Kama umewahi kuona biashara zinazofanya vizuri sana lakini ikatokea zikafa ghafla, unatakiwa kujua ya kwamba kifo cha biashara hizo hakitoki nje bali ndani ya biashara.  Na kwa biashara zote kinachopelekea biashara kufa siyo sababu za nje, bali sababu za ndani. Na hivi piia ndivyo ilivyo kwa mafanikio ya biashara, yanaanzia ndani ya biashara yenyewe.

Kumekuwa na hatari ambazo wafanyabiashara wamekuwa wanazitengeneza wao wenyewe kwenye biashara zao. Hatari hizi zimekuwa zikisababisha biashara zao kukutana na ushindani mkubwa na kupelekea biashara kufa kabisa.

Pale biashara inapokwenda vizuri, inapojiendesha kwa faida, wamiliki wengi wa biashara hujisahau. Huchukulia kwamba mambo ni mazuri na kuona yataendelea kuwa mazuri wakati wote. Kwa kuridhika huku wanaacha kuwa wabunifu, wanaacha kulisoma soko linahitaji nini zaidi. Wafanyabiashara wengine wanaiona fursa kubwa ambayo bado haijatumika na wanaitumia vizuri. Hali hii huleta ushindani mkali ambao hupelekea biashara kufa.

Dunia ya sasa mabadiliko yanatokea kwa haraka sana, na kila siku kuna vitu vipya vinakuja na vitu vingine vinasahaulika. Kama wewe mfanyabiashara huangalii mambo yanavyokwenda na kuipanga biashara yako kwenye mwelekeo huo, unaiweka biashara yako kwenye hatari. Unatoa nafasi wa wengine kukutoa wewe kwenye soko lako na pia unakosa fursa ya kuikuza zaidi biashara yako.

Biashara inatakiwa kubadilika la sivyo inapotea, hivi ndivyo mambo yanavyokwenda kwenye ulimwengu wa sasa wa utandawazi na maendeleo ya kiteknolojia. Kadiri teknolojia inavyokua wateja wanazidi kupata nguvu ya kuchagua. Sio mfanyabiashara anayeamua tena awauzie watu nini, bali watu ndio wanaoamua wanunue nini na wanunue watu. Watu wana taarifa za kutosha juu ya mahitaji yao na wanajua ni wapi wanayapata. Na pia mabadiliko yanapotokea wanapata taarifa haraka.

Njia pekee ya kuendelea kuikuza biashara yako kwenye nyakati hizi ni kuwa mbunifu. Kuwa mbunifu kwa kuangalia mabadiliko yanayotokea kwenye biashara yako na biashara kwa ujumla. Angalia mabadiliko kwenye mahitaji ya wateja wako. Angalia mabadiliko kwenye utoaji wa bidhaa au huduma za biashara yako, na angalia ni kwa jinsi gani biashara yako inaweza kuwa bora zaidi kwenye maeneo hayo.

Pia kuwa mbunifu kwa kufikiria mahitaji ya wateja wako ambayo wao wenyewe hawajayajua kwa sasa. Hapa unaangalia mambo yanavyokwenda na unapata picha kwamba huko mbeleni mambo yatakuwa tofauti na yalivyo sasa na hivyo kuandaa vile ambavyo vitahitajika wakati huo. Kwa kuweza kuona kinachoweza kubadilika na kufanyia kazi utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuwa wa kwanza kuwapatia wateja wako mahitaji yao kabla washindani wako hawajatumia nafasi hiyo.

Unahitaji kuwa mbunifu katika utoaji wako wa huduma kwa wateja wako. Usifanye kitu chochote kwa mazoea kwenye biashara yako. Wateja wanapoona kwamba wameshazoea kitu fulani, hupenda kujaribu kitu kipya na hivyo kwenda kwa wengine wanaofanya biashara kaka yako. Kama kule watapatiwa huduma bora hawatarudi tena kwako. Mara zote kuwa mbunifu kwa kuwapa wateja huduma bora ambazo hawakutarajia kupata kwenye biashara zako. Hili litawafanya waendelee kufanya biashara na wewe kwa sababu wanajua kuna kitu bora watakipata. Ila kama watajua mambo yanaenda kwa mazoea, hawatasukumwa kuja kwenye biashara yako.

Ushindani wa biashara kwa sasa ni mkali sana. Kila mtu anaweza kufanya biashara unayofanya wewe. Na kuna uwezekano ulianza kufanya biashara hiyo kwa sababu uliona wengine wanafanya, au hata kama uliibuni mwenyewe, wengine wakiona inakuletea faida na wao watakuiga na kuanza kuifanya. Hivyo ukileta mazoea utazidiwa haraka sana na wengine.

Kuwa mbunifu kwenye biashara yako na mara zote tafuta njia za kumpatia mteja wako kilicho bora zaidi. Ukifanya kwa mazoea utatengeneza hatari ya biashara yako kuondolewa sokoni na washindani wako. Mambo yanapokuwa mazuri kwenye biashara jua ni kwa muda tu na sio kwamba yatadumu hivyo. Ili yaweze kudumu unahitaji kuwa mbunifu kila mara na kuja na vitu vipya ambavyo vitawafanya wateja wapende kufanya biashara na wewe. Kila la kheri.