Kuna watu hawapendi kusikia neno utajiri, yaani ni kama wana ‘allergy’ na neno hilo. Na siyo jambo la kushangaza kwa sababu ukiweka mambo ya kijamii na kidini pia, kuna mkanganyiko mkubwa.

Wengine watakuambia siyo kila mtu anaweza kuwa tajiri, kwa hiyo wanachagua wao kuwa upande wa masikini. Wengine watakuambia masikini hawataisha mahali popote, na hivyo wanakuwa wamechagua kuwa upande wa masikini. Ninaamini kama unaweza kujua haya basi unahitaji kuwa tajiri.

Kwa kifupi naamini kila mtu anapaswa kuwa tajiri. Ndiyo wewe unapaswa kuwa tajiri ili uweze kuishi maisha ya ndoto yako, maisha bora na yenye furaha. Lakini kabla hujaniambia wewe huwezi kuwa tajiri, nikupe maana halisi ya utajiri.

Maana halisi ya utajiri ni kuwa na uhuru wa kuchagua. Huu ndiyo msingi mkuu wa utajiri, uweze kuwa na uhuru wa kuchagua ni kipi unataka na kipi hutaki. Na hii haijalishi kama una ndege yako binafsi au huna.

Tunachohitaji kwenye haya maisha ni kuwa na uhuru wa kuchagua maisha yetu yaendeje. Na ndiyo ili uweze kupata uhuru huu ni lazima uwe na kiasi kikubwa cha fedha.

Kama una shilingi elfu tano kwa ajili ya kula kwa siku nzima huna uwezo mkubwa wa kuchagua kile unachotaka au usichotaka, badala yake utapata kile ambacho kinapatikana kwa kiasi cha fedha ulichonacho. Lakini unapokuwa na laki moja kwa ajili ya kula kwa siku, una nguvu ya kuchagua unataka kula nini au hutaki kula nini.

Kama unaumwa na una shilingi elfu hamsini, huwezi kuchagua ni matibabu gani upate, bali utapata yale yanayopatikana kwa kiasi hiko cha fedha ulichonacho. Lakini kama unaumwa na una milioni kumi ya dharura, unaweza kuchagua ni matibabu gani upate na uyapate wapi, hata nje ya nchi.

Swali litakuja, ni kiasi gani cha fedha unahitaji ili uwe tajiri? Na hapa hakuna jibu moja kwa watu wote, bali kila mtu ana kiasi chake. Jua kiwango chako ni kipi na fanyia kazi kukipata. Kikubwa unachohitaji ni kujitengenezea uhuru wa kifedha. Na kama bado hujui unawezaje kujitengenezea uhuru huu soma kitabu hiki; KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, bonyeza hayo maandishi kukipata.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kwenye maisha yangu nahitaji kuwa tajiri ili niweze kuwa na uhuru wa kuchagua. Kadiri ninapokuwa na kiasi kikubwa cha fedha ndivyo ninavyokuwa na uhuru wa kuchagua kile ninachotaka. Maisha bora ni yale ambayo mimi mwenyewe ninachagua ni kipi hasa ninachotaka. Ndiyo maana lazima niwe tajiri zaidi kwenye maisha yangu.

NENO LA LEO.

Maana halisi ya utajiri ni kuwa na uhuru wa kuchagua ni kitu gani unataka na kipi hutaki. Hivyo utajiri unaweza kuwa wa viwango tofauti kwa watu tofauti, ila kwa kila mtu lazima awe na uhuru wa kifedha ndiyo awe tajiri.

Jua ni kiasi gani cha fedha unachohitaji ili kuweza kuendesha maisha yako bila ya wasiwasi na hapo unakuwa tajiri, bila ya kujali unamiliki ndege yako mwenyewe au la.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.