Tofauti ya uongozi na usimamizi ni kwamba kwenye uongozi watu wanachagua kukufuata, wanachagua kufanya kile ambacho unawashawishi wafanye. Kwenye usimamizi ni watu wanalazimika kukufuata, hawana namna ila lazima wafanye kile unachowataka wafanye.
Bila ya shaka uongozi unakufikisha mbali kuliko usimamizi. Maana watu wanapochagua wao wenyewe wanajitoa kuliko unapowalazimisha.
Sasa kuna sifa moja ya uongozi ambayo unapaswa kuijua na kujijengea. Kwa sifa hii watu wanaamua kukufuata na kufanya kile unachowashawishi wafanye.
Sifa hii ni kujua unakokwenda na kuwa na uhakika na kile unachotaka. Watu wanapenda kuwafuata wale watu ambao wanajua ni wapi wanakwenda, wanajua ni nini wanataka na wanaujasiri wa kukiendea. Kama wewe mwenyewe hujui ni wapi unakwenda, watu watakufuataje? Kama wewe mwenyewe hujui ni nini unataka, unawezaje kuwashawishi watu? Kama huna ujasiri wa kuendea kitu ni kipi kitawavuta watu kwako?
Jua unachotaka, jua unapokwenda na kuwa na ujasiri wa kuchukua hatua.
SOMA; Mahitaji Manne Ya Mtu Kuwa Kiongozi.
TAMKO LANGU;
Nimeijua sifa kuu ya uongozi ambayo ni kujua ninapotaka kwenda na kipi hasa ninachotaka. Pia nahitaji kuwa na ujasiri katika kuendea kile ninachotaka. Nimechagua kuwa kiongozi kwenye maisha yangu kwa sababu najua wapi nataka kufika, nini ninataka na nina ujasiri wa kufanyia kazi.
NENO LA LEO.
Kwenye uongozi watu wanachagua kumfuata mtu, kwenye usimamizi watu wanalazimika kumfuata mtu. Watu wanachagua kuwafuata wale ambao wanajua ni wapi wanakwenda, ni nini wanataka na wana ujasiri wa kuendea kile wanachotaka.
Ili kuwa kiongozi bora jua ni wapi unapokwenda, ni nini unachotaka na kuwa na ujasiri wa kuendea kile unachotaka. Watu watachagua wao wenyewe kukufuata.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.