Watu wengi wanaishi maisha yao yote bila ya kujijua wao wenyewe. Hawajui uwezo mkubwa ulio ndani yao na wanaondoka kwenye dunia hii wakiwa bado hawajatumia uwezo wao huo.
Kwa kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, au ulichochagua kufanya lakini unafanya kwa hali ya kawaida, huwezi kujijua wewe mwenyewe. Unaishia kufanya kile ambacho tayari unakijua na kupata matokeo yale ambayo unatarajia kupata.
Ni pale unapofanya zaidi ya kawaida ndipo unapojijua wewe ni nani. Ni pale unapojisukuma zaidi ya ulivyozoea ndipo unajua uwezo mkubwa uliopo ndani yako. Ni pale unapofanya kile ambacho hujawahi kufanya na huna uhakika wa kushinda ndipo unapojua kwamba uwezo unao mkubwa.
Mara nyingi siyo rahisi mtu kuweza kufanya mwenyewe, kwa sababu ya hofu. Wale wachache wanaokutana na hali ngumu ambapo hawana namna nyingine ndiyo wanalazimika kufanya na hapa ndipo wanapogundua ya kwamba walikuwa wanaweza ila hawakuwa na uthubutu wa kuchukua hatua.
Rai yangu kwako ni mara kwa mara ufanye zaidi ya kawaida. Kwamba kwa kawaida huwa unafanya kwa kiwango fulani, basi jaribu kwenda mbali zaidi, nenda hatua ya ziada. Hii ni kwenye kazi, biashara na hata maisha yako ya kawaida. Na ni kwa mambo yote yanayohusisha kazi na hata mahusiano yako na wengine.
Usiishie tu kufanya kile ambacho umezoea kufanya, au kile ambacho kila mtu anafanya, angalia ni kipi kinaonekana ni kigumu kwako lakini kina maslahi makubwa na anza kukifanya. Uwezo wetu ni kama mpira, unaongezeka kadiri unavyovutwa. Jivute zaidi ili kuongeza uwezo wako zaidi.
SOMA; Vitu vinne vinavyochangia thamani na kipato cha biashara yako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba ili niweze kujijua mimi mwenyewe na kuweza kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yangu ni lazima nifanye zaidi ya kawaida. Nisiishie tu kufanya kama nilivyozoea kufanya au kama wengine wanavyofanya, bali nitafute kufanya zaidi. Nitaangalia yale ambayo nimekuwa naona ni magumu kufanya lakini yana maslahi na nitayafanya.
NENO LA LEO.
Watu wengi wanakuja duniani na kuondoka bila ya kujijua wao wenyewe na kujua uwezo mkubwa ambao upo ndani yao. Hii inasababishwa na watu kufanya mambo kwa mazoea na kufanya yale ambayo kila mtu anafanya.
Kama unataka kujijua kwa undani na kuweza kufikia uwezo wako mkubwa, fanya zaidi ya kawaida. Angalia ni mambo gani umekuwa unaona ni magumu lakini yana maslahi na anza kuyafanya, utajijua na kuweza kutumia uwezo wako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.