaa badala ya kufanya kazi iliyowaleta pamoja. Marashi pia yasiwe makali kiasi cha kuwafanya watu waulize kila mara marashi ya nani makali.

14. Kwenye chakula pia kuna mambo mengi unayohitaji kuzingatia kwenye uwapo kwenye shughuli ya kikazi au kibiashara. Kama wewe ni mgeni agiza kama mwenyeji wako anavyoagiza. Kama wewe ni mwenyeji mpe mgeni nafasi ya kuagiza kwamba, na lipia bili. Pia wakati wa kula weka simu mbali na wewe.

15. Unapokula kwenye mgahawa au hoteli, kuwa mkarimu kwa wahudumu wanaokuhudumia. Tabia yako inapimwa kwa jinsi unavyowachukulia watu ambao hawana nguvu ya kukuharibia chochote. Kama ukiwa mkali sana na kudharau wahudumu, wengine wanaliona hilo na wataepuka kufanya kazi au biashara na wewe. Hata kama mhudumu amekosea, usifanye jambo ambalo sio la kiungwana.

16. Kupata chakula pamoja pia ni njia ya kutatua migogoro ya kikazi au kibiashara. Kama kuna mtu ambaye hamna mahusiano mazuri kikazi au kibiashara unaweza kumwalika kupata chakula cha pamoja na hapo mkapata nafasi ya kutatua tofauti zenu.

17. Mitandao ya kijamii ni mizuri lakini pia inaweza kuwa mibaya sana kwa kazi au biashara yako. unapotumia mitandao hii tumia kwa akili na jua ni mambo gani ya kuweka kwenye mitandao na ipi siyo ya kuweka. Yafuatayo ni mambo ambayo ni marufuku kuweka kwenye mitandao ya kijamii;

Moja; malalamiko yoyote kuhusu kazi yako au biashara yako.

Mbili; kumsoma vibaya bosi wako au mfanyakazi mwenzako.

Tatu; kuonesha kwamba kazi yako huipendi.

Nne; picha na habari za maisha yako binafsi, ambayo usingependa kila mtu ajue.

Tano; burudani au starehe unazofanya, usiweke picha au habari ukiwa unatumia vilevi au ukiwa kwenye hali nyingine ambazo usingependa kila mtu aone.

18. Mitandao ya kijamii ina nguvu kubwa ya kukupatia kazi na hata kukupotezea kazi. Zama hizi waajiri wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuangalia sifa za waombaji wa kazi. Hivyo kama kwenye wasifu wako umeandika wewe ni mchapakazi na chanya, halafu kwenye kitandao yako ya kijamii ni mlalamikaji wa kila kitu na unapost mambo yanayohusu ‘BATA’ pekee, hakuna atakayekuwa tayari kukuajiri. Kuna watu wengi wamefukuzwa kazi kwa mambo waliyoandika wkenye mitandao ya kijamii, kuwa makini.

19. Kuna mitandao mikuu mitatu ya kijamii ambayo ni lazima uwepo kama kweli upo makini kwenye kazi au biashara unayofanya.

Mtanzao wa kwanza ni FACEBOOK; Huu ndiyo mtandao wa kijamii wenye watumiaji wengi zaidi. Mtandao huu utakukutanisha na wengi na unaweza kuutumia vizuri kuwashirikisha wengine ujuzi wako na uzoefu wako pia.

Mtandao wa pili ni TWITTER; Huu ni mtandao ambao unatumia kushirikishana habari fupi fupi wa mambo yanayoendelea. Kupitia mtandao huu unaweza kutengeneza sauti yako na ukawa na wafuasi wanaoamini kile ambacho unaamini wewe.

Mtandao wa tatu ni LINKEDIN; Huu ni mtandao ambao umekaa kitaalamu zaidi. Mtandao huu unakusaidia kuwaeleza watu wasifu wako na pia kukukutanisha na watu wanaotafuta kile ambacho unacho. Huu unachukuliwa kama mtandao wa kijamii ambao ni wa kitaalamu zaidi na watu wenye taaluma mbalimbali wanakutana kupitia mitandao hii.

Kuna mitandao mingine lakini haina nguvu sana, hakikisha unakuwa kwenye hii mitatu, na unakuwa hai.

20. Haijalishi unafanya kazi au biashara gani, unahitaji kuwa na blog. Blog yako inakuwa ni sehemu ya kuishirikisha dunia ujuzi na uzoefu ulionao. Kwa kuwa na blog ambayo unaandika mara kw amara kuhusu kile unachofanya, unaonekana ni mtaalamu zaidi na unaweza kuitumia kama wasifu wako. Kama ni biashara watu wanaweza kukujua kupitia blog yako na hivyo kukuamini na kufanya biashara na wewe. Kama ni kazi, ukiitwa kwenye usaili na mkawa watu ambao mna sifa sawa, kama wewe una blog ambayo unaandika kuhusiana na utaalamu wako utapewa kipaumbele kuliko yule ambaye hana. Ni muhimu uwe na blog, hii inaonesha ni nini hasa unacho bila ya kujali elimu yako au umetokea wapi.

Hayo ni mambo muhimu unayohitaji kuzingatia kwenye tabia na mahusiano yako ya kibiashara. Yafanyie kazi na mara zote hakikisha unatuma picha nzuri kwa wale unaofanya nao kazi au biashara.

Nakutakia kila la kheri.