Lengo la kila mmoja wetu ni kufanikiwa, kuwa bora zaidi ya tulivyo sasa na kufikia hatua ambazo kwa sasa bado hatujazifikia. Lakini kama kwenye kila kitu unachofanya unafanikiwa, kama kila lengo unaloweka unalifikia ni hatari kubwa sana.
Unaweza kushangaa kwa nini iwe hivyo, kama kweli utaweka juhudi na kufikia kile unachotaka kuna hatari gani. Lakini ukweli unabaki kwamba kuna changamoto nyingi kwenye safari ya mafanikio, na hakuna anayeweza kuzivuka changamoto zote hizo. Na kadiri malengo yanavyokuwa makubwa ndivyo changamoto hizi zinavyokuwa kuwa kubwa.
Kwa hiyo kama unafikia kila lengo unalojiwekea kwa asilimia 100 kuna uwezekano mkubwa kwamba unajiwekea malengo ambayo ni madogo sana. Unajiwekea malengo ambayo tayari ulishayafikia huko nyuma hivyo unaendelea tu kuyafikia. Lakini unapoweka malengo makubwa, ambayo hujawahi kuyafikia, utakutana na changamoto.
Nakushirikisha hili ili tujikumbushe kuyaangalia malengo yetu vizuri. Kwa sababu kwa kufikia kila malengo unaweza kuwa unajidanganya na ukawa unarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Ili uweze kwenda mbele unahitaji malengo ambayo yatakusukuma, ambayo yatakuhitaji ubadili aina ya maisha uliyonayo sasa.
Kama umeweka malengo na unayafikia bila ya kubadili chochote kwenye maisha yako, hayo siyo malengo makubwa, bali ni kurudia kufanya kile ambacho umezoea kufanya.
Tunahitaji kuweka juhudi kubwa kufikia malengo yetu, lakini kufikia kila lengo kwa asilimia 100 ni hatari kubwa na dalili kwamba hakuna hatua kubwa tunazopiga.
Lakini pia hili lisikufanye ujiwekee malengo makubwa sana ambayo yatakukatisha tamaa. Pia lisikufanye ubweteke na kuona kutokufikia malengo ni kitu kizuri. Bali likupe hamasa ya kuweka malengo ambayo unajua yatakusukuma zaidi na unaposhindwa unajifunza zaidi.
SOMA; Umuhimu wa changamoto kwenye maisha yako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kufikia kila lengo ninalojiwekea ni hatari kubwa sana kwangu. Hii ni kwa sababu kuna changamoto nyingi kwenye kufikia malengo na malengo yanavyokuwa makubwa changamoto nazo zinakuwa kubwa. Kufikia kila lengo ni dalili kwamba malengo hayo ni madogo. Nitajiwekea malengo ambayo yananisukuma na nitakaposhindwa najifunza.
NENO LA LEO.
Kama unafanikiwa kwenye kila jambo unalofanya upo kwenye hatari kubwa.
Kama unafikia kila lengo unalojiwekea upo kwenye njia ya kupotea.
Mafanikio yoyote yana changamoto zake, hivyo kama wewe hukutani na changamoto inawezekana umejiwekea malengo madogo sana ambayo hawatakufikisha mbali.
Jiwekee malengo yatakayokusukuma na ambayo ukishindwa utajifunza zaidi. Tunajifunza zaidi kwenye kushindwa kuliko kushinda.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.