Moja ya tofauti ya wajasiriamali na wafanyabiashara ni kwenye faida. Wafanyabiashara wanaongozwa na faida pekee, yaani wao wanaangalia ni kipi chenye faida na hivyo kukifanya. Lakini wajasiriamali wapo tofauti kidogo, wao hawaangalii faida pekee, bali wanaangalia mchango wanaoutoa kwa wengine. Wajasiriamali wanaangalia ni kipi ambacho kinakosekana na wanatafuta njia ya kuwapatia watu kile wanachokikosa. Kwa njia hii wanaboresha maisha wa wengine na kupata faida pia.
Leo kupitia makala hii ya KONA YA MJASIRIAMALI tutakwenda kuangalia jinsi ya kubadili na kuboresha mtazamo wetu juu ya faida na maendeleo ya biashara zetu. Uhitaji wetu wa faida umekuwa mkubwa sana kiasi cha kuingilia ubora ambao tunatoa kupitia biashara tunazofanya. Hivyo tunahitaji kufanya mabadiliko ya kimtazamo ili kuweza kujua kipi muhimu na kipi ni matokeo.
Faida siyo dhumuni kuu la biashara yako.
Japokuwa unafanya biashara ili upate faida, lakini usifanye hii kuwa ndiyo dhumuni kubwa la biashara yako. Kwa sababu kwa kufanya hivi, utazidi kukosa faida. Kila mtu anajua ni jinsi gani ambavyo biashara zimekuwa na ushindani, biashara yoyote unayoifanya kuna wengine wengi pia wanaoifanya. Na kama ni bei wengi wapo tayari kushusha bei na kutengeneza angalau faida kidogo tu. Hivyo kuangalia upande wa faida pekee, utajikuta ukikazana kushusha bei ili angalau uendane na wengine.
Dhumuni sahihi la biashara yako, ambalo ukilifanyia kazi litaboresha biashara yako ni kutengeneza wateja. Na unatengeneza wateja kwa kuangalia ni kitu gani ambacho wanakihitaji sana ila hawakipati na wewe ukawa tayari kuwapatia. Unaangalia watu wana maumivu gani na wewe unawaletea suluhisho la maumivu yao. Utafanya hivi kwa njia ambayo utapata faida, lakini faida siyo msukumo wako. Utasukumwa zaidi na kile ambacho unawapatia wengine. Na wateja wako watajua kama kweli unajali kuwapa kile wanachotaka au unataka tu kutengeneza faida. Ukiweza kutengeneza uhusiano mzuri na wateja wakajua wanaweza kuboresha maisha yao kupitia wewe, itakuwa rahisi kwao kuwaambia wengine na hivyo ukaongeza wateja zaidi.
Kwa kubadili mtazamo wako juu ya dhumuni la biashara yako, utaweza kutoa huduma bora sana kwa wateja wako. Pia utaweza kutatua changamoto ambazo wateja wako watakutana nazo kupitia biashara unayofanya. Utaweza kuzioa fursa zaidi za kuwasaidia wateja wako na kwa njia hii utaongeza nafasi za kutengeneza faida. Lakini kama utaangalia faida pekee, utaona njia nyingi za kumuumiza mteja. Wateja wataliona hilo na kutafuta mtu mwingine wa kufanya naye biashara.
Faida ni matokeo ya kuwa na wateja bora.
Japokuwa faida siyo dhumuni lako kuu kwenye biashara yako, lakini utaipata nyingi sana pale utakapobadili mtazamo wako juu ya biashara yako. Hii ni kwa sababu faida ni matokeo ya huduma bora unazotoa kwa wateja wako. Faida ni matokeo ya kuwa na wateja walioridhishwa na kile unachokifanya na kuwa tayari kukulipa kile unachohitaji wakulipe. Unapoiweka faida pale inapostahili, kwamba ni matokeo ya kutoa huduma bora kwa wateja wako, utajua mbinu bora za kuongeza faida yako.
Kwa mfano kama unachukulia lengo la biashara yako ni kupata faida pekee na ikatokea hupati utaangalia ni njia zipi za kuongeza faida yako. na hapa utakuja na hatua z akuchukua kama kuongeza bei, kupunguza ubora na nyingine kama hizi ambazo zinamuumiza mteja moja kwa moja na hivyo unakuwa kwenye hatari ya kumpoteza mteja wako. Lakini unapokuwa unachukulia dhumuni la biashara yako ni kutengeneza wateja wanaoridhishwa na faida ni matokeo, inapotokea hupati faida, utajua moja kwa moja kuna kitu ambacho wateja hawakipati. Na hapa utakitafuta na kukijua ili kuimarisha zaidi biashara yako na hivyo kuwa bora zaidi.
Mtazamo sahihi kwenye biashara yako ni muhimu kama unataka kuikuza na kupata mafanikio. Anza sasa kujenga mtazamo sahihi kuhusu wateja na faida, ili uweze kutengeneza wateja wa kudumu kwenye biashara yako na ambao watakuwezesha kupata faida kubwa. Fanyia kazi mtazamo huu kwenye biashara yako na utaona matokeo bora.