Mtoto mdogo wa miaka mitatu, ambaye ndiyo kwanza amejua kuongea, akiangalia unachofanya na kukuambia huwezi kufanya kitu hiko au utashindwa unamchukuliaje?
Hutampa uzito sana, kwa sababu unajua bado ni mtoto na hajui lile analolisema. Utamchukulia ni mtu ambaye hajui hata kitu chenyewe kinafanywaje ila amejisikia tu kusema hivyo. Kauli hiyo ya mtoto haitakufanya hata uanze kufikiria mara mbili kuhusu unachofanya.
Lakini inapotokea mtu mzima amekuambia maneno hayo hayo ambayo mtoto mdogo amekuambia unachukuliaje? Unaanza kuyapa uzito, unaanza kufikiria mara mbili kuhusu maamuzi uliyofanya na hapa unafikia kuchukua maamuzi ambapo unaweza kuchagua kuacha kile unachofanya, au kujaribu kumwelewesha mtu huyo akuelewe kile unachofanya.
Kwa bahati mbaya sana huwa hatuchimbi mbali na kutaka kujua uelewa hasa wa watu hawa ambao wanatuambia maneno ya kukatisha tamaa, ambao hawajaelewa kile tunachofanya. Kwa sababu ni watu wazima, moja kwa moja tunachukulia ya kwamba wanajua na wana uhakika na wanachosema. Kitu ambacho siyo kweli kabisa.
Angalia kwa undani zaidi kwa mtu yeyote anayekuambia kitu cha kukukatisha tamaa, wengi hawana tofauti na mtoto wa miaka mitatu, inapokuja kwenye jambo kubwa unalofanya. Hawajui ila wanahofu ambazo wanataka na wewe uwe nazo. Ukishajua hivi utachukulia kama ulivyochukulia kwa mtoto, kuendelea na kile unachofanya.
Kuna watu ambao hawatakuelewa kwa kile unachofanya, lakini watahakikisha wanakupa maoni yao. Usikubali watu hawa wakurudishe nyuma, hasa pale ambapo wanajua ni wapi unakosea, ila hawajui ni njia ipi utumie kuepuka makosa hayo na kufanikiwa. Kujaribu kuwaelewesha watu wa aina hii ni kupoteza muda wako maana hawatakuelewa.
SOMA; Sababu 5 Kwa Nini Ni Marufuku Wewe Kukata Tamaa.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba siyo watu wote watakaonielewa kwa maisha ya mafanikio ambayo nimechagua kuishi. Na hivyo nimeamua kuacha kujaribu kumwelewesha kila mtu na badala yake naweka juhudi kwenye kile ninachotaka kufikia. Sikubali asiyejua anirudishe nyuma kwa hofu zake.
NENO LA LEO.
Watu wengi hawatakuelewa pale unapoamua kufanya mambo makubwa, ambayo yatakufikisha kwenye mafanikio makubwa. Lakini watu hawa ndio watakuwa wa kwanza kukukatisha tamaa na kukupinga.
Wachukulie watu hawa kama watoto ambao bado wanajifunza na hivyo waache wajifunze taratibu. Kujaribu kumwelewesha kila mtu ni kupoteza muda ambao ungeweza kuutumia kuboresha kile unachofanya.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.