Tunaishi kwenye wakati ambao kuna usumbufu mkubwa sana. Ni vigumu kuweza kupata utulivu wa kuweza kufanya kazi zako kwa ufanisi. Na usumbufu huu unaanza na sisi wenyewe kutokana na vifaa vya kiteknolojia tunavyotumia.

Simu za mkononi za kisasa zina uwezo wa kufanya mambo mengi na hizi zimekuwa chanzo kikubwa cha usumbufu. Kwa simu hizi kuweza kuingia kwenye mtandao, tunapata usumbufu kupitia mtandao na mitandao ya kijamii. Imekuwa ni vigumu sana mtu kuweza kukaa muda mrefu kwa utulivu bila ya kuanza kugusa simu yake na kuangalia ni nini kinaendelea. Na kama mtu atajaribu kujipa muda bila ya kuangalia, anaona kama kuna kitu kikubwa anakosa, kama anapitwa.

Kwa usumbufu huu ni vigumu sana kufanya kazi ya maana. Na hivyo tunahitaji dawa ya kuondokana na hali hii. Ambayo tutaipata hapa leo.

Dawa ni kujiwekea kikomo, kwa jinsi tunavyoishi sasa na simu zetu ni kama hatuna ukomo. Tukiamka tunashika simu na kuangalia, siku nzima tunaiangalia na hata inapofika wakati wa kulala tunakwenda nayo kitandani, tunaendelea kuiangalia mpaka usingizi utuingie. Na ili kuhakikisha hatukosi hata sekunde moja, tuna vifaa vya kutunza chaji za simu hizi (power bank), ili inapoisha tu tunaongeza chaji hata kama hatupo karibu na umeme.

Dawa ni kujiwekea kikomo, usijipe uhuru wa kuperuzi mtandao kila muda wa siku yako. badala yake jitengee muda maalumu ambao utaperuzi mitandao kwa siku. Na muda huu uwe ni baada ya wewe kufanya kazi yenye maana. Na pia usiwe muda mrefu, hivyo uangalie yale ambayo ni muhimu kwako tu. Kwa muda mwingine zima kabisa mtandao kwenye simu yako na weka mawazo yako na juhudi zako kwenye kuzalisha kazi yenye maana kwako na kwa wengine.

Mwisho wa siku tutakuangalia kwa kipi umezalisha, siyo kwa wingi kiasi gani umetembelea mitandao ya kijamii au kujibu jumbe za watu. Jiwekee kikomo kwenye mitandao ili upate muda bora wa uzalishaji.

Na kuhusu mitandao ya kijamii, kama kuna mtandao wa kijamii umezoea sana kuutumia, lakini hauna mchango wowote kwako na kwenye kazi unayofanya, basi acha kutumia mtandao huo, unakupotezea muda.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; EAT THAT FROG, JINSI YA KUPANGILIA MUDA WAKO NA KUEPUKA TABIA YA KUAHIRISHA MAMBO.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba usumbufu wa mitandao unanirudisha nyuma kwenye kufikia malengo yangu. Nimeijua dawa ya usumbufu huu ni kujiwekea kikomo katika kutembelea mitandao hii. Nitatenga muda maalumu na mchache wa kutembelea mitandao hii. Na muda mwingine nitaweka akili yangu kwenye kazi zangu. Kwa ile mitandao ya kijamii ambayo haina manufaa kwangu nitaacha kuitumia.

NENO LA LEO.

Simu zetu na mitandao ya kijamii, ni usumbufu mkubwa kwa sasa kwenye ufanyaji wa kazi yenye maana. Ni vigumu kuweka akili yako kwenye kazi huku upo kwenye mitandao.

Dawa ya usumbufu huu ni kutenga muda maalumu na mchache wa kutembelea mitandao, muda mwingine zima mitandao na weka akili yako kwenye kazi unayofanya. Na kwa ile mitandao ambayo haina manufaa kwako, acha kuitumia.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.