The 50th law ni kitabu kilichoandikwa na mwandishi Robert Green ambapo amefuatilia maisha ya mwanamuziki 50 Cent ambaye ameweza kufanikiwa sana kwenye muziki. Mwandishi alifuatilia kwa makini maisha ya mwanamuziki huyu ambaye amepitia maisha magumu sana lakini bado akaweza kufikia mafanikio makubwa. katika uchambuzi wake, mwandishi aliweza kuona falsafa moja ambayo imemwezesha mwanamuziki 50 cent kuweza kufanikiwa sana. Na falsafa hii ni kuweza kuishinda hofu. Hofu ndiyo inazuia watu kuchukua hatua kwenye maisha yao na hivyo kushindwa kufikia mafanikio makubwa.
Hapa nakushirikisha mambo muhimu niliyojifunza kupitia kitabu hiki. Karibu tujifunze kwa pamoja.
- Kila binadamu ana hofu, na hofu hii tumeirithi kutoka kwa binadamu wa zamani sana ambao waliishi kwenye mazingira magumu na ya hatari. Hofu ndiyo iliwawezesha kuwa salama na kuendeleza uzao wa binadamu. Hofu hii iliwafanya kuepuka wanyama wakali, kuepuka mazingira mabaya kama baridi kali na hata joto kali. Hali hizi ziliwalazimisha kukaa pamoja na kufanya maamuzi kama kundi.
- Pamoja na muda mwingi kupita, pamoja na mazingira kubadilika na kuwa bora sana, bado watu tumeendelea kuwa na hofu kubwa. Na hofu hizi zimehama kutoka kwenye mazingira na hali ngumu, na sasa zimeelekea kwa wengine na kushindwa. Wengi wanashindwa kuchukua hatua kwa sababu wanahofia wataonekanaje na wengine, au wanaogopa kushindwa.
- Dunia ya sasa imekuwa na ushindani mkubwa sana ambao mtu asipokuwa imara na jasiri hawezi kufikia mafanikio. Na njia ya kwanza ya kuweza kuvuka ushindani huu mkali ni kuondokana na hofu. Unapokuwa na hofu unafikiria upande hasi wa jambo lolote na hivyo kushindwa kuchukua hatua. Lakini unapokuwa jasiri unaona upande chanya na kuhamasika kuchukua hatua.
- Kuna njia mbili za kupambana na hofu, njia ya kwanza ni ya moja kwa moja na njia ya pili ni isiyo ya moja kwa moja.
Njia isiyo ya moja kwa moja unaikimbia hali inayokuletea hofu, au kujaribu kukwepa hali hiyo. Kwa mfano mtu anaweza kuahirisha kufanya maamuzi kwa sababu anahofia matokeo yanaweza yasiwe mazuri. Kwa njia hii huwezi kufanya makubwa.
Njia ya moja kwa moja ni pale ambapo unakutana na hali ambayo huna namna bali kuchukua hatua. Hii ni njia ambayo itakuwezesha kufanya mambo makubwa.
- Kinachowatofautisha watu wanaochukua hatua na wale wanaokwepa kuchukua hatua ni vitu viwili; nia na madaraka. Wale ambao wana nia ya dhati ya kupata au kufanya kitu watafanya kila linalowezekana kukipata. Na pia wale ambao wana njaa ya madaraka, watachukua hatua bila ya kuhofia chochote.
- 50 Cent anasema hofu kubwa sana ambayo watu wengi wanayo ni hofu ya kuwa wao kama wao. Wengi wanaiga maisha ya wengine, wanataka kuwa kama watu fulani ambao wanaona wamefanikiwa, na wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya hata kama hakiendani nao. Hakuna mtu anayeweza kusonga mbele na kufikia mafanikio makubwa kwa njia hii, nguvu inakuwa ndogo na hakuna anayejali kwa sababu hakuna cha tofauti unachofanya. Hapo unakuwa unakimbia kitu kimoja ambacho kinaweza kukuletea mafanikio makubwa, wewe mwenyewe. 50 Cent aliweza kuishinda hofu hii na kuchagua kuishi maisha yake yeye kama yeye na kuweza kufika mbali zaidi.
- Sisi binadamu tuna udhibiti mdogo sana wa mazingira yetu. Hatuwezi kuchagua kitu gani kitokee, na pia hatuwezi kuzuia vitu vingi vinavyotokea. Lakini tuna udhibiti wa kitu kimoja muhimu sana, mtazamo wetu. Kwa lolote lile linalotokea, liwe baya au zuri kiasi gani, haliwezi kukuathiri kama wewe mwenyewe hutachagua kuathirika nalo. Kama unaweza kuwa na mtazamo huu unaweza kubadilisha chochote kinachotokea na kikawa bora sana kwako.
- Kitu kingine kikubwa ambacho kinatupa hofu ya kuchukua hatua na kuishi yale maisha ambayo ni halisi kwetu ni tabia yetu ya asili kama binadamu. Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, tunapenda kuwa sehemu ya jamii na hivyo tunalazimika kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Kwa sababu tuna hofu kwamba tukifanya tofauti, wengine hawatatukubali. Lakini wale wanaofikia mafanikio wanathubutu kuwa tofauti na jamii nzima inawakubali zaidi kwa uthubutu wao. Amua na wewe kuwa mmoja wa watu hawa.
- Unatakiwa kuweza kujua ukweli kama kweli unataka kuishinda hofu na kufanya mambo makubwa. kwa sababu mambo mengi ambayo tunayaona au kuyafikiria siyo ukweli au uhalisia, bali ni maigizo ambayo tumetengeneza kwenye akili zetu. Tunapokutana na hali ngumu au changamoto, badala ya kupambana kuondokana nazo, huwa tunatafuta njia rahisi ya kuondoka kwenye hali hiyo na hapa ndipo maigizo huanza. Tunaanza kufikiria maisha yangekuwaje kama tusingekuwa na changamoto hiyo, au kutafuta nani kasababisha au kuikimbia kwa kutumia vileo na vitu vingine. Lakini ukweli ni kwamba una changamoto na kama unataka kuondokana nayo unatakiwa kuchukua hatua, bila ya kuwa na hofu.
- Mambo yanapokwenda vizuri watu huwa wanajisahau na kuona yatakwenda hivyo hivyo, kitu ambacho ni hatari sana kwani hujikuta kwenye wakati mgumu. Mambo yanapokuwa magumu watu hujaribu kukimbia na kufikiri kwamba ugumu utaondoka wenyewe. Hivi ndivyo jamii inavyochukulia mambo. Unatakiwa kuona uhalisia, kwamba kama mambo ni mabaya unahitaji kuchukua hatua, na kama mambo ni mazuri uzuri huo hautadumu milele, bali unahitaji kuchukua hatua ili mambo yaendelee hivyo, ukijisahau na kuona umeshaweza kila kitu ndiyo unaanza kupotea.
- Unahitaji kutengeneza mafanikio yako mwenyewe, hakuna anayekutengenezea wewe mafanikio. Ni lazima uweze kujitegemea na kutumia kila fursa unayoipata ili kufikia mafanikio unayotaka. Miliki kile ambacho unakifanya, fanyia kazi kile ambacho unakiamini na weka juhudi zako zote, Usitegemee wengine moja kwa moja kwa kila kitu, ni kujiweka kwenye hatari kubwa.
- Unapowafanyia kazi wengine, iwe ni kwa ajira au utaratibu mwingine, wao ndio wanamiliki kazi unayofanya, na wanakumiliki na wewe pia. Na mbaya zaidi wanachukua kujiamini kwako na hivyo unahofu kama ukichukua hatua mwenyewe huwezi kufika mbali. Ni muhimu uweze kujitoa kwenye hali hizi za kuruhusu wengine wamiliki kazi yako na wewe pia na ufikie hatua ya kumiliki kazi yako na kuweza kuchukua hatua kwa kile unachotaka.
- 50 Cent anasema kwamba siyo malengo ya bosi wako kukufanya wewe ufanikiwe, hata kama bosi wako ni rafiki yako. Lengo la bosi wako ni kukutumia wewe ili kufikia malengo yake yeye, na anahakikisha anakupa kiasi kidogo ya kile unachomtengenezea, na kukupa hofu kwamba peke yako huwezi. 50 Cent alichukua maamuzi kwamba hatokubali kuajiriwa na mtu, ni bora afe akiwa anapambana mwenyewe. Hii ni muhimu kwa kila mtu anayetaka kufikia mafanikio makubwa, ni lazima uweze kumiliki kile unachofanya na kumiliki maisha yako pia.
- Utegemezi ni tabia ambayo ni rahisi sana kuishika. Kwa sababu tunaishi kwenye jamii ambayo imetengeneza mazingira mengi ya utegemezi, washauri wa kila jambo, dawa za kutimu kila tatizo la kisaikolojia, starehe za kupotezea muda na ajira za kutuwezesha kusogeza maisha. Hizi zote ni hali za utegemezi ambazo zinawafanya watu washindwe kusimama wenyewe kwa kuwa jamii nzima haijazoea kuona watu wakisimama wenyewe. Ni lazima uweze kusimama na kukataa kumezwa na utegemezi huu uliotengenezwa na jamii. Kama huna furaha usitafute starehe gani itakayokupa furaha, bali tafuta ni nini hufanyi ambacho kinafanya maisha yako yasiwe na furaha.
- Kitu pekee unachotakiwa kukithamini sana kwenye maisha yako ni umiliki na siyo fedha. Kama utajikuta kwenye hali ya kuchagua kati ya kuwa na umiliki au kupata fedha nyingi, chagua kuwa na umiliki, maana umiliki utakutengenezea uhuru ambao utakuwezesha kutengeneza fedha nyingi sana baadaye. Kwa mfano umepata kazi mbili, kazi moja unapata mshahara mkubwa lakini inachukua muda wako wote, huwezi kufanya kitu kingine cha ziada, na kazi nyingine ina mshahara kidogo lakini una uhuru mkubwa wa kufanya mambo yako mengine, chagua ile inayokupa uhuru mkubwa na tumia uhuru huo kujijengea umiliki.
- Badili hali mbaya kuwa fursa nzuri. Kila hali hasi ina fursa nzuri ambazo unaweza kuzitumia kuboresha maisha yako zaidi, inategemea wewe unaichukuliaje hali hiyo. Kukosa kwako rasilimali au mtaji wa kuanza kitu ndiyo kunatakiwa kukusukuma wewe kutumia chochote ulichonacho ili kuanza. Kushindwa kwenye pambano ni fursa ya wewe kujiandaa huku wengine wakikuchukulia huwezi. Kila hali mbaya unayopitia angalia ni kipi kizuri unachoweza kukitumia, na lazima utakiona. Usiishie kulalamika na kulaumu, angalia hatua ya kuchukua.
- Mambo yanayotokewa kwenye dunia siyo mazuri wala mabaya, bali tafsiri yetu ndiyo inachagua kuyaona ni mazuri au mabaya. Mambo yanayotokea kwenye dunia yanatokea kwa asili na hayajali wewe unachukuliaje. Wakati mwingine maisha yanaweza kuonekana magumu sana. Unaweza kukazana kutafuta fedha na wakati huo huo kuna mwingine anapambana kukuibia, au hali fulani inatokea na unashindwa kuendelea. Unatakiwa kujua kwamba mambo usiyoyapenda yatatokea na hivyo kujiandaa kuyatumia kama fursa ya kusonga mbele zaidi.
- Jua ni wakati gani wa kuwa mbaya, kuna wakati unahitaji kutumia shari ili kuweza kupata kile unachotaka, au kuwapa watu funzo fulani. Kwa chochote kile unachofanya, kuna watu ambao wanajaribu kukuzuia au kukurudisha chini, kuna watu ambao wapo tayari kukuzuia wewe usipate kile ambacho unakipigania. Kuna wakati unahitaji kutumia shari kulazimisha upate kile ambacho umekuwa unakipigania. Au kuwafanya watu waondoke kwenye njia yako ya kuelekea kwenye mafanikio.
- 50 Cent anasema kwamba alichojifunza ni yule mtoto ambaye hapendi kupigana shuleni ndiyo ambaye kila siku anapigwa. Na yule ambaye anakazana kukaa mbali na matatizo ndiyo ambaye matatizo huwa yanamwandama. Maisha ya binadamu ndivyo yalivyo, usipoweka mipaka ambayo huruhusu mtu avuke, kila mtu atakusumbua anavyotaka yeye. Lakini unapoweka mpaka, na kumwadhibu vibaya anayevuka mpaka huo, wengine wanajifunza na hawajaribu tena kuvuka mpaka ulioweka.
- Ongoza ukiwa mbele, kuwa na mamlaka. Kwenye kundi lolote, yule ambaye yupo juu ndiye ambaye anatengeneza sifa ya kundi zima. Kama aliye juu ana hofu na hachukui hatua basi kundi zima linakuwa na sifa hiyo. Kama aliye juu anachukua hatua na kujituma sana basi kundi zima linakuwa hivyo. Kama kuna watu wako chini yako, labda umewaajiri au unawasimamia, chochote unachotaka wafanye, kuwa mfano. Anza wewe kufanya na wao watafanya tu. Kama unataka watu wawahi kazini, anza wewe kuwahi na wahi kila siku, utaona nao wanafuata. Kama unataka watu waweke juhudi anza wewe kuweka juhudi. Tabia yoyote utakayokuwa nayo ndiyo walioko chini yako watakuwa nayo. Jiamini, jitume, fanya maamuzi muhimu na jiwekee viwango vya juu na wengine watafuata.
- Kuwa kiongozi maana yake unahitaji kufanya maamuzi magumu, unahitaji kuwashawishi watu wafanye vitu ambavyo hawapo tayari kufanya. Kama utachagua kuwa legelege na kutaka kumridhisha kila mtu ili upendwe, utajikuta inakuwia vigumu kwako kuongoza wengine, na mbaya zaidi watakuchukia. Kama utajijenga sifa ya kuwa mtu wa vitendo na kuleta matokeo bora, watu wanaweza wasikupende, lakini watakuheshimu kwa matokeo bora unayoleta.
Hofu ndiyo adui mkubwa sana wa mafanikio yetu. Na mapambano ya hofu yanaanza na sisi wenyewe kwa kujijua vizuri, kujua ni kipi tunataka na changamoto zinazotuzuia. Hapa tunaamua kuchukua hatua na kutokurudi nyuma. Amua leo kushika hatamu ya maisha yako na kuweka juhudi kupata kile ambacho unakitaka, amua kumiliki kile unachofanya na kumiliki muda wako. Na onesha kwa mfano kile ambacho unataka wengine wafanye.
Fanyia kazi haya uliyojifunza, ili uweze kuondokana na hofu na kuchukua hatua ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.
Kila la kheri.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Asante.
LikeLike