Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Karibu kwenye kipengele chetu cha FALSAFA MPYA YA MAISHA ambapo tunashirikishana mbinu za kujenga falsafa ambayo itatuwezesha kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa. kile tunachotaka kinaanzia ndani yetu na tunapokuwa na falsafa imara tunaweza kujenga maisha imara.

Leo tunakwenda kuangalia kitu kimoja ambacho kimekuwa changamoto kwa wengi. Kitu hiki kimekuwa kinawazuia watu kuishi yale maisha wanayoyataka. Kimekuwa kinawapeleka kwenye changamoto ambazo zinawazuia kuwa na maisha ya furaha na mafanikio. Kitu hiki ni hisia, hisia zimekuwa zinatusumbua sana, hasa hisia ambazo ni hasi. Mtu yeyote ambaye anaongozwa na hisia zake hawezi kufanya maamuzi bora ya maisha yake.

Ni rahisi kusema dhibiti hisia zako, lakini kwenye utekelezaji ni jambo ambalo ni gumu. Leo tutaangalia kwa nini tunashindwa kudhibiti hisia zetu na hatua zipi za kuchukua ili kuweza kudhibiti hisia zetu.

Chimbuko la kuongozwa na hisia.

Kwa akili zetu binadamu, tuna mifumo miwili mikuu ya mawazo. Mfumo wa kwanza ni ule ambao unaongozwa na sehemu ya ubongo ambayo inahusika na hisia. Na mfumo wa pili ni ule unaoongozwa na sehemu ya ubongo inayohusika na kufikiri kwa kina.

Kwa asili yetu binadamu, sehemu inayohusika na hisia ni ya awali kabla hatujatengeneza uwezo wa kufikiri zaidi. Na pia mfumo wa hisia unachukua taarifa kwa kasi kuliko mfumo wa kufikiri. Kwa mfano wanyama wote wanaongozwa na sehemu zao za hisia. Swala anapomwona simba porini haanzi kufikiria ni njia gani rahisi kumkwepa simba bali anaanza kukimbia mara moja, hapo ndipo usalama wake ulipo.

Sasa na sisi binadamu tulikuwa tunaishi kwenye mazingira hatarishi kama haya miaka mingi iliyopita. Watu walikuwa wakiishi katika hali ndogo sana ya usalama na hivyo hisia zilikuwa sehemu muhimu ya kuweza kupona. Pale ambapo mtu alijikuta kwenye mazingira hatarishi, mfumo unaoongozwa na hisia unauandaa mwili kwa ajili ya kupambana au kukimbia. Mwili unapata nguvu kubwa sana kwa ajili ya kuhakikisha hatari ile haikudhuru.

Nafikiri umewahi kujikuta kwenye mazingira ya hatari na ukapata nguvu ambazo hukuweza kuelezea baadaye. Labda ulikuwa unakimbizwa na mbwa na ukajikuta umeruka ukuta ambao hukuweza kuuruka tena baadaye. Au mtu anakukasirisha na ghafla unaanza kutokwa na jasho na mwili kukutetemeka. Hii yote inatokana na jinsi ambavyo tumerithi kutoka kwa watangulizi wetu.

Kama mtu wa zamani angekutana na mazingira hatarishi, ambapo labda amepita kwenye kichaka na akasikia sauti asizozielewa, kuna mambo mawili angeweza kufanya, kuanza kukimbia haraka sana kwa kufuata hisia zake ili kujiokoa kwenye hali hiyo hata kama hana uhakika ni nini anachokimbia. Au angeweza kutumia fikra zake kuchunguza kwa makini ni sauti gani hizo alizosikia.

Sasa ukija kwenye faida na hasara za maamuzi yake ndipo utaelewa kwa nini ni hisia ni bora kuliko kufikiri. Kama mtu huyo ataamua kuacha kukimbia na kufikiri, faida ni kwamba anaweza asisumbuke kukimbia, lakini hasara ni kwamba anaweza kuliwa na mnyama mkali. Na kama mtu huyu ataamua kuanza kukimbia mara moja, faida ni kwamba ataokoa maisha yake na hasara ni kwamba atakuwa amejichosha kama haikuwa hatari kweli. Sasa kwa fikra za kawaida ni kipi bora, kukimbia hata kama huna uhakika kuokoa maisha yako, au kusubiri na mwishowe ukaliwa? Jibu lipo wazi.

Hivi ndivyo hisia zilivyopata nguvu na kuweza kuwa msingi mkuu wa watu kufanya maamuzi.

Mambo yamebadilika.

Sasa hivi tunaishi kwenye ulimwengu wa tofauti sana na walioishi watangulizi wetu. Tunaishi kwenye ulimwengu ambao usalama ni wa hali ya juu sana. Lakini bado tunatumia mfumo ule tuliorithi kutoka kwa watangulizi wetu. Bado tunafanya maamuzi yetu kwa kuendeshwa kwa hisia na mara nyingi tumekuwa tunafanya maamuzi ambayo siyo bora kwetu.

Tumekuwa tunafanya maamuzi tukiwa na hisia kali na baadaye hisia hizi zinapoisha tunajutia maamuzi ambayo tumeyafanya. Tumekuwa tukichukua hatua bila ya kufikiri kwa kina na baadaye tunaumizwa na hatua zetu wenyewe. Kusema tu kwamba nataka kudhibiti hisia zangu hakuwezi kukusaidia, unahitaji kuwa na hatua za kufuata pale unapojikuta kwenye hali ya kufanya maamuzi huku ukiwa na hisia kali.

