Moja ya vitu vinavyowafanya wengi kushindwa kuchukua hatua z akuboresha maisha yao ni vikwazo au changamoto wanazokuwa nazo au kukutana nazo. Muulize mtu yeyote ambaye amekuwa anasema anataka kuanza biashara ila haanzi, atakupa sababu nyingi sana kwa nini mpaka sasa hajaanza. Atakuambia mtaji, wazo, muda, usimamizi na kadhalika.

Lakini sababu au vikwazo ambavyo tunatoa havisaidii chochote, bado vinatuacha na hali kwamba hatujafanya tulichotaka kufanya. Na mwisho wa siku tutabaki kuwa washindwa na sababu tunazotoa hazitasaidia chochote.

Hapa kuna njia nyingine ya kuliangalia hili, na njia hii ni kuichukulia ile sababu kubwa ya kushindwa kuanza iwe ndiyo fursa kwako kuanza. Kwa mfano kama sababu ya kushindwa kuanza biashara ni mtaji, basi tumia hii kama fursa, na jiulize ni biashara zipi ambazo unaweza kuanza kwa mtaji kidogo na ikakua zaidi siku zijazo. Kama kikwazo ni muda, jiulize ni biashara gani unaweza kuianza kwa muda mdogo ulionao na ukaweza kuikuza.

Lengo hapa ni wewe usiishie tu kusema siwezi kwa sababu hii, badala yake sema je hali hii inanisukumaje kuanza. Ukianza kutumia vikwazo kama fursa zenyewe, hakuna kitakachokushinda na utapiga hatua kubwa.

Wanaofikia mafanikio makubwa siyo watu wa sababu bali ni watu wa vitendo, ondoa sababu na kuwa mtu wa vitendo. Kile kinachokuzuia kifanye kuwa ndiyo fursa yako.

SOMA; ONGEA NA KOCHA; Tabia Moja Inayokuingiza Kwenye Matatizo Na Kukunyima Fursa Nyingi.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kwenye jambo lolote ninalotaka kufanya nitakutana na vikwazo au changamoto. Vikwazo hivi vinaweza kunizuia kama nitavichukulia kama vikwazo, ila kama nitavichukulia kama fursa nitaona njia nyingi ninazoweza kutumia kufanya. Kuanzia sasa kila kinachonizuia nitakibadili kuwa fursa, na nina uhakika nitafanya makubwa sana.

NENO LA LEO.

Jambo lolote utakalotaka kufanya kwenye maisha yako, utakutana na vikwazo na changamoto. Hivi vinaweza kuwa sababu tosha ya kukuzuia usifanye. Lakini unaweza kuvishinda kwa kuamua kugeuza vikwazo na changamoto hizi kuwa ndiyo fursa bora kwako kuchukua hatua.

Usiseme huwezi kwa sababu umekosa hiki, badala yake sema nimekosa hiki na hivyo nitatumia hali hii kufanya hivi. Ni mabadiliko madogo kwenye mtazamo wako lakini yana matunda mazuri sana.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.