Mambo ya kuzingatia ili kudhibiti hisia zako na kuepuka kufanya maamuzi mabovu.

  1. Usikimbilie kuchukua hatua, pumua.

Jambo lolote linapotokea, huwa tunakimbilia kuchukua hatua, au kuhukumu. Kama tulivyoona, mfumo wa hisia unachukua taarifa haraka kuliko mfumo wa kufikiri. Hivyo hatua yoyote utakayochukua kwa haraka, itakuwa inaongozwa na hisia. Unahitaji kujipa muda kuelewa kitu kabla hujachukua hatua. Hata kama ni mtu ameambia maneno mabaya, kabla hujakimbilia kumjibu, jipe muda kidogo na fikiri kwanza. Na kama unakuwa vigumu kwako kufikiri kutokana na hasira unazokuwa nazo basi pumua huku ukihesabu pumzi zako.

Moja ya njia za kujua kwamba upo chini ya udhibiti wa hisia zako ni kupumua haraka haraka na kwa juu juu, haya ni maandalizi ya mwili wako kuchukua hatua. Unapokuwa kwenye hali hii pumua taratibu na kwa kina. Hesabu pumzi zako kwa angalau dakika tano. Utaanza kuona mwili unapoa na kuona hali siyo mbaya kama ulivyokuwa unachukulia awali.

Usikimbilie kufanya maamuzi, jipe muda wa kufikiri kwa kina na utaona hatua bora kwako kuchukua.

  1. Tafuta njia ya kuondokana na hisia hasi.

Mara kwa mara huwa tunakutana na hisia hasi kwenye maisha yetu. Inawezekana hisia hizi zikatokana na kazi zetu, biashara zetu au hata wale wanaotuzunguka. Kitu kibaya unachoweza kufanya ni kujaribu kufukia hisia hizi, huwezi kuzifukia, zitaibuka tena na tena. Yaani unavyokazana kuzifukia ndivyo zinavyokazana kutoka nje. Jambo bora kufanya ni kutafuta njia ambayo unaweza kuitumia kuondokana na hisia hizo hasi. Inawezekana ikawa kusoma vitabu, au kusikiliza miziki fulani unayoipenda, au kuongea na watu fulani, au kuandika, au kufanya mazoezi. Pia inawezekana ikawa kwa kufanya tahajudi(meditation). Usiziache hisia hizi hewani, bali kuwa na njia ya kuziondoa kwenye akili yako ili uweze kufanya maamuzi bora kwako.

  1. Ona maana kubwa ya maisha yako.

Pale tunapokuwa tumezingirwa na hisia hasa zile hisia ambazo ni hasi, ni rahisi kuona kama dunia haina maana tena. Ni rahisi kuona kama hakuna namna unaweza kuendelea na kile unachotaka. Hali hii ndiyo inayopelekea wengi kukata tamaa na hata wengine kukatisha maisha yao. Unatakiwa kujua ya kwamba hata kama unapitia mambo magumu kiasi gani, siyo mwisho wa dunia. Unapaswa kujua ya kwamba maisha yako yataendelea na utapata kile unachotaka. Unachohitaji ni kumaliza salama kile kilichopo mbele yako, na baada ya kukimaliza utakuwa umejifunza zaidi.

  1. Kaa mbali na vishawishi vya hisia.

Kuna vitu mbalimbali kwenye maisha yetu ambavyo vimekuwa vinachochea hisia fulani hasa zile ambazo ni hasi. Vitu hivi vimekuwa ni vishawishi vya wewe kuingia kwenye hisia ambazo zinakupelekea kufanya maamuzi ambayo siyo mazuri kwako. Inawezekana vishawishi vyako ni watu fulani ambao ukikaa nao mazungumzo mnayofanya ni ya kukatisha tamaa, ya kuona kwamba mambo hayawezekani. Inawezekana vishawishi vyako ni pale unapoanza kufuatilia maisha ya wengine na kuona kwamba yako vizuri kuliko yako na hivyo kupata wivu. Angalia ni vitu gani kwenye maisha yako ambavyo vimekuwa vinakuletea hisia ambazo huzitaki na viepuke.

  1. Samehe.

Kwenye haya maisha watu watakuudhi, kukukasirisha na hata kufanya maamuzi ambayo siyo bora kwako. Kwa kuwa wanakuwa wameumiza hisia zako unaona ya kwamba unastahili kuwawekea kinyongo na kutowasamehe. Lakini hili linajenga hisia mbaya zaidi na hivyo kupelekea wewe kufanya maamuzi ambayo siyo mazuri. Samehe kwa jambo lolote ambalo limetokea kwako, haijalishi ni dogo au kubwa kiasi gani, samehe na utaipa akili yako uhuru wa kufanya maamuzi bora kwako.

Ni zoezi gumu kuweza kuzidhibiti hisia zetu, lakini ni kitu kinawezekana kama hatutakata tamaa katika kufanyia udhibiti wa hisia zetu. Tuepuke kufanya maamuzi yanayoongozwa na hisia pekee, na badala yake tujipe nafasi ya kufikiri kwa kina kabla ya kufanya maamuzi na kuchukua hatua.

Nakutakia kila la kheri.

Rafiki na kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